Raia watatu wa China wamekamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na meno 706 ya tembo, sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini.
Pia watuhumiwa hao wa Kichina wamekutwa na fedha taslim shilingi milioni 30.2 za Kitanzania, sawa na zaidi ya dola elfu 18 za Kimarekani.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki akifuatana na kikosi maalum cha polisi, waliwanasa Wachina hao katika makaazi yao jijini Dar es Salaam.
Waliokamatwa na meno hayo ya tembo wametajwa kuwa ni Chen Jinzha, Huang Qin na Xu Fujie wote kutoka mji wa Guangdung nchini China.
Raia hao wa China wamekuwa wakiishi katika nyumba walimokamata meno ya tembo kwa miaka mingi wakifanya biashara ya kuingiza vitunguu swaumu nchini Tanzania kutoka China huku wakisafirisha nje makombe ya konokono wa baharini.
Akizungumza na waziri Kagasheki, mtuhumiwa Huang Qin amesema shehena yote iliyokamatwa ndani mwake ilikuwa ikiletwa kidogo kidogo na rafiki yake ambaye hakumtaja jina.
Kukamatwa kwa meno haya ya tembo Jumamosi, kumekuja wakati tayari serikali imetangaza kusitisha "Operesheni Tokomeza Ujangili", ambayo ililenga kunusuru wanyama walio hatarini kutoweka kutokana na kuuawa katika hifadhi za taifa nchini Tanzania. Wanyama wanaolengwa zaidi na majangili kutokana na meno yao na pembe ni tembo na faru.
Matukio ya kukamatwa kwa meno ya tembo kutoka Afrika Mashariki yamekuwa yakiripotiwa kila mara. Oktoba, 20, 2012, tani nne za meno ya tembo yenye thamani ya dola milioni 3.4 za Kimarekani yalikamatwa Hong Kong, yakidaiwa kusafirishwa kutoka Kenya na Tanzania.
Pia Agosti 16 mwaka huu polisi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, walimkamata raia mmoja wa Vietnam akiwa na meno ya tembo yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 18 sawa na dola za Kimarekani zaidi ya elfu 11, yakisafirishwa kwenda nje.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment