Wanfunzi wa darasa la saba wafanya mitihani chini ya Ulinzi mkali.

 

WANAFUNZI wa darasa la saba jana walianza kufanya mitihani yao ya kuhitimu elimu ya msingi, huku katika Jiji la Dar es Salaam ulinzi mkali ukiwa umeimarishwa katika shule mbalimbali Tofauti na miaka ya nyuma, ambapo ulinzi umekuwa ukifanywa na askari wa kawaida, lakini mwaka huu ulinzi umeimarishwa kwa kuwapo Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).

Ulinzi huo mkali ulionekana zaidi katika shule za msingi za Serikali, huku katika shule zinazomilikiwa na watu binafsi, kukiwa na ulinzi wa kawaida.

MTANZANIA ilitembelea katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam, ikiwamo Shule ya Dk. Omari Ali Juma, Karume, Mianzini, Mburahati, Mapinduzi, Buguruni Viziwi, Mtakatifu Agostino, Atlas, Mtakuja, Kombo, Mugabe, Al-hikma, Hekima, Buguruni ‘A’ na German Rutihinda.

Mlinzi wa Shule ya Msingi Dk. Omari Ali Juma ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema: “Hali ya ulinzi ni kali sana, tofauti na miaka yote.

“Miaka iliyopita kulikuwa na askari polisi na wasimamizi, lakini leo wapo hadi FFU, sisi wenyewe haturuhusiwi kusogea maeneo ya madarasa, zamani haikuwa hivi,” alisema mlinzi huyo.

Baadhi ya shule mageti yake yalifungwa na wanafunzi hawakuruhusiwa kutoka nje ya shule kipindi cha mapumziko.

Wakati kukiwa na ulinzi huo, baadhi ya shule zilizopo karibu na maeneo ya barabara ikiwamo Shule ya Msingi Mianzini iliyopo maeneo ya Mburahati, Kombo na Mtakuja zilizopo Vingunguti zilitawaliwa na kelele nyingi hususani za pikipiki na muziki.

Muda mfupi baada ya waandishi kuondoka katika lango la shule hiyo, mlinzi huyo aliondoka katika eneo lake la kazi na kwenda kuwaamuru wafanyabiashara wa maduka yaliyopo karibu na shule hiyo kuzima muziki wao.

Maoni ya wanafunzi
Wakizungumza na MTANZANIA kuhusu ulinzi mkali, baadhi ya wanafunzi waliokuwa mapumziko walisema suala hilo halikuwaathiri kisaikolojia, kwani walimu wao waliwaandaa na kuwataarifu kuhusu suala la ulinzi wa aina hiyo.

Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Yusuph Makamba, iliyopo Wilaya ya Temeke, Amina Kushoka alisema: “Ulinzi ni mkali lakini hatuogopi, askari na wasimamizi wako poa kabisa, hawatukatishi tama,” alisema.

Mwanafunzi mwingine, Angella Godwin alisema katika mitihani waliyoifanya jana hakukuwa na mtihani mgumu tofauti na mtihani uliopita wa Mock.

“Matarajio ya kufaulu ni makubwa sana kutokana na mitihani ilivyotungwa ni mitihani ya kawaida na hakuna sababu ya kufeli, tunaomba Watanzania watuombee,” alisema Angella.

Kwa upande wake, Abdallah Abdul alisema: “Tumeshawahi kufanya mitihani mingi ukiwamo wa Mock, hatujawahi kulindwa na askari kama hivi.

“Kitu kilichotusaidia walimu walituandaa mapema na kutueleza kuwa mtihani huu tutalindwa na askari, hatujaathirika maana hawaingii kwenye vyumba vya mitihani,” alisema.

Hata hivyo alisema mtihani wa Sayansi na Kiswahili ilikuwa ya kawaida isipokuwa mtihani wa hisabati.

“Maswali yote ya hisabati yalikuwa ya kuchagua, lakini kuanzia swali la 40 mpaka 50 yalikuwa magumu,” alisema Abdul.

Naye Asengo Hamis alisema katika ufanyaji mtihani huo hakuna changamoto iliyowapata kwa sababu vifaa vyote vya kufanyia mtihani vilifika kwa wakati na vipo vya kutosha.
 
@Mtanzania
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment