MADIWANI MOSHI WAMJIA JUU MKURUGENZI ATUHUMIWA KUPORA ENEO LA UWANJA!!
Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi Bw. Shaaban Ntarambe.
SAKATA la kiwanja
kilichopo Kata ya Mawenzi Manispaa ya Moshi, chenye L.O.Na. 9850,
limechukua sura mpya, baada ya kikao cha Baraza la Madiwani la Manispaa
hiyo kuvunjika, wakimtuhumu Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Shaaban
Ntarambe, kuhusika na uporaji wa eneo hilo.
Kikao hicho cha Baraza
kilichoanza saa 4:30 asubuhi,kilifunguliwa kwa sala; na Mkurugenzi
kumkaribisha Mstahiki Meya kufungua kikao, ndipo diwani wa Kata ya Rau,
Peter Kimaro, aliposimama na kuomba kutoa hoja.
Akitoa hoja, Kimaro
alisema moja ya majukumu ya madiwani ni kulinda na kutetea mali za
wananchi ikiwemo viwanja; na taarifa walizonazo, ni kwamba Mkurugenzi wa
Halmashauri hiyo, ameshiriki uporaji wa kiwanja cha kata ya Mawenzi na
kwamba ameondoa kwa siri zuio lililowekwa na baraza hilo bila madiwani
kushirikishwa.
“Mkurugenzi amedharau
agizo la baraza na kuagiza wataalamu wake kutengeneza kwa siri,hati ya
kiwanja hicho kwa watu binafsi," alisema.
Kimaro aliongeza kuwa
ni muhimu kukaundwa timu itakayohusisha watendaji wa Halmashauri na
madiwani, ili kuchunguza sakata hilo na kulipatia ufumbuzi, ikiwa ni
pamoja na kuwachukulia hatua wale wote ambao walihusika katika
kukihujumu kiwanja hicho.
Baada ya kauli hiyo ya
Kimaro baadhi ya madiwani walisimama na kuanza kupiga kelele, huku
wakitamka kuwa; "Tutoke hatumtaki mkurugenzi huyu... anahujumu mali za
umma."
Wakati madiwani hao
wakitoa maneno hayo walikuwa wakitoka nje na kuwaacha Watendaji, baadhi
ya madiwani wa CCM pamoja na Meya ambaye ni mwenyekiti wa Kikao na
Mkurugenzi ambaye ni katibu.
Hali hiyo ilisababisha
kikao hicho cha bajeti kuvunjika, huku mkurugenzi wa Halmashauri
akilalamikia kuvunjwa kwa kanuni na sheria za uendeshaji wa vikao vya
baraza la madiwani, jambo ambalo lilipingwa vikali na mwenyekiti wa
kikao hicho, Jaffari Michael, kwa madai kuwa kikao hicho kilikuwa
hakijafunguliwa.
Akizungumza mara baada
ya kuvunjika kwa kikao hicho Mstahiki Meya wa halmashauri hiyo, Michael,
alisema kuna hoja ya msingi iliyosababisha madiwani kuvunja kikao
hicho,kutokana na kwamba wapo kwa masilahi ya wananchi.
Meya alisema anaungana
na madiwani wenzake kuamua kususia kikao hicho kutokana na kuwepo kwa
tatizo la kupuuzwa maazimio mengi ambayo yamekuwa yakipitishwa na baraza
la madiwani na ofisi ya Mkurugenzi, jambo ambalo wanaona ni dharau.
“Kuna hujuma dhidi ya
kiwanja hicho, kwani haiwezekani hatimiliki ya eneo hilo ikamilike ndani
ya wiki moja, huku Mkurugenzi akienda kwa siri kwenda kuondoa zuio
lililowekwa na baraza la madiwani bila kurudi kutushirikisha, hali hii
inatufanya tuamini kuwa, kuna mazingira ya rushwa katika sakata hili,”
alisema Meya.
Mstahiki Meya alisema,
amefanya jitihada mbalimbali kushughulikia sakata hilo bila mafanikio,
hivyo kuviomba vyombo husika kuingilia suala hilo na kufanya uchunguzi
ili kuweza kulipatia ufumbuzi.
Kwa upande wake
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji katika Halmashauri hiyo,Raymond
Mboya, alikiri kamati hiyo kutoshirikishwa, katika mchakato wa utoaji
hati ya kiwanja hicho, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za mipango
miji.
Alisema kiwanja hicho
kiliwahi kuvamiwa na kujengwa, lakini baraza la madiwani liliagiza
pavunjwe, agizo ambalo lilitekelezwa na mkurugenzi,hivyo hawako tayari
kuona tena eneo hilo likivamiwa.
Hata hivyo, mkurugenzi
wa Manispaa hiyo alipofuatwa na waandishi wa habari ofisini kwake ili
kutoa ufafanuzi kuhusiana na sakata hilo, aligoma na kuomba wanahabari
kuonana naye leo kwa kuwa ameitwa kwenye kikao na mkuu wa mkoa huo.
No comments:
Post a Comment