Siku ya
UKIMWI Duniani iliasisiwa rasmi na
Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa
(WHO) mwaka 1998 na
imeendelea kuadhimishwa kila mwaka ifikapo Desemba mosi kwa uratibu wa Shirika
la Umoja wa Mataifa la Kupambana na UKIMWI (UNAIDS).
Maadhimisho
haya hutoa fursa ya kutathmini hali halisi na mwelekeo wa udhibiti wa UKIMWI na
vilevile kubaini changamoto, mafanikio na mikakati mbalimbali katika kupambana
na janga hili.
Siku hii pia hutoa nafasi ya kuwakumbuka wale wote waliopoteza
maisha yao kutokana na janga la UKIMWI na kuwajali yatima waliotokana na janga
hili. Katika ngazi ya kitaifa siku hii huadhimishwa kwa mzunguko katika mikoa
yote ya Tanzania Bara na mwaka jana iliadhimishwa kitaifa mkoani Lindi.
Mwaka huu
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam
wameratibu maadhimisho haya kitaifa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Katika ngazi ya kitaifa mwaka huu maadhimisho haya yalianza kuanzia tarehe 25
Novemba 2013 na yanafikia kilele chake tarehe 1 Desemba 2013.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa
kuwa Mgeni Rasmi kwenye kilele cha maadhimisho haya yatakayotanguliwa na
matukio mbalimbali ikiwemo Maonyesho ya Shughuli za wadau wa udhibiti UKIMWI
Nchini yaliyoanzakufanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja Mkoani Dar es Salaam
kuanzia tarehe 25 Novemba 2013.
Vilevile
katika maadhimisho hayo kulikuwepo na
kongamano la kitaifa la kutathmini hali na mwelekeo wa udhibiti UKIMWI nchini
lililofanyika tarehe 27 na 28 Novemba 2013 kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa
Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.
Kauli mbiu
ya maadhimisho ya mwaka huu inaendelea kuwa “TANZANIA BILA MAAMBUKIZI MAPYA YA
VVU; VIFO VITOKANAVYO NA UKIMWI NA UNYANYAPAA INAWEZEKANA”. Kauli mbiu hii
inalenga kutoa msukumo wa utekelezaji wa mikakati ya kudhibiti UKIMWI kitaifa
na kimataifa ili kufikia azma ya sifuri tatu (3) yaani maambukizi mapya sifuri,
vifo sifuri na unyanyapaa sifuri ifikapo mwaka 2015. Kauli mbiu hii inahimiza
utekelezaji wa dhati wa Malengo ya Maendeleo ya Milenia (Millennium Development
Goals-MDGs) na maazimio yaliyowekwa kwenye Mkutano Maalum wa Umoja wa Mataifa
kuhusu UKIMWI uliofanyika mwaka 2001 Jijini New York, Marekani.
Hata hivyo wito umetolewa kwa wananchi katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na sehemu za
kazi, makanisani, misikitini, mashuleni, na katika jumuia zetu mbalimbali
kuadhimisha siku hii kwa njia mbalimbali kama vile Makongamano, Kumbukumbu za
Wapendwa wetu waliofariki kwa UKIMWI, Midahalo, Mikutano ya wazi, Vipindi
kupitia vyombo vya habari, Kutembelea na kutoa misaada kwa yatima na wagonjwa
wa UKIMWI, Kuzima mishumaa nk.
“TANZANIA BILA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU, VIFO VITOKANAVYO NA UKIMWI NA UBAGUZI NA UNYANYAPAA INAWEZEKANA”
Written by:Emanueli Onesmo NdanshauPosted by:http://www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment