Kambi ya
Rasmi ya Upinzani Bungeni, itafanya mabadiliko makubwa katika Baraza
lake Kivuli wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Bunge unaoanza leo mjini
Dodoma.
Habari
zilizopatikana jana mjini Dodoma zilisema Zitto ni mlengwa mkuu wa
mabadiliko hayo ikiwa ni utekelezaji wa maazimio ya Kamati Kuu (CC) ya
chama chake.
Kamati Kuu
chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe iliagiza kuvuliwa nyadhifa zote,
Zitto pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitilla Mkumbo kwa kile
kilichodaiwa ni kukisaliti chama.
Kwa mujibu
wa habari hizo, katika Mkutano wa 14 wa Bunge unaoanza leo, kambi rasmi
ya upinzani imepanga kumvua rasmi Zitto nafasi ya Naibu Kiongozi wa
Upinzani Bungeni na Waziri Kivuli wa Fedha.
Jana,
Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu alithibitisha kuwapo
kwa mpango wa mabadiliko hayo na kwamba yanatarajiwa kufanyika kati ya
mwishoni mwa wiki hii na mwanzoni mwa wiki ijayo.
“Tutakaa
mwishoni mwa wiki hii au mwanzoni mwa wiki ijayo kwa sababu Kiongozi wa
Kambi (Freeman Mbowe), atafika bungeni Desemba 6, mwaka huu na ndiye
Mwenyekiti wa Baraza Kivuli,” alisema Lissu na kuongeza:
“Mbali ya
Zitto kuna Said Arfi (Mbunge wa Mpanda Mjini) ambaye amejiuzulu nafasi
zake zote ikiwa ni pamoja na Waziri Kivuli wa Uchukuzi na tutaangalia
ufanisi wa mawaziri wengine kivuli”.
Baraza kivuli linaundwa na mawaziri 18 wakiongozwa na Mbowe na Zitto aliyekuwa Naibu wake na Manaibu saba.
Kujitoa kwa wanachama
Lissu ambaye
pia ni Mbunge wa Iramba Mashariki, alisema angeogopa kama kungekuwa na
wimbi la wanachama zaidi ya 1,000 kuondoka katika chama kupinga misingi
ya chama.
“Lakini kama
walimfuata Zitto ndani ya chama ni ruksa sisi hatuna shida lakini kama
ni chama hapo kuna la kuangalia… Sisi tunaamini wanachama wetu hawafuati
mtu, bali misingi,” alisema.
Kuhusu suala
la Mwenyekiti wa Mkoa wa Lindi, Ally Omary Chitanda, aliyejiondoa
Chadema, Lissu alisema kiongozi huyo aliondoka katika chama hicho baada
ya kuona anapoteza masilahi yake.
“Huyu
alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Lindi, wakati huohuo alikuwa ni ofisa
anayetumikia makao makuu jambo ambalo lilileta mgogoro kwa wanachama,”
alisema Lissu.
Aliongeza:
“Yeye alitakiwa kuachia nafasi ya ofisa wa chama Makao Makuu kwa sababu
wanachama walikuwa wakilalamika kwamba anakaa Dar es Salaam wakati yeye
ni Mwenyekiti Lindi”.
Dk Slaa kutua jimbo la Zitto
Katika hatua
nyingine, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa amesema atafanya
ziara ya kukijenga chama mkoani Kigoma licha ya kuwapo taarifa
inayomzuia kwa madai kwamba hali ya usalama kwa viongozi wa kitaifa
kwenda huko kwa sasa si nzuri.
Hatua ya Dk
Slaa imekuja wakati kukiwa na taarifa kwamba wafuasi wa Chadema mkoani
humo wamekasirishwa na kuvuliwa madaraka kwa Zitto ambaye pia ni Mbunge
wa Kigoma Kaskazini.
Mwenyekiti
wa Chadema Mkoa wa Kigoma, Jafar Kasisiko alisema uchunguzi wao
unaonyesha kuwa watu wengi mkoani humo wamejenga uhasama na uongozi wa
juu kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kutoridhika na uamuzi wa Kamati Kuu
dhidi ya Zitto.
Hata hivyo,
Dk Slaa alisema jana kwamba hana wasiwasi na atatua keshokutwa katika
mkoa huo kuanza ziara wiki moja kuanzia Desemba 5 hadi 13 kwa lengo la
kuimarisha chama.
“Mimi
sijapewa taarifa hizo… wanachama wengi wananipigia wanasema wananisubiri
kwa hamu na hakuna taarifa zozote mbaya,” alisema Dk Slaa akiashiria
kwamba chama hicho mkoani humo kiko bega kwa bega na uongozi wa juu.
Juu Kusini waunga mkono
Chadema
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, imeunga mkono hatua ya Kamati Kuu ya
chama hicho kuwavua nyadhifa zote za uongozi Zitto, Dk Kitila na
aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba.
Mratibu wa
Chadema Kanda hiyo, Frank Mwaisumbe alisema uongozi na wanachama cha
Chadema Nyanda za Juu Kusini wanaunga mkono uamuzi uliochukuliwa na wana
imani kubwa na viongozi wa juu wa Chadema.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment