IDADI YA KATA, VIJIJI, NA VITONGOJI VYAONGEZEKA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA HUKU KUKIWA NA MALALAMIKO YA WANASIASA!!


Waziri Mkuu,Mizengo Pinda 
Dar es Salaam. Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) imetangaza ongezeko la idadi ya kata, vijiji, mitaa na vitongoji nchini vitakavyotumika kwa ajili ya uchaguzi serikali za mitaa, huku hatua hiyo ikiibua hoja miongoni mwa wanasiasa na wasomi.


Tayari vyama vya siasa vimeanza kufanya maandalizi ya uchaguzi huo wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu.
 Wanasiasa na wasomi wametoa maoni yao kuhusu hatua hiyo, wengi wakilalamikia jinsi isivyokidhi mahitaji ya wananchi na wengine wakielezea kuwa imetangazwa wakati huu kuwanufaisha wachache ili wapate madaraka.

 Mkurugenzi wa Serikali za Mitaa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kalist Luanda alisema Serikali imeongeza idadi hiyo ili kuanzisha maeneo mapya ya kiutawala ambayo yatawawezesha wananchi kupata huduma za kijamii na kiutawala kwa karibu.

Alisema ongezeko hilo limefanywa kwa kuzingatia idadi ya watu kuongezeka kwa kasi na kupanuka kwa maeneo baada ya watu kujisajili, hivyo kata zimeongezwa na kuwa 465, vijiji 628, mitaa 746 na vitongoji 4,257. Kata kwa nchi nzima zimeongezwa kutoka 3,802 mwaka 2009 hadi 3,337, vijiji vimeongezeka kutoka 11,795 hadi 12,423 na mitaa imetoka 2,995 hadi 3,741 kwa upande wa vitongoji imeongezeka kutoka 60,359 hadi 64,616.

Nae Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye akizungumzia uamuzi huo aliikosoa hatua hiyo akieleza kwamba idadi ya vijiji vilivyoongezwa ni ndogo ikilinganishwa na mahitaji yaliyopo.

“Kuna malalamiko mengi kuhusu vijiji hata hivi karibuni kwenye ziara huko Iringa tulifikishiwa malalamiko hayo bado hatujapata uhakika wa vigezo vilivyotumika kuongeza idadi ya vijiji hivyo na kwamba kwa kata mimi sina shida,” alisema.

Nape alisema hata kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM, wajumbe wengi walitoa malalamiko yao kuhusu maombi ya vijiji, ingawa kuna maelezo ya awali yaliyotolewa na Serikali kuhusu kukwamishwa na gharama za kuwalipa viongozi wa ngazi hizo.

“Hii bado siyo sababu ya kujitosheleza nafikiri Serikali ichukue hatua ya kuongeza vijiji zaidi, bado ina nafasi ya kufanya hivyo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa, gharama inazosema nafikiri madiwani kupitia halmashauri zao walivipitisha baada ya kutambua kuwa watazimudu,” alisema Nape.

Akizungumzia jinsi CCM ilivyojidhatiti kushinda katika uchaguzi huo alisema kwamba, watashinda karibu mitaa yote kwa asilimia 96, hasa kwa kuwa upinzani wamejiunga na kuwa Ukawa, itakuwa ngumu kwao kujipanga na kushinda.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbrod Slaa alisema kuwa anatarajia kufanya utafiti ili kujua ongozeko hilo kama lilifanywa kwa kuzingatia utaratibu unaostahili au umefanywa kwa manufaa ya mtu binafsi.

