MSEKWA ASEMA; HAONI SABABU YAKUWEPO NA KATIBA MPYA!!

Spika mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa akikusanya baadhi ya vitabu alivyoviandika  alipokuwa akifanya mahojiano na wahariri wa gazeti hili nyumbani kwake jijini Dar es Salaam jana.

Spika mstaafu, Pius Msekwa amesema haoni haja wala sababu ya msingi ya Tanzania kuandika Katiba Mpya kwa sasa kwani hakuna matukio makubwa ya kisiasa nchini yanayolazimisha kufanya hivyo.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake Oysterbay, Dar es Salaam jana, Msekwa alisema hata hivyo, anakubaliana na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete kuruhusu kufanyika kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa sababu alikuwa na sababu zake na alikwishazieleza wazi.
Alisema, “Sioni haja ya kuwa na Katiba Mpya. Mnatunga Katiba Mpya kama kuna mabadiliko makubwa ya kisiasa, yaani mabadiliko ya kiutawala,” alisema.
Alifafanua Katiba ya Tanganyika na hata ya Tanzania ilibadilishwa pale palipokuwa na matukio makubwa ya kiutawala, lakini pia kuna matukio mengine ambayo hayakulazimisha kuandikwa upya kwa Katiba.
Msekwa aliyeshiriki michakato yote ya katiba zilizotangulia ikiwamo hii ya sasa, alisema kwa kawaida Katiba Mpya inaweza kuandikwa panapokuwa na mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini kama ilivyotokea mwaka 1962 baada ya Tanganyika kupata uhuru wake, lakini Malkia wa Uingereza akaendelea kuwa mkuu wa nchi.
“Katika mazingira hayo Watanzania hawakujua maana ya uhuru ni nini, ikaleta sintofahamu, ikabidi Mwalimu (Julius Nyerere) na wenzake waamue kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa kutoka kuwa chini ya Malkia kwenda kwa uongozi wa wananchi,’’ alisema.
Pia, alieleza kuwa kuanzishwa kwa Muungano baina ya Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964 na kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lilikuwa tukio jingine kubwa na la msingi lililosababisha kuandikwa kwa Katiba Mpya ya mwaka 1977.
“Mfano wa pili tulipoingia katika Muungano mwaka 1964, hapa kulikuwa na nchi mbili ambazo ni sovereignty (nchi zenye utawala kamili) tukaziunganisha, mazingira kama hayo yalidai Katiba Mpya.
Hata hivyo, Msekwa alisema hata mabadiliko kama ya mwaka 1965 kutoka mfumo wa vyama vingi vya siasa kuingia chama kimoja licha ya kuwa tukio kubwa, hayakulazimisha kuandikwa kwa Katiba Mpya, bali iliyokuwepo ilifanyiwa marekebisho.
Alisema tukio jingine ni la mwaka 1984 ambako mabadiliko mengine yalifanyika katika Katiba kwa kuingiza kipengele cha haki za binadamu na ukomo wa kipindi cha urais kuwa wa vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja ambalo halikuhitaji Katiba Mpya.
Badiliko jingine kubwa ambalo halihitaji katiba mpya, Msekwa alisema ni lile la mwaka 1992 la kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini … “Tuliporejea mfumo wa vyama vingi hatukutunga katiba kwa kuwa haikuwa lazima. Unaondoa vile vifungu vinavyoondoa chama kimoja na vingine vinaendelea kama kawaida.
Kwa hiyo hata sasa hakuna haja ya kuandika Katiba Mpya, kitu chochote kinachotakiwa kingeweza kuingizwa katika Katiba iliyopo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment