WAZIRI
Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete
kusitisha mzunguko wa nne wa utoaji wa leseni za utafutaji wa gesi asili
na mafuta hadi sera na sheria ya gesi asili zikamilike, na marekebisho
ya sera ya nishati na sheria za mafuta yafanyike.
Mnyika
ambaye pia ni mbunge wa Ubungo (CHADEMA), alisema hatua hiyo ni kurejea
maoni na mapendekezo aliyoyawasilisha bungeni kwa niaba ya Kambi Rasmi
ya Upinzani Mei 22 mwaka huu.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, alisema rais anapaswa kuchukua
hatua hiyo kwa kuzingatia kwamba Mei 25 mwaka huu, badala ya
kushughulikia mapendekezo hayo, Waziri wa Nishati na Madini, Prof.
Sospeter Muhongo alitoa majibu ya uongo na upotoshaji bungeni kuhusu
masuala mbalimbali.
“Aidha Ikulu
inapaswa kueleza iwapo Baraza la Mawaziri chini ya Rais Kikwete ndilo
lililofanya uamuzi wa kuendelea na mchakato wa kutoa leseni za vitalu
vya utafutaji wa gesi asili bila ya kuwepo kwa sera ya gesi asili na
sheria ya gesi asili, na sera ya nishati na sheria zinazohusu mafuta au
ni maamuzi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) na Wizara ya
Nishati na Madini,” alisema.
Mnyika
aliongeza kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda anapaswa kueleza iwapo kauli ya
kejeli, dharau na uongo ya hivi karibuni iliyotolewa na Waziri Muhongo,
kwamba uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania ni kuwekeza kwenye soda na
juisi, si kwenye sekta ya gesi, ni msimamo wa serikali au maoni ya
waziri binafsi.
“Izingatiwe
kwamba Wizara ya Nishati na Madini, kupitia Shirika la Maendeleo ya
Petroli nchini (TPDC), imetangaza mzunguko wa nne wa utoaji leseni za
utafiti wa gesi asili na mafuta katika vitalu nane ndani na nje ya maji
ya Ziwa Tanganyika vyenye ukubwa wa kilomita za mraba elfu tatu kila
kimoja utakaofanyika Oktoba 2013.
“Serikali
pia imetenga mipaka ya vitalu viwili kwenye bahari kuu, na kuingia ubia
wa utafiti na kampuni inayoitwa mbia wa kimkakati (Strategic Partner)
ambae serikali haijamtaja,” alisema.
Alisema
mchakato huu unafanyika wakati taifa likiwa halina sera (mchakato wa
kuiandika bado unaendelea) na hatimaye yaanze maandalizi ya kupata
sheria mahususi za kusimamia sekta ndogo ya gesi, hatua ambayo inapaswa
kuambatana na marekebisho ya kisera na kisheria ya sekta.
Aliongeza
kuwa tayari Tanzania imeshafanya ugunduzi wa futi za ujazo zaidi ya
trilioni 32 za gesi katika maeneo kadhaa nchini, hivyo kuifanya kuwa
kati ya nchi vinara wa gesi nyingi Afrika na duniani.
“Utajiri huu
wa gesi hadi sasa hauna sera wala sheria zinazotoa mwongozo wa
usimamizi na udhibiti wake, ili kuhakikisha unawanufaisha Watanzania,
kuepuka makosa yaliyofanyika katika uwekezaji mwingine wa gesi asili na
rasilimali nyingine uliofanyika bila mifumo thabiti,” alisema.
0 comments:
Post a Comment