PITIA HOJA ZA HATI YA MUUNGANO PAMOJA NA MAWAZIRI WA ZANZIBAR WALIOLIPULIWA BUNGENI DODOMA HAPA!!


Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba,Ismail Jussa Ladhu.
 
Mjumbe  wa Bunge Maalumu la Katiba, Ismail Jussa Ladhu, amewalipua mawaziri watatu wa Zanzibar kuwa ni ‘wanafiki’ kutokana na kushindwa kusimamia msimamo wao kuhusiana na Muungano. 
Jussa alitoa kauli hiyo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha maoni ya wajumbe wachache wa Kamati Namba Sita kuhusu Sura ya Kwanza na ya Sita ya Rasimu ya Katiba.

Aliwataja baadhi ya mawaziri, ambao walionyesha msimamo wao wakiwa Zanzibar na  baada ya kufika Dodoma wamegeuka, kuwa ni pamoja na Waziri wa Fedha, Yusuph Omary Mzee; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Utawala Bora), Mwinyi Haji Makame na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Kazi), Haroun Ally Suleiman. 
Jussa alisema mawaziri hao wote walikuwa wakionyesha kukasirishwa na jinsi Muungano huo ulivyoisababishia Zanzibar kukwama kiuchumi.
 
“Mheshimiwa mwenyekiti, kuna rekodi hata na CD ya semina ya Baraza la Wawakilishi lililoitishwa na Mheshimiwa Spika wetu, Ameir Pandu Kificho…nashukuru sana Spika wetu, mawaziri watatu walionyesha ni jinsi gani wamedhalilishwa na Muunganoo huu. Lleo kimewapata nini Dodoma? Mimi sijui,” alisema Jussa.
 
Alisema kuna siku walikuwa wanajadili muswada wa kurekebisha sheria na kwamba, alipendekeza neno moja kwa njia ya maandishi ili kutoa kipaumbele cha ajira kwenye sekta ya utalii upande wa Muungano kisiwapo ila kiwapo kwa Zanzibar kwa kuwa ndiyo sekta ya utalii ilipo.
 
“Tukakataliwa. Mimi na Mheshimiwa Asha Bakari tulitoka naye nje ya Baraza la Wawakilishi, huku Asha akisema wenzie wamempinga. Lakini wamekuja Dodoma wamegeuka misimamo yao,” alisema Jussa.
 
Aliongeza: “Leo sisi wajumbe wa Baraza la Wawakilishi…ambao tumesimama mara nyingi na Baraza la Wawakilishi kupigania Muungano kutoka pande zote mbili (CCM na CUF) kulalamikia…leo tumefika Dodoma, wengine wamefyata.”
 
Alisema Wazanzibar wengi hawaridhishwi na muundo uliopo sasa wa Muungano kwa kuwa umekuwa ukiwanyonya zaidi na kuwapendelea Watanganyika.
 
Jussa alisema katika mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yapo mambo 17 ya ushirikiano, lakini katika hayo, mambo manne tu ndiyo ya Jamhuri ya Muungano.
 
Aliyataja mambo hayo, ambayo wana ushirikiano na Jamhuri ya Muungano kuwa ni ushirikiano katika mambo ya fedha na uchumi, haki ya ukazi, ushirikiano katika mambo ya siasa, uhuru wa mtu kwenda atakapo na uhuru wa kazi.
 
Kuhusu upotoshaji kwamba, kuruhusu serikali tatu ni kuvunja Muungano na kumrejesha Sultani, Jussa alisema Januari 12, 2000 katika Uwanja wa Amani mbele ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Benjamin Mkapa, aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. Salmin Amour, alitoa msamaha na kumwambia Sultan kuwa anaweza kurudi Zanzibar.
 
“Je, alipokuwa anatoa msamaha huo, alikuwa anakiwakilisha chama gain? na kusema akifika serikali itampa kila aina ya msaada na arudi kuwa raia wa Zanzibar…mheshimiwa mwenyekiti kwa zana hii tunajua basi kama kuna watu, ambao wanataka kurejesha mambo ya Sultani basi kitakuwa ni Chama Cha Mapinduzi kwa kutumia kauli hii, ambayo haikufutwa hadi hii leo,” alisema.
 
Alisema ikiwa kila anayedai serikali tatu anataka kumresheja Sultani. “Najiuliza je, katika waasisi wa Afro Shiraz aliyekuwa katibu mipango badala ya Rais wa Afro Shiraz, Mzee Jumbe alipotaka serikali tatu…alikuwa na nia ya kumrejesha Sultan?” alihoji
 
Jussa alisema utaratibu wa kila siku kuzusha mzuka wa Sultani ili kuzima hoja ya serikali tatu haitawasaidia kitu chochote.
 
“Kama hoja ni kwamba, Zanzibar iliwahi kutawaliwa na Sultani…mimi nilipokuja hapa (bungeni) katika maktaba yako nilipitia katiba ya Tanganyika ya Uhuru ya mwaka 1961…katiba ile bado ilikuwa inaendelea kumtambua Malkia kama ni mkuu wa nchi ya Tanganyika,” alisema.
 
Aliongeza: “Na ilikuwa na Gavana hapa, ambaye alikuwa na mamlaka kama aliyokuwa nayo Sultani…lakini hata siku moja Watanganyika wakitoa maoni yao hawaambiwi kwamba, wanataka kurudisha Malkia au Gavana wa Tanganyika.”
 
HATI HALISI YA MUUNGANO KUWASILISHWA BUNGENI
Baada ya madai ya muda mrefu ya baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu ya Katiba kutaka hati halisi ya makubaliano Muungano wa Tanganyika na Zanzibar iwasilishwe bungeni ili kuthibitisha uhalali wake, hatimaye serikali imeahidi kuwasilisha hati hiyo bungeni. 
Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, kabla ya kuwasilisha maoni ya wajumbe wa kamati Namba Sita juu ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya katiba.
 
Wasira alisema hayo baada ya awali mjumbe wa Bunge hilo, Tundu Lissu, wakati akitoa ufafanuzi wa maoni ya wachache wa kamati namba nne kuhusiana na sura hizo, kudai kuwa hati za Muungano hazipo mahali popote, hivyo Muungano uliopo siyo halali.
 
Alisema hati hiyo ipo na imehifadhiwa katika hali nzuri, hivyo itawasilishwa bungeni ndani ya siku mbili zijazo.
 
Kauli hiyo ya Wasira ilipokelewa kwa vifijo na wajumbe wa Bunge hilo bila ya kujali tofauti zao.
 
“Naahidi kwa niaba ya dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa hati ipo na itawasilishwa hapa ndani ya siku mbili zijazo na ina sahihi za waasisi wetu, hayati Mwalimu Julius Nyerere, na marehemu Abeid Amani Karume,” alisema Wasira.
 
Kauli ya Wassira ilikuja baada ya kuwapo kwa utata juu ya hati hiyo, kwani wajumbe wengi wakati wakijadili sura za rasimu hiyo katika kamati zao, walihoji uhalali wa hati hiyo na sehemu ilipo.
 
Kumekuwa na madai kuwa hati hiyo ipo Umoja wa Mataifa (UN), huku taarifa nyingine ikisema ipo katika Ikulu ya Dar es Salaam na Zanzibar, ambako zimehifadhiwa baada ya Nyerere na Hayati Karume kutia saini na kubadilishana.
 
Pia baadhi ya wajumbe wa kamati hizo, walikuwa wakihoji sahihi za aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano, Nyerere na aliyekuwa Rais wa Serikali ya Watu wa Zanzibar, Karume wakidai kuwa zimeghushiwa.

 
 MNYIKA ASHUPALIA HATI
Pamoja na maelezo hayo ya Wasira, Mjumbe John Mnyika, aliendeleza hoja ya kutaka kuona hati halisi za makubalino ya Muungano kabla ya kuanza mjadala wa kuchambua sura hizo za rasimu ya katiba. 
Akiongea kwa jazba, Mnyika alimkumbusha Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, kuwa amemuandikia barua akiomba Bunge hilo liahirishwe hadi hapo hati halisi zitakapowasilishwa bungeni ili wathibitishe uhalali wake.
 
“Leo nimekuandikia barua rasmi nisichangie lolote hadi hati ziwasilishwe au Bunge lisianze mjadala hadi hati ziwasilishwe kwanza. Maana isijekuwa Wasira ametuuzia mbuzi kwenye gunia…” alisema Mnyika.
 
Akijibu ombi hilo, Sitta alisema: “Mwenye mamlaka ya kupanga shughuli za Bunge ni Kamati ya Uongozi na hili la Mnyika ni la ajabu. Eti kuwa asipoona hati sisi wote tuache kazi mpaka ipatikane. Haiwezekani. Na maombi ya namna hiyo hayakubaliki,” alisema Sitta.
 
Aliongeza: “Bunge hili linaendeshwa kwa gharama kubwa za wananchi. Na mambo kama hayo hayakubaliki na kuwaonya wanapoomba kitu wasimuwekee mwenyekiti bastola kichwani.”
 
Kwa upande wake, mjumbe mwingine, Freemaan Mbowe, alimpongeza Wasira kwa kuliahidi Bunge kuwa hati hizo zitawasilishwa bungeni ili wajumbe wazione.
 
Hata hivyo, aliomba hati hizo kuwasilishwa haraka badala ya kuchukua siku mbili, kwa kile alichosema zimeleta utata mkubwa na kuufanya mjadala mzima kukosa nguvu.
 
“Kwa umuhimu wa mjadala huu, serikali ina uwezo wa kuileta hati hata leo. Tunachoomba iletwe haraka, kwa sababu ndiyo msingi wa majadiliano. Uhalali wake tutaangalia itakapoletwa na kuiona,” alisema Mbowe.
 

MBOWE ATAKA BUNGE LIVUNJWE
Mjumbe Freeman Mbowe, ametaka Bunge hilo livunjiliwe mbali kama msingi wake wa serikali tatu haukubaliki. 
Aidha, amewataka wajumbe wanaowakilisha mapendekezo ya wengi wasiwabeza wajumbe wa tume kwani ni viongozi waandamizi wa serikali wanaoongoza nchi.
 
Akianza na hoja kuvunja Bunge hilo, Mbowe alisema kama rasimu inapuuzwa na kulazimisha kufuata mapendekezo ya serikali mbili hakuna haja ya kuendelea kuijadili.
 
Anaungana na Juma Duni Haji, aliyetahadharisha kuwa iwapo rasimu ya katiba ya serikali tatu haitakiwi serikali irudi tena kwa wananchi kuwauliza wanataka muundo gani.
 
“Tunapuuza msingi wa rasimu, ambao umetuweka hapa leo ni bora hii isiwepo ili aiandaliwe rasimu nyingine ya serikali mbili ambayo haijapendekezwa na tume.”
 
KASHFA KWA TUME
Alipinga kuwakashifu viongozi walioandaa rasimu hiyo, Jaji Joseph Warioba, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na Mwanasheria Mkuu, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, na Katibu Mkuu wa uliokuwa Muungano wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk. Salim Ahmed Salim. 
Alitaja baadhi ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuwa ni watumishi wa umma, wakiwamo waandamizi kutoka Ikulu na Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
 
Mbowe alisema viongozi hao ndiyo waliotafiti, kuchambua nyaraka na kusikiliza maoni ya umma na kuandaa ripoti inayokashifiwa.
 
Alisema wanapohukumiwa kuwa wamefanya kazi chafu ya kuchakachua takwimu, umma uelewe kuwa takwimu hizo zimetangenezwa na watumishi waandamizi wanaoongoza serikali. 

 “Viongozi wanaohudumu katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano na na ya SMZ,” alitahadharisha.
 
Aliongeza: “Mnapobeza taarifa ya tume ambayo ni ya viongozi wa serikali na chama tawala mjue kuwa mnaikana serikali yenu na kuwakana watu wenye dhamana ya kusimamia nchi.”
 
Akizungumzia gharama, alisema taifa limetumia kodi za wananchi kuendesha tume hiyo na kwa mujibu wa taarifa za Bunge, karibu Sh. bilioni 68 zimetumika kufanya utafiti, ambao walio wengi leo wanaukana.
 

KUPINGWA

Wakati akiwasilisha taarifa hiyo, Mbowe alionywa na Mjumbe Fahmi Dovutwa, kuwa asiwatishe wala kuwazuia wajumbe kusema wanaloamini. 
Alisema wajumbe wasikosolewe wanapohoji tatizo lililofanywa na kiongozi aliyeshika mamlaka. Alitaka watu wavumiliane na wajumbe wakubali ukweli.
 
Mbowe akimjibu Dovutwa, alisema hayuko bungeni kutetea wala kulaumu, bali kuzungumza hoja.
 
 “Warioba akikosea ama hayati Mwalimu Julius Nyerere watakosolewa. Lakini wakiwa na jambo jema wasifiwe,” alisema.
 

KIGWANGALLA AMTUHUMU SITTA
Wakati hayo yakijiri, hali ya kutoaminiana iliendelea kutawala katika Bunge hilo, baada ya Mjumbe Dk. Hamis Kigwangalla, kumtuhumu Sitta kuwa anapendelea upande wa wachache.
 
Dk. Kigwangalla alitoa tuhuma hizo bungeni jana baada ya kuomba utaratibu mara baada ya Sitta kumuita mjumbe wa kamati namba nne, Tundu Lissu, kumalizia muda uliobaki Ijumaa iliyopita kutokana na Bunge kuahirishwa kabla ya muda wake wakati akitoa ufafanuzi wa taarifa ya wachache ya kamati yake.
 
 Sitta aliahirisha Bunge hadi jana kutokana na kukatika ghafla kwa matangazo ya moja kwa moja ya Kituo cha Televisheni cha TBC wakati Lissu akitoa ufafanuzi huo.
 
Katika kikao cha jana, Sitta alimruhusu Lissu kumalizia kiporo cha muda uliobaki kabla ya kamati nyingine zilizokuwa zimesalia kusoma taarifa zao kuhusiana na sura ya kwanza na ya sita za rasimu ya katiba.
 
“Kama mnavyokumbuka Ijumaa tuliahirisha Bunge wakati Lissu akiendelea na kutoa utetezi wa wachache kwenye kamati yake kutokana na matatizo yaliyotokea TBC. Sasa namruhusu aje amalizie dakika 16 zilizokuwa zimebaki ili tuendelee na mambo mengine,” alisema Sitta.
 
Wakati Lissu akielekea katika sehemu maalumu ya mzungumzaji, Dk. Kigwangalla alisimama na kuomba utaratibu, akitaka na yeye apewe muda wa kusoma taarifa ya wachache, kwa maelezo kuwa amepata taarifa kuwa matangazo ya TBC yalikatikia wakati na yeye akiendelea kusoma taarifa ya wengi.
 
“Mheshimiwa Mwenyekiti ili haki itendeke na mimi naomba nipewe nafasi ya kusoma taarifa ya wengi, nimepata taaarifa kuwa mitambo ya TBC ilizimika wakati na mimi nikisoma taarifa, Sababu gani Lissu apewe nafasi na mimi nisipewe,” alisema.
 
 Aliongeza: “Lakini Mwenyekiti umekuwa ukisikiliza zaidi upande wa wachache, unawapendelea, mimi siridhishwi na upendeleo huu.”
 
 Alidai muda uliokuwa umebaki kwa Lissu kumaliza kutoa ufafanuzi ulikuwa ni dakika mbili, lakini Sitta alimpa dakika 16.
 
 Akijibu taarifa hiyo, Sitta, alisema: “Nimesikitika kutuhumiwa kuwa nawapendelea wachache. Mimi nategemea wataalamu makatibu wangu hapa ambao wameniambia kuwa muda uliobaki ni dakika 16 na si dakika mbili. Lakini kama kuna mtu anahisi ninapendelea alete malalamiko kimaandishi kwa mujibu wa kanuni yatashughulikiwa.”
 
 Kuhusu madai ya  Dk. Kigwangalla kutaka na yeye apewe muda wa kusoma taarifa ya wachache, Sitta, alisema wakati matangazo ya TBC yalipokatika Lissu akitoa ufafanuzi wa taarifa ya wachache, kuna mjumbe alisimama na kuomba muongozo juu ya suala hilo, lakini kwa upande wa Kigwangalla hakupewa taarifa yoyote kuwa kulikuwa na tatizo hilo.
 
Pia alisema uchunguzi uliofanywa haujathibitisha kama ni kweli kuwa matangazo yalikatika wakati Dk. Kigwangalla akisoma taarifa ya wengi hivyo hawezi kutoa taarifa hiyo.
 
Hata hivyo, Sitta, aliwatahadharisha wajumbe kuwa kutokana na hali ya hewa kutotabirika, hasa katika mikoa ya Pwani, ambako mvua kubwa zinanyesha, mitambo ya televisheni ikizimika Bunge halitaahirishwa tena.
 
LISSU
Lissu jana aliendelea na madai yake yake kuwa hati za makubaliano ya Muungano hazipo mahali popote, hivyo Muungano uliopo siyo halali.
 
Alidai Mwasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliivunja Tanganyika na kuungana na Zanzibar kuwa Jamhuri ya Tanzania kwa amri (Presidential Decree) badala ya makubaliano ya pande mbili.
 
Imeandikwa na  Theodatus Muchunguzi, Abdallah Bawazir, Gaudensia Mngumi na Jacqueline Massano, Dodoma.
CHANZO: NIPASHE
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment