Waziri wa ujenzi, DK John Magufuli |
WANACHAMA
watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) leo wanatarajiwa kuchukua fomu,
kuomba ridhaa ya uteuzi wa kuwania urais wa Tanzania, wakati wakiwa
hawajatangaza nia kama ilivyo kwa wengi wao.
Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mohammed Gharib Bilal,
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na Katibu Msaidizi wa Siasa na
Ushirikiano wa Kimataifa katika Ofisi Ndogo ya CCM, Dar es Salaam, Amos
Robert wanachukua fomu leo mjini hapa.
Watatu
hao ambao hawajatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa
nchi wakipitia CCM, wataungana na mawaziri wakuu wa zamani, Frederick
Sumaye, Edward Lowassa na Balozi Ali Karume kuchukua fomu leo.
Sumaye,
Lowassa na Karume wote wamekwishatangaza nia ya kumrithi Rais Kikwete,
tofauti na Dk Bilal, Magufuli na Robert ambao hawajatangaza popote nia
yao.
Kwa
mujibu wa Katibu wa Halmshauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) wa
Oganaizesheni, Dk Muhammed Seif Khatib, Robert atakuwa wa kwanza
kuchukua fomu leo kuanzia saa nne asubuhi katika Makao Makuu ya CCM.
Dk Khatib
alisema Katibu Msaidizi huyo atafuatiwa na Sumaye saa 5:30 asubuhi, Dk
Bilal atafuata saa saba kamili, Balozi Karume saa 8:30 mchana, Lowassa
ambaye aliahirisha jana atafuata saa 9:30 alasiri na Magufuli atafunga
dimba kwa leo atakapochukua saa 10:30 jioni.
Lowassa
aliahirisha kuchukua jana baada ya kuelezwa kuwa ilitokana na kushiriki
kuaga mwili wa aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, marehemu Eugen Mwaiposa,
ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati yake ya Mambo ya Nje ya Bunge la
Tanzania.
Aliagwa
bungeni. Dk Bilal alikuwa mmoja wa wanaCCM waliowania urais wa Zanzