Thursday, 18 September 2014

WASSIRA ASEMA; MUUNGANO TULIOKUWA NAO SI UTAJIRI!!

 

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Bw. Stephen Wassira (pichani), amesema Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umejikita katika misingi ya kidugu si utajiri.

Bw. Wassira aliyasema hayo Mjini Dodoma juzi akizungumzia madai ya baadhi ya watu waliodai Muungano uliopo uvunjike kwani una gharama kubwa na umeegemea upande mmoja.

Alisema kuungana kwa nchi hizo hakukutokana na utajiri wa nchi mojawapo bali ulifanywa na waasisi kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi hizo ndio maana umejikita kindugu zaidi.

"Wanaodhani upande mmoja unanyonywa, hawaitendei haki Tanzania ambayo imejikita katika misingi ya undugu na kuzaa amani na utulivu uliodumu hadi sasa," alisema.

Alisema amani na utulivu ni sehemu ya mafanikio ya Muungano ambapo wananchi wa nchi hizo, wanafanya shughuli zao kwa amani, utulivu na ushirikiano mkubwa ndio maana leo hii, kila Mtanzania ana haki ya kufanya shughuli zake eneo lolote ilimradi havunji sheria au Katiba ya nchi.

"Huwezi kusema gharama zinazotumika katika Muungano ni kero, tunapaswa kuangalia mambo kwa misingi ya kujenga nchi si kubomoa, nawaomba baadhi ya wabunge wachunge ulimi wao kwani nchi nyingi zimeingia katika machafuko kwa kauli kama hizo," alisema.

Alikemea tabia ya baadhi ya Watanzania wakiwemo wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kutoa kauli zinazoweza kuwagawa wananchi kwani mataifa mengi duniani, yanatamani Muungano uliopo.

No comments:

Post a Comment