MAREFA SIMBA, YANGA WAZOA MILIONI MOJA!!
SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA!!
UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA!
PATA TAARIFA KAMILI:
Release No. 181
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 22, 2013
NASSIB AWAZAWADIA MAREFA SIMBA, YANGA
Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Ramadhan Nassib ametoa sh. milioni moja
kwa waamuzi waliochezesha mechi ya Simba na Yanga iliyochezwa wikiendi
iliyopita jijini Dar es Salaam.
Nassib ambaye alichaguliwa katika nafasi
hiyo akiwakilisha klabu amesema ametoa fedha hizo ili kuwapongeza
waamuzi hao kwa kuchezesha vizuri mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya
mabao 3-3.
“Waamuzi wanapofanya vibaya
tunawaadhibu, hivyo wakifanya vizuri wanastahili kupongezwa pia.
Vilevile kuwapongeza ni kuwaongezea ari ya kuchezesha vizuri zaidi,”
amesema.
Israel Nkongo ndiye aliyeongoza jopo
hilo ambapo mwamuzi msaidizi namba moja alikuwa Hamis Chang’walu wakati
namba mbili alikuwa Ferdinand Chacha. Mwamuzi wa mezani alikuwa Oden
Mbaga.
Waamuzi wote hao wana beji za Shirikisho
la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), na watoka Dar es Salaam ukiondoa
Chacha ambaye maskani yake ni Bukoba mkoani Kagera.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Release No. 182
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Oktoba 22, 2013
SERENGETI BOYS YAALIKWA MICHUANO YA ANOCA
Timu ya Taifa ya Tanzania kwa vijana
wenye umri chini ya miaka 20 (Serengeti Boys) imealikwa kushiriki
Olimpiki ya Afrika itakayofanyika Mei mwakani.
Mpira wa miguu ni kati ya michezo 22
itakayoshindaniwa katika mashindano yatakayofanyika Gaborone, Botswana
chini ya Kamati za Olimpiki za Afrika (ANOCA).
Kwa mujibu wa Kamati ya Olimpiki ya
Tanzania (TOC), Tanzania imepewa nafasi ya kushiriki katika michezo hiyo
ya Olimpiki kwa Afrika kutokana na kuwa na programu nzuri za vijana
hasa chini ya umri wa miaka 17.
Hiyo itakuwa ni michezo ya Pili ya Afrika kwa Olimpiki ambapo ya Kwanza ilifanyika mwaka 2010 jijini Rabat, Morocco.
YANGA, SIMBA VIWANJANI VPL J5
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea
kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi tatu; ambapo Yanga itaikaribisha
Rhino Rangers katika mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Coastal Union inaikaribisha Simba katika
mechi itakayopigwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga na kuchezeshwa na
mwamuzi Dominic Nyamisana kutoka Dodoma.
Tanzania Prisons ambayo imepoteza mechi
mbili zilizopita ugenini dhidi ya Ashanti United na Simba inarejea
uwanja wake wa Kumbukumbu ya Sokoine kwa kuikaribisha Kagera Sugar.
Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL)
inaendelea kesho (Oktoba 23 mwaka huu) kwa mechi moja ya kundi A
itakayozikutanisha Tessema na Villa Squad kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Karume jijini Dar es Salaam.
KIINGILIO MECHI YA U20 WANAWAKE 1000/-
Kiingilio cha chini kwenye mechi ya
wanawake chini ya miaka 20 katika ya Tanzania na Msumbiji itakayochezwa
Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kitakuwa sh. 1,000.
Mechi hiyo itachezwa kuanzia saa 10
kamili jioni, na kiingilio hicho ni kwa ajili ya viti vya rangi ya
kijani, bluu na chungwa. Viingilio vingine ni sh. 2,000 kwa VIP C, sh.
5,000 kwa VIP B wakati VIP A itakuwa sh. 10,000.
Timu ya Msumbiji inatarajiwa kuwasili
nchini kesho (Oktoba 23 mwaka huu) saa 8 kamili mchana kwa ndege ya LAM.
Msumbiji yenye msafara wa watu 25 itafikia kwenye hoteli ya Sapphire.
UCHAGUZI TPL BOARD KUFANYIKA IJUMAA
Uchaguzi wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPL
Board) utafanyika Oktoba 25 mwaka huu kwenye ukumbi wa mikutano uliopo
Golden Jubilee Tower.
Kwa mujibu wa Kamati ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wajumbe wanaounda Mkutano wa
Uchaguzi ni wenyeviti kutoka klabu 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL),
na 14 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL).
Wagombea kwenye uchaguzi huo ni Hamad
Yahya Juma (Mwenyekiti), Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti)
wakati wanaoumba ujumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Khatib Omari Mwindadi
na Kazimoto Muzo.
RAMBIRAMBI MSIBA WA JIMMY MHANGO
Shrikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya
klabu ya Ashanti United, Jimmy Mhango kilichotokea jana (Oktoba 21 mwaka
huu).
Msiba huo ni mkubwa kwa wadau wa mpira
wa miguu kwani Mhango aliutumikia mpira wa miguu kwa muda mrefu, tangu
akiwa mchezaji, kocha na baadaye kiongozi.
Kabla ya kuingia kwenye Bodi ya Ashanti
United, enzi za uchezaji wake alichezea timu za Mapinduzi ya Dodoma,
Ushirika ya Moshi na Pan African ya Dar es Salaam. Pia aliwahi kuwa
Kocha Mkuu wa Ashanti United.
TFF inatoa pole kwa familia ya marehemu
Mhango, klabu ya Ashanti United na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar
es Salaam (DRFA), na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi
hiki kigumu cha msiba huo mzito.
Maziko yamefanyika leo mchana katika
makaburi ya Abeid (Mchikichini) Dar es Salaam. Mungu aiweke roho ya
marehemu Mhango mahali pema peponi. Amina
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment