PROF. LIPUMBA KUGOMBEA URAIS 2015

Mwenyekiti Chama cha Wananchi (CUF),Profesa Ibrahim Lipumba. 

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimemnadi Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kugombea kwa mara nyingine kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015, huku yeye binafsi akitangaza neema kwa Watanzania ya kuwajaza fedha mifukoni.

Katika mkutano wa uzinduzi wa operesheni ya mchakamchaka kuelekea mwaka 2015 uliofanyika juzi katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanga cha Ndege Morogoro, viongozi wengi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, walimnadi Prof Lipumba jukwaani wakidai kuwa bado ni kiongozi anayestahili kugombea wadhifa huo kupitia CUF.
Awali kabla ya kufanyika kwa mkutano huo uliopambwa na shamra shamra za ngoma zilizoanza siku mbili kabla ya uzinduzi huo zikiambatana na baadhi ya wafuasi na wapenzi wa chama hicho kupita katika mitaa mbalimbali ya mji wa Morogoro  wakiperusha bendera, uliingia dosari baada ya kutanguliwa na mvua kubwa iliyokwamisha baadhi ya shughuli na kuchelewa kuanza kwa mkutano huo.
Mvua hiyo ilianza kunyesha Saa 9.40 jioni mara baada ya mabasi madogo takriban 15 yaliyowabeba wanachama, wafuasi na viongozi wa CUF kutoka Dar es Salaam kuwasili katika viwanja vya mkutano,hali ambayo iliwalazimu viongozi wa juu kuanza na zoezi la kufungua matawi ya jumuiya za vijana na jumuiya ya akinamama kabla ya kwenda kuhutubia.
Akizungumza katika mkutano huo, Profesa Lipumba alisema utatifi uliofanywa katika baadhi ya nchi duniani zikiwamo nchi za Brazil na Mexico umebaini kuwa njia nyepesi ya kumuondolea mwananchi umasikini ni kumpatia fedha taslimu.
Prof Lipumba ambaye ni mtaalamu wa masuala ya uchumi,alisema kuwa jambo hilo linawezekana kufanyika nchini kwa kutumia teknolojia ya simu za mikononi na kuwapo kwa vitambulisho vya taifa vinavyotumia alama za vidole kama alama za ulinzi.
Alisema India yenye watu zaidi ya bilioni 1.2 imefanikiwa kutumia vitambulisho vya taifa katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na uhifadhi na usalama wa fedha zao na hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kuchukua vitambulisho hivyo vinavyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema  chama chake kikipewa ridhaa na Watanzania ya kuongoza nchi kitatumia rasilimali zilizopo nchini za madini, gesi, mafuta, mbuga za hifadhi na maeneo ya utalii kuweza kuboresha miundombinu, lakini kuwapatia fedha taslimu wananchi ikiwa ni njia rahisi ya kupambana na umasikini.
Mwenyekiti wa CUF alisema  nchi nyingi duniani zilizopata nishati ya gesi na mafuta zimejikuta katika mgogoro mkubwa ikiwa usimamizi wa raslimali hiyo utawanufaisha wachache na kutolea mfano wa Nigeria.

 Profesa Lipumba alidai kuwa watafiti wamegundua kuwa gesi iliyogunduliwa Mtwara inafuti za ujazo trioni 33, kiwango ambacho kinaweza kuvunwa kwa zaidi ya miaka 10 na kina uwezo wa kuingizia serikali wastani wa pato la Sh 6.5 bilioni (USD 4 milioni) mpaka Sh 8.1 bilioni (USD5 milioni) kwa mwaka.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment