Mvutano umeibuka katika Mji wa Moshi utata ukiwa nani hasa ni mmiliki halali wa kiwanja chenye hati namba 10660 ambacho Manispaa ya Moshi imekitumia kwa miaka 40 sasa.
Mgogoro huo uliozua sintofahamu wiki iliyopita,
ulisababisha madiwani wanaotokana Chadema ambao ndiyo wengi, kususia
kikao cha Baraza la Madiwani kilichokuwa kijadili bajeti ya manispaa
hiyo kwa mwaka 2015/2016.
Wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar
Michael, madiwani hao walisusia kikao hicho wakipinga kile walichodai ni
“mpango” mahususi unaofanywa na vigogo wa Serikali kusaidia kuporwa
eneo hilo.
Kitendo cha madiwani hao wa Chadema ambao ndiyo
wanaoongoza Baraza la Madiwani Manispaa ya Moshi kususia kikao hicho,
kumeibua maswali mengi kwa wananchi, wakitaka kujua ukweli halisi wa
mmiliki wa kiwanja hicho.
Kiwanja hicho kipo katikati ya mji kwenye eneo la
kibiashara kimepakana na jengo la makao makuu ya polisi Mkoa Kilimanjaro
pia ndipo zilipo ofisi za Serikali za Kata ya Mawenzi ya mjini Moshi.
Ni kiwanja hicho hicho ambacho mwaka 2012,
kilianishwa kama eneo la uwekezaji na halmashauri ikalitangaza rasmi
katika kikao cha Kanda ya Kaskazini kilichofanyika mkoani Tanga ili
kuvutia wawekezaji.
Mbali na kiwanja hicho kuwa na jengo la ofisi ya
Serikali Kata ya Mawenzi kwa miaka 40 mfululizo, kuna maduka ambayo
wapangaji wake wanalipa kodi zao moja kwa moja kwa halmashauri husika.
Hata hivyo, wakati Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi ikiwa katika mchakato wa kutafuta hati ya kumiliki kiwanja hicho,
imejitokeza Taasisi ya Mawenzi Sports Club (MSC), inayodai kulimiliki
eneo hilo.
Tayari Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael
na madiwani wake, wameweka kizuizi kisheria ili kuzuia mtu yoyote au
taasisi kufanya uhamisho wa umiliki wa kiwanja hicho.
Wakati hayo yakiendelea, leo Januari 26, madiwani
wa halmashauri hiyo wanakutana katika kikao maalumu cha baraza lao kwa
lengo la kujadili ajenda moja tu nayo ni kuhusu kiwanja cha Mawenzi,
hasa; nani ni mmiliki halali wa kiwanja?
0 comments:
Post a Comment