RUSHWA INASHUSHA MAADILI YA VIONGOZI NCHINI-SUMAYE.
WAZIRI Mkuu mstaafu,
Bw. Federick Sumaye (Picha na Maktaba)
WAZIRI Mkuu mstaafu,
Bw. Federick Sumaye, amesema vitendo vya kuomba na kupokea rushwa
vinavyofanywa na baadhi ya viongozi na watendaji wa idara za umma,
binafsi nchini, vinaporomosha maadili ya viongozi hao na watendaji
husika.
Bw. Sumaye aliyasema
hayo juzi katika mdahalo maalumu wa kitaaluma uliolenga kuchochea
mageuzi ya taaluma kupitia mitandao ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha
Askofu Mihayo Tabora (AMUCTA) kupitia kitivo chake cha Mahusiano ya
Umma.
Alisema watu
wanaotafuta uongozi kwa kutoa rushwa, hawana maono wala dira ya kile
ambacho watakifanya maada ya kuingia madarakani na ufanisi wao katika
kutekeleza jukumu ambalo watapewa utakuwa mdogo kwa sababu
watakachoangalia ni maslahi binafsi kwanza.
Aliongeza kuwa, rushwa
ni tatizo kubwa katika nchi nyingi duniani ambayo inachangia kuharibu
utendaji wa viongozi wengi, kuvuruga amani na utulivu wa Mataifa
mbalimbali.
"Viongozi wengi
wanaotafuta madaraka hutumia pesa nyingi na wakipata madaraka, hufikiria
namna ya kurudisha pesa zao kwanza badala ya kuwatumika wananchi.
"Kimsingi viongozi
wanaoingia madarakani kwa rushwa hawawezi kupambana na rushwa wala
kuwakemea viongozi wenye tabia hiyo," alisema Bw. Sumaye ambaye anatajwa
kuwa miongoni mwa viongozi wastaafu mwenye nia ya kutaka kuwania urais
katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Alisema kupambana na
rushwa kunahitaji viongozi waadilifu, wasiotanguliza masilahi binafsi,
wenye dira ambapo kiongozi anayeweza kupambana na rushwa ni yule
asiyekuwa na hulka ya kutoa rushwa.
"Tunahitaji viongozi wenye dhamira ya kupambana na rushwa, kuikemea na kusimamia dhana ya utawala bora," alisema.
Akizungumzia rasilimali
za nchi, alisema Tanzania ni moja ya Mataifa kadhaa duniani
iliyobahatika kuwa na rasilimali nyingi zenye utajiri mkubwa lakini watu
wake ni maskini kutokana na kukosekana wasimamizi wazuri wa rasilimali
hizo na uwepo wa viongozi wanaojali maslahi binafsi.
"Tanzania ina utajiri
mwingi kama madini, mbuga za wanyama, mlima Kilimanjaro, mito, maziwa na
misitu...cha ajabu utakuta watu wanakata misitu ovyo na kuondoa uoto wa
asili, kuchoma moto misitu, kufanya biashara haramu ya mbao na mkaa,
hali hii inachangiwa na usimamizi mbovu wa rasilimali hizo.
Alisema wingi wa rasilimali zilizopo nchini hauendani na maisha anayoishi mwananchi bali watu wachache ndio wanaonufaika.
No comments:
Post a Comment