Wakati wananchi wa kada mbalimbali
wakishinikiza Rais Jakaya Kikwete kutokusaini Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2013, kwa maelezo kuwa una
kasoro, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
naye amesema sheria ina upungufu.
Kauli hiyo ya Warioba imekuja wakati
vyama vya NCCR Mageuzi, Chadema na CUF, vikifanya mikutano nchi nzima
kuwashawishi wananchi kupinga kile wanachokiita hujuma dhidi ya
upatikanaji wa Katiba Mpya.
Sheria hiyo ambayo Warioba amesema ina
upungufu, muswada wa marekebisho yake ulijadiliwa na kupitishwa wa
wabunge Septemba 6, mwaka huu katika Mkutano wa 12 wa Bunge Mjini
Dodoma, ikiwa ni baada ya kubadilishwa kwa baadhi ya vifungu na hivi
sasa Rais Kikwete anasubiriwa kuusaini ili iwe sheria kamili.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Jaji Warioba alisema: "Mwisho
wa kazi ya tume ni baada ya kukabidhi rasimu, hilo ni tatizo. Maana tume
itakuwa imeshavunjwa, sasa itafanyaje kazi ya kutoa elimu kwenye kura
ya maoni?"
Jaji Warioba pamoja na kukiri upungufu huo, alisema kurekebisha au kutokurekebisha kasoro hizo si jukumu la tume hiyo.
"Tunawaomba watafakari, waone jinsi gani
tume ambayo imekwishavunjwa itakuja kutoa elimu wakati wa kura ya maoni,
sheria ina 'contradiction' (ina mkanganyiko)," alisema.
Muswada huo ulipitishwa na wabunge wa CCM
baada ya wale wa upinzani kutoka nje baada ya Kiongozi wa Kambi ya
Upinzani, Freeman Mbowe kuamuriwa na Naibu Spika, Job Ndugai kutoka nje
kutokana na kukaidi kwake amri ya kukaa chini alipokuwa akitaka kutoa
hoja kabla ya mjadala wake kuanza.
Muswada huo unapingwa kwa kuwa Rais
amepewa mamlaka ya kuteua wajumbe 166, ambao si wabunge wala wawakilishi
na Zanzibar kutokushirikishwa kikamilifu kwenye maandalizi ya muswada
huo.
Hata hivyo, Warioba alisema pamoja na
kasoro hizo Tume hiyo inafanya kazi yake kwa kufuata sheria hiyo huku
akisisitiza, "Wanaotunga sheria ni wengine siyo sisi, tulipoteuliwa
tulikuta sheria na kuanza kazi kwa kuifuata. Imefanyiwa marekebisho sisi
tunafuata."
Alisema waliofanya mabadiliko ya sheria
hiyo wana haki ya kufanya hivyo na kwamba Tume ya Mabadiliko ya Katiba
haiwezi kuzuia kutokufanyika kwa mabadiliko hayo, kwani yapo baadhi
yanaihusu.
Alisema baada ya kuipata sheria hiyo:
"Tulijiuliza maswali kwa sababu miswada huwa inapelekwa bungeni na
Serikali ikiwemo ya Katiba. Anayeipeleka kama ni waziri ndiye anayetoa
ufafanuzi pale inapohitajika."
Alisema kulingana na sheria, tume yake
ndiyo inayotakiwa kutoa ufafanuzi katika Bunge la Katiba, kama ambavyo
Waziri hutoa maelezo anapowasilisha muswada bungeni.
"Tulipouliza tulielezwa kwamba sisi ambao
tumepewa jukumu la kupata maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ndiyo
tutaitwa pale tu patakapohitajika ufafanuzi wa jambo fulani," alisema.
Alisema kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba itafanyika na kukamilika katika muda uliopangwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
"Tulianza kazi Mei mwaka jana na
tunatakiwa kumaliza Novemba mwaka huu, sheria inaruhusu kuongeza miezi
miwili kama tutakuwa hatujakamilisha kazi. Katiba Mpya inatakiwa iwe
imekamilika Aprili 26, 2014," alisema.
0 comments:
Post a Comment