“Siwezi kueleza maoni yangu vyema kama zijafanya utafiti ili nijiridhishe kwa sababu inawezekana kuna mambo ya kisiasa yaani mitaa imeongezwa kumnufaisha mtu kisiasa,” alisema Dk Slaa.
Mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR- Mageuzi, David Kafulila kwa upande wake alieleza kufurahishwa na ongezeko hilo, akieleza kwamba kwa wilaya yake ya Uvinza hali hiyo itamwezesha hata katika kinyang’anyiro cha ubunge wakati wa uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
“Licha ya kwamba ongezeko hilo litawanufaisha wananchi kwa kupata huduma za kiutawala na kijamii, lakini pia kwa upande wa upinzani tutaendelea kunufaika kwa kuwa vijiji vilivyoongezwa ambavyo ni Mwakizega, Bosanza Herembe na Kandaga ni maeneo tunayokubalika vyema,” alisema Kafulila.
Mbunge wa Mtera kwa tiketi ya CCM, Livingstone Lusinde aliipongeza hatua hiyo ya serikali akieleza kwamba itasogeza karibu huduma kwa wananchi, licha ya kwamba wapo wanaolalamikia kwamba imechelewa kutangazwa.
“Hao mimi wananishangaza wanaolalamika kwamba serikali imechelewa kutangaza je, mshahara ukichelewa utashindwa kufanya matumizi, kwangu wananchi wanafurahia hatua hiyo,” alisema Lusinde.
Mbunge wa Viti Maalumu kutoka mkoani Mwanza, kwa tiketi ya CUF, Mkiwa Kimwanga alisema kwamba anaona kulikuwa na umuhimu kwa Serikali kufanya ongezeko katika maeneo hayo ya utawala kutokana na ongezeko la idadi ya watu lilivyo sasa.
“Hata hivyo, kwa upande mwingine siungi mkono jinsi walivyokata hayo maeneo kwa sababu kwa huku kwetu wameweka mahali ambapo hatukupendekeza kwenye baraza la madiwani, hivyo kuna jambo linaloendelea ambalo inabidi tulifanyie utafiti,” alisema Kimwaga.
Alifafanua kuwa Wilaya ya Ilemela ilikuwa na mitaa 101 na wakapendekeza iongezwe iwe 165, lakini jambo la ajabu ni kwamba wamepelekewa 172 na maeneo, pia hakuna ushirikishwaji kwa wananchi kuhusu maeneo hayo ili wakati wa uchaguzi wajitambue wapo wapi. 

Mbunge wa Nkasi Kaskazini kwa tiketi ya CCM, Ally Keissy alisema ni jambo ambalo amakuwa akilipigia kelele kwa muda mrefu, anashukuru kwamba pia kwamba wamepata kata nne mpya.
“Safi kabisa kata moja kwangu ni sawa na majimbo matatu ya Zanzibar, ila nafikiri bado kuna kata mbili Wantende na Nkwamba ambazo nazo inapaswa zifikiriwe tena kugawanywa, miundombinu inakuwa ni tatizo kwa jinsi zilivyo sasa,” alisema Kessy.

Mbunge mwingine Chiku Abwao alisema kuwa hajakubaliana na hatua hiyo kwa kuwa haijatekelezwa katika hali ya usawa, kwa sababu bado kuna majimbo mengine ni makubwa wakati yangeweza kugawanywa kutokana mitaa mipya iliyoanzishwa.
“Nafikiri ingekuwa vyema kama Serikali ingegawanya mitaa au kata kwa kuzingatia idadi ya watu, kama wenzetu wa Zanzibar, kwetu huku kuna tofauti kubwa na uanzishwaji wa mitaa na kata hizi mpya haukuzingatia hali hiyo,” alisema Abwao.
Machi 8, 2012 Serikali ilitoa matangazo rasmi ya Serikali (Government Notices), kuhusu uanzishaji wa mikoa mipya minne na wilaya mpya 19. Kwa mujibu wa tangazo hilo mikoa mipya ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Mikoa hiyo ilichapishwa katika Tangazo la Serikali Na. 72.
Wilaya 19 ambazo zimeanzishwa na kuchapishwa katika Tangazo la Serikali Na.73 ni Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi na Itilima. Wilaya nyingine ni Kakonko, Kalambo, Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama na Mlele. Nyingine ni Momba, Nyang’hwale, Nyasa, Uvinza na Wanging’ombe.
Kwa mujibu wa matangazo hayo makao makuu ya mikoa hiyo mipya minne ni Geita (Geita), Simiyu (Bariadi) Njombe (Njombe) na Katavi (Mpanda). Mikoa hiyo itakuwa na wilaya zifuatazo; Geita utakuwa na wilaya tano za Bukombe, Chato, Geita, Mbongwe na Nyang’hwale. Mkoa wa Katavi utakuwa na wilaya mbili za Mlele na Mpanda.
Mkoa wa Njombe utakuwa na wilaya nne za Makete, Njombe, Ludewa na Wanging’ombe wakati mkoa wa Simiyu utakuwa na wilaya tano za Bariadi, Busega, Maswa, Meatu na Itilima.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment