Rais Jakaya Kikwete amesema wale wote wanaombeza kuhusu utendaji wake, wataona aibu atakapomaliza muhula wake 2015 huku akiwananga baadhi ya wanaCCM kwa kushindwa kuyaelezea mafanikio ya Serikali chini ya chama hicho.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa
kusambaza umeme katika mikoa ya Mwanza na Geita unaofadhiliwa na Mfuko
wa Changamoto za Milenia (MCC), Rais Kikwete alisema: “Wakati wa kampeni
nilibezwa sana, lakini sasa ninawaomba walionibeza kufika vijijini na
kuangalia ukamilishaji wa ahadi zangu.
“Nataka waje waone, kwa sasa ninakamilisha
usambazaji wa umeme katika vijiji vyote ili kufikia lengo la Watanzania
asilimi 30 kufikiwa na nishati hiyo. Hadi 2015 umeme utakuwa umesambaa
nchi nzima.
“Serikali yangu itavunja rekodi ya kusambaza umeme
katika vijiji vingi nchini…Tumejenga mtandao wa barabara kwa sasa, hali
yetu ya barabara ni bora Afrika Mashariki, tuliahidi meli Bukoba naomba
niwaeleze kuwa zinakuja, tena siyo moja ni meli mbili.
“La umeme leo nazindua nataka kuwaeleza
walionibeza waje waone sasa ahadi zangu...hayo yote niliyasema kwenye
ahadi zangu 2010,” alieleza Kikwete huku akishangiliwa na wananchi.
Mradi huo umegharimu Dola za Marekani 15.54
milioni sawa na Sh24.87 bilioni kwa Mwanza na Geita pekee, fedha ambazo
ni asilimia 25 ya Dola za Marekani 62.6 milioni sawa na Sh103.24 bilioni
zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi 225 ya upanuzi wa njia
za kusambazia umeme katika mikoa kumi nchini.
Rais Kikwete alisema Serikali inajipanga kusambaza
umeme na kufikiwa vijiji vyote na kubainisha kuwa mpango huo unakwenda
sambamba na uanzishaji wa vyanzo vya umeme ili viweze kuzalisha megawati
3,000 ifikapo 2015 na kwamba ziada itauzwa nje ya nchi.
Septemba 2 mwaka huu, Serikali kupitia Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) ilitangaza kuanza kwa awamu ya pili ya usambazaji
wa umeme vijijini, mpango ambao utagharimu Sh881 bilioni na kukamilika
Juni 2015.
Katika utekelezaji wa mradi huo, huduma za jamii
zitakazopewa kipaumbele katika kuunganishiwa umeme ni shule, zahanati,
misikiti, makanisa na visima vya maji.
Mpango huo unatarajiwa kuinufaisha mikoa 24 ya
Tanzania Bara, huku wateja 250,000 wa awali wakiunganishwa pamoja na
kuhusisha kazi ya usambazaji umeme kwenye makao makuu ya wilaya 13
zisizokuwa na umeme.
Mwenyekiti wa Bodi ya REA, Balozi Ami Mpungwe
alisema tayari mikoa 14 imepata makandarasi na ujenzi wa vituo sita vya
usambazaji umeme, wakati mchakato wa kuwapata wajenzi katika mikoa 13
iliyokosa wakandarasi awali, unaendelea.
Awananga viongozi wa CCM
Rais Kikwete amewananga baadhi ya viongozi wa chama chake na
kusema kuwa ni dhaifu katika uongozi kwani wameshindwa kueleza mafanikio
ya Serikali chini ya CCM.
“Baadhi ya viongozi wa CCM pamoja na wanachama
wamezubaa kiasi cha kushindwa kuzungumzia mafanikio ya Serikali
inayoundwa na CCM, lakini wamekuwa mahodari wa kujadili wanapobezwa na
wapinzani.
“Tatizo lenu CCM mmezubaa, huo ndiyo udhaifu wenu
mkubwa, kupata maji ya bomba ni hatua kubwa na maendeleo, lakini
viongozi wa CCM nyie mmezubaa na ni dhaifu, hamuwezi kueleza mafanikio
haya, lazima niliseme hili na ujumbe uwafikie,” alieleza na kuongeza.
“Kwa nini mnasubiri mimi nifike hapa ndipo mje
kwenye miradi kama hii, mimi nikija huku siji nikiwa nimebeba miradi hii
mgongoni, kwa nini mmekuwa dhaifu wa kuyasema haya na badala yake
mmekuwa hodari wa kushupalia dosari zinazosemwa na wapinzani na kuacha
mazuri haya?”
alisema Kikwete.
Alisema Tanzania ni nchi kubwa kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki, lakini ina mtandao mkubwa wa barabara kuliko nchi kama Kenya, lakini akawalaumu watu wanaoisifia nchi hiyo jirani na kubeza mafanikio ya Serikali yake.
alisema Kikwete.
Alisema Tanzania ni nchi kubwa kuliko nchi zingine za Afrika Mashariki, lakini ina mtandao mkubwa wa barabara kuliko nchi kama Kenya, lakini akawalaumu watu wanaoisifia nchi hiyo jirani na kubeza mafanikio ya Serikali yake.
Azungumzia Elimu
Wakati huohuo, Rais Kikwete amewaagiza wakuu wa
mikoa kuhakikisha kila sekondari ya kata inakuwa na maabara zenye vifaa
viliyokamilika na kwamba atakayeshindwa kufanya hivyo atamwajibisha.
Alisema vijana lazima wasome katika shule zenye
vifaa na kusisitiza kuwa, kwa sasa Serikali imekamilisha mpango wa
kusambaza walimu ili kukabiliana na uhaba uliopo.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali inajiandaa kukamilisha mpango wa Tehama kwa shule zote nchini kutokana na kuwapo kwa mtandao wa mawasiliano kupitia mkongo wa taifa.
-Mwananchi.
Rais Kikwete alisema kwa sasa Serikali inajiandaa kukamilisha mpango wa Tehama kwa shule zote nchini kutokana na kuwapo kwa mtandao wa mawasiliano kupitia mkongo wa taifa.
-Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment