Kuna hofu ndani ya chama hicho kwamba mgawanyiko
uliojitokeza wakati wa vikao vya kamati utahamia kwenye Bunge zima
ambako mbali na waandishi wa habari kuruhusiwa kushiriki, pia huonyeshwa
moja kwa moja na vituo kadhaa vya televisheni.
Msigano unaotabiriwa kutokea ni ule uliojengwa
katika mambo yaliyozua mvutano ndani ya kamati kiasi cha wajumbe wenye
itikadi moja kusigana kwa misingi tofauti lakini kubwa likiwa ni lile la
Uzanzibari na Ubara.
Tofauti hizo za kimaeneo zilionekana dhahiri
wakati wa mjadala wa Sura ya Tisa na 10 ambazo zinahusu muundo wa Bunge
na mambo mengine ya utawala, pia katika Sura ya 14 hususan mgawanyo wa
mapato.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya wenyeviti
wa Kamati za Bunge hilo walitabiri mvutano mkali bungeni, wakirejea hali
ilivyokuwa ndani ya kamati zao ambako baadhi ya wajumbe hawakuridhika
na baadhi ya uamuzi.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Nne, Christopher Ole
Sendeka alisema mjadala katika kamati yake ulikuwa mkali na kwamba hali
itakuwa ni ngumu zaidi watakapoingia bungeni.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Tatu, Dk Francis
Michael alisema suala la ardhi linaweza kuzua mvutano mkali kwani ni
moja ya mambo muhimu katika Katiba.
Makamu Mwenyekiti wa kamati Namba Kumi na Moja,
Hamadi Yusufu Masauni alisema jambo pekee analotarajia kuwa litasumbua
ni muundo wa Bunge la Muungano.
Alisema unapotajwa muundo wa Bunge ndipo unapotajwa mfumo wa Muungano ambao umekuwa ni kero ya muda mrefu.
Mwenyekiti wa Kamati Namba Moja, Ummy Mwalimu
alisema hofu yake iko kwenye suala la mgawanyo wa mapato ambalo kamati
yake ilisita kulijadili hadi walipoitwa wataalamu kutoka Benki Kuu ya
Tanzania na Wizara ya Fedha za Muungano na ile ya Zanzibar.
Kwa msingi huo, wakati kamati zikianza safari ya
siku tano kuwasilisha taarifa zake kuanzia leo hadi Septemba 8, mwaka
huu, kutakuwa na maoni ya wachache katika baadhi ya kamati suala ambalo
linatoa picha ya kuwapo kwa mawazo tofauti katika mambo kadhaa.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa mengi ya
mambo hayo ni yale yaliyobadilishwa kinyume na yalivyokuwa kwenye Rasimu
ya Katiba iliyotungwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba au mambo mapya
yaliyoingizwa kwenye rasimu hiyo.
0 comments:
Post a Comment