DK SLAA,ANUSURIKA KUUWAWA!!

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa 
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa amesema analindwa na Mungu na ndiyo maana chama hicho kimegundua mpango wa mlinzi wake kushawishiwa na maofisa usalama wa taifa ili kumwekea sumu katika chakula au maji.

Mlinzi huyo (jina tunalihifadhi kwa sasa) ambaye alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi cha Oysterbay juzi, pia anadaiwa kutumiwa na kigogo mmoja wa CCM kuiba siri za chama hicho.
Tayari polisi imeanza kuchunguza taarifa hizo na jana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura alisema kuwa mtuhumiwa huyo ana haki kama watuhumiwa wengine wanaofikishwa polisi wakikabiliwa na kesi za jinai na kusisitiza kuwa; “Tuhuma zinazomkabili ni za kawaida na tunazichunguza.”
Akieleza alivyopokea taarifa hizo Dk Slaa alisema, “Ninalindwa na Mungu ndivyo ninavyoweza kusema. Chadema sisi huwa tunaanza na Mungu na kumaliza na Mungu. Ushahidi umewekwa wazi na hili ni jambo la kweli na limenigusa kwa kiasi kikubwa.”
Alisema baadhi ya mambo yaliyofanywa na mlinzi wake ameyaona kwa macho na kusisitiza kuwa njama zinazofanywa na wanaomtumia haziwezi kukiondoa chama hicho katika harakati zake za kila siku.
“Tupo makini ndiyo maana tumebaini yote. Tunawajua waliohusika na tupo makini katika kuwafuatilia. Kama Mungu yupo upande wetu tumuogope nani zaidi,” alisema.
Alisema Chadema ina safari ndefu hivyo ni lazima wana-Chadema kuvaa viatu ili kujikinga na vumbi na uchafu wa kila aina, akimaanisha kuwa chama hicho kinakumbana na vikwazo vingi.
Tuhuma dhidi ya mlinzi huyo zilitolewa juzi na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando kuwa wamebaini nyendo za mlinzi huyo na kuzifuatilia kwa ukaribu hadi kupata taarifa hizo alizosema ni ukweli mtupu.
Hili ni tukio la tatu kwa Chadema kudai kuna mipango ya kumfuatilia Dk Slaa, mara ya kwanza ilikuwa Februari 2009 alipobaini kutegewa vinasa sauti hotelini mkoani Dodoma na mkakati uliotajwa kuwa wa kuwaua yeye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika.

 “Mlinzi alitueleza kwamba alikuwa akipewa fedha kwa ajili ya kutoa siri za vikao vya chama kupitia simu yake…kwa kuwa anaruhusiwa kuingia kwenye vikao vya chama hicho kama mlinzi amekuwa akitegesha simu yake ili kuwapa taarifa watu wa CCM `live’ ili wasikie kila kinachojadiliwa,” alidai Marando.
Akieleza jinsi walivyombaini mlinzi huyo, Marando alisema pamoja na ushahidi wa mawasiliano ya simu, lakini pia mlinzi huyo alikiri kwa kinywa chake kutumiwa na maofisa hao ambao hakuwataja majina lakini alisema wako 22.

Akifafanua namna mipango hiyo ilivyofanywa, Marando alidai walibaini mlinzi huyo kutumiwa muda wa maongezi kwa nyakati tofauti wa jumla ya Sh7 milioni kwenye simu zake.
Marando alisema, “Kilichokuwa kinatokea ni kwamba kigogo wa CCM (anamtaja) na wenzake walikuwa wanasikia kila kinachozungumzwa kutoka kwenye vikao vya ndani vya Chadema kwa sababu ya mlinzi huyo.”
Kigogo huyo wa CCM hakupatikana juzi na jana kujibu tuhuma dhidi yake, lakini ofisa mmoja wa makao makuu alisema taarifa hizo zimewafikia na zitajibiwa kwa njia rasmi.
Kadhalika, Marando alisema walibaini kuwa mlinzi huyo amekuwa akizungumza kwa simu kwa saa mbili hadi tatu na maofisa usalama hao ili kuwapa taarifa mbalimbali za chama.
Marando alisema kwa miaka miwili mfululizo mlinzi huyo amekuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na ofisa mmoja usalama wilayani Kinondoni ambaye ana uhusiano wa karibu na kigogo huyo wa CCM.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment