CHAMA cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimetamba kuwa hatua ya wabunge wake
kugomea hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa Bunge mwaka
2010 ndiyo imezaa mchakato wa Katiba mpya.
Kauli hiyo
ilitolewa jana na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, wakati
akihutubia wananchi wa mji wa Kahama, mkoani Shinyanga ukiwa ni
mwendelezo wa mikutano ya chama hicho kujadili rasimu ya Katiba mpya
katika mabaraza yao.
Mbowe
alisema kuwa kitendo hicho cha wabunge wao kutoka nje wakati Rais
Kikwete alipoanza kuhutubia kilikuwa ni kielelezo cha kupeleka ujumbe
kwamba Katiba iliyopo imepitwa na wakati.
“Licha ya
ulimwengu mzima kutoelewa na kutushutumu kwa kitendo hicho, lengo letu
lilikuwa ni kuishinikiza serikali ya CCM ikubali kufanyika kwa mchakato
wa kuanzishwa Katiba mpya ambayo ndiyo njia pekee ya kuelekea katika
ukombozi wa wananchi wanyonge,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hiyo ilikuwa moja ya sababu za Rais Kikwete kuridhia kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba mpya.
“Tulifanya hivyo kwa nia njema kabisa na baadaye tulianza maandamano nchi nzima kwa lengo hilo hilo,” alisema.
Mbowe
alifafanua kuwa jambo kubwa lililowasababisha kusuia na hatimaye
maandamano, ni matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, ambayo chama
hicho kinaamini yalichakachuliwa.
Alisisitiza kuwa uchakachuaji huo ulisababishwa na Katiba mbovu iliyopo sasa.
“Baada ya
kususia hotuba hiyo na kisha maandamano, Rais Kikwete alikubali kukutana
na viongozi wa vyama kikiwamo CHADEMA, kwa lengo la kujadiliana na
kukubaliana muundo wa uanzishwaji wa mchakato huo,” alisema.
Mbowe
alivionya vyama vya siasa kutouchukua mjadala wa Katiba katika sura ya
kisiasa zaidi, badala yake alivitaka viwe nyenzo ya kuwezesha wananchi
kuandikwa kwa Katiba mpya.
Mbowe ambaye
pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni,
katika ziara hiyo ya mikutano ya mabaraza ya kujadili rasimu ya Katiba
mpya, ameongozana na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John
Mnyika.
0 comments:
Post a Comment