Dodoma. Bunge la Katiba
jana lilianza kujadili Rasimu ya Katiba kwa misukosuko kwenye Kamati
baada ya kuvamiwa na kundi la wanaharakati waliokuwa na mabango wakidai
hati halisi ya Muungano yenye saini za Mwalimu Julius Nyerere na Abeid
Karume.
Msukosuko mwingine uliozikumba karibu
kamati zote zinazoanza kujadili rasimu hiyo kwa kuanzia sura mbili
zinazohusu Muungano – sura ya kwanza na ya sita na kuzua malumbano, ni
maana ya maneno dola, shirikisho, muungano na nchi.
Wakati waandamanaji wenye mabango
wakiishia mikononi mwa polisi, suala la Muungano lilitulizwa kwa kuitwa
wanasheria kutoa tafsiri sahihi kwa kila neno.
Katika kamati zote, suala la muda wa
kamati kujadili sura hizo mbili kwa siku mbili kila moja pia liliibua
mjadala mkali, hadi kuwalazimisha baadhi ya wenyeviti wa kamati kuamua
kumwandikia mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kuomba muda uongezwe.
Hali hiyo imejitokeza Bunge hilo likiwa
limeshakaa siku 40 kabla ya kuingia katika mjadala rasmi, baada ya
kupoteza muda mwingi katika kutengeneza kanuni za uendeshaji wa chombo
hicho.
Wanaharakati wavamia
Wakati kamati zikijiandaa kuanza mjadala,
wanaharakati wawili walivamia kwenye ukumbi wa Royal Village, wakiwa na
mabango yenye maandishi yanayowataka wajumbe kutetea maoni ya wananchi
yaliyomo kwenye rasimu ya Katiba.
Hata hivyo, watu hao baadaye waliondolewa kwenye eneo la hoteli hiyo na maofisa wa usalama majira ya saa 2:00 asubuhi.
Hata hivyo, mwenyekiti wa Kamati Namba 9,
ambayo inafanya vikao vyake kwenye hoteli hiyo, Kidawa Hamis alisema
kuwa hali ni shwari kwenye kamati yake na wajumbe wanaendelea kuchambua
rasimu.
Katika kumbi zilizopo kwenye Hoteli ya
St. Gasper, pia watu wawili walikamatwa wakiwa na mabango yanayowataka
wajumbe kutambua kwamba katiba ni mali ya wananchi na si ya wanasiasa.
Hati ya Muungano
Katika makundi karibu yote, jana
kuliibuka hoja juu ya Hati ya Muungano, wajumbe wakitaka kabla ya kuanza
mjadala ionyeshwe kwa kuwa ndio msingi wa hoja.
Hata hivyo, habari za ndani ya kamati
zinadai kuwa hati ambazo zilipelekwa kama vielelezo katika makundi hayo,
zilitiliwa shaka na wajumbe baada ya kukosekana saini za waasisi hao wa
Muungano na nakala halisi.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 11, Anna
Kilango alikiri kuwapo mjadala mzito juu ya Hati ya Muungano, lakini
akasema kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othman
alisaidia sana kulitafutia ufumbuzi.
“Katika kundi letu, tulikuwa na
mwanasheria wa Zanzibar na baada ya majadiliano alitueleza kuwa
viambatanisho vya Hati ya Muungano vilivyopo kwenye randama ya Jaji
(Joseph) Warioba ni sahihi,” alisema Kilango.
Alisema kuwa pia katika kundi lao,
kulikuwa na utata juu ya maana ya maneno dola, shirikisho, nchi na
Muungano, hasa kwa wajumbe ambao si wabunge.
Kilango alisema kutokana na utata huo,
Kamati yake imeazimia kumuomba Sitta kuwapatia mwanasheria ambaye
atasaidia kuelimisha wajumbe maana ya vyombo hivyo.
“Kanuni ya 56 fasili ya saba, inatupa
nafasi kuwasiliana na mwenyekiti ili kupata mtaalamu ambaye atasaidia
kuwaelimisha wajumbe,” alisema.
Kuhusu ufinyu wa muda, Kilango alisema
katika kamati yake suala hilo lilijitokeza kwa kuwa hadi jana walikuwa
wanajadili sura ya kwanza pekee yenye ibara tano.
“Sote tumebaini muda ni mfupi na nitawasiliana na mwenyekiti ili tuongezewe muda,” alisema Kilango.
Mwenyekiti wa Kamati Namba 1, Ummy
Mwalimu pia alieleza tatizo la hati, tafsiri ya maneno na muda kwamba
ilikuwa ni changamoto kubwa.
“Ni kweli kuna changamoto ambazo
zimejitokeza za wajumbe kutaka hati ya Muungano ambayo imesainiwa na
waasisi na muda ni mfupi,” alisema.
Hata hivyo, alisema jana jioni alitarajia
kukutana na viongozi wa Bunge ili kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya
wajumbe ili kuwezesha kuendelea vizuri na mjadala.
“Lakini kimsingi tunakwenda vizuri, wajumbe wanabishana kwa hoja na hakuna vurugu hali ni shwari kabisa,” alisema Mwalimu.
Katika makundi mengine, mijadala
ilikwenda mbali zaidi na kupendekeza kuongezwa ibara itakayoruhusu
kuongeza nchi nyingine kwenye shirikisho.
Kwa kundi jingine, kulitokea malumbano baada ya mapendekezo ya mabadiliko ya rasimu, hoja ambayo ilipingwa.
Mnyika ataka hati ya Muungano
Wakati huo huo, mjumbe wa Bunge la
Katiba, John Mnyika aliwasilisha bungeni hoja binafsi ya kupatiwa nakala
halisi ya Hati ya Muungano.
Alisema hati ambayo imesambazwa kwa wajumbe sio halisi na ni maudhui ya hati halisi, jambo ambalo sio sahihi kisheria.
“Mpaka sasa takriban wiki moja tangu
kuomba hati hii kwa barua …sijapata majibu, lakini sheria ya Muungano
mwisho kuna jedwali la sheria ambalo lina hati ambayo haina saini na
uthibitisho,” alisema.
Nimemuomba kupatiwa hati hiyo kwa
kuzingatia kanuni ya 4 (6) ambacho kinatoa haki kwa mjumbe kupatiwa
taarifa au nyaraka ya kumuwezesha kutekeleza majukumu yake.
“Sasa tunajadili ibara ya kwanza kifungu
cha kwanza, ambayo imeibua mjadala mkali kwa umma juu ya muundo wa
Muungano, lakini naamini ilikuwa ni vyema tunapojadili hoja hii tuwe na
hati halisi ya Muungano na sio nakala,” alisema Mnyika.
Watatu mbaroni
Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, David
Misime alithibitisha kukamatwa kwa watu watatu kwa tuhuma za kufanya
mkusanyiko isivyo halali na kuwa na mabango yenye lengo la kuhamasisha
uvunjifu wa amani.
Alisema watu hao walikamatwa jana saa 3:30 asubuhi Wilaya ya Dodoma Mjini.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni mkazi
mmoja wa Kilimani anayeitwa Augustino Pancras (60), Cosmas Katebeleza
(44), Mkazi wa Kikuyu na Jotam Tarukundo (35), Mkazi wa Chidachi.
Alisema mabango waliyokutwa nayo yalikuwa
na ujumbe unaosomeka “wajumbe msijivunie wingi wenu humo ndani, sisi
wananchi tupo nje na ndiyo wengi maoni yetu yaheshimiwe.”
Kamanda Misime alisema watu hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika kulingana na ushahidi watafikishwa mahakamani
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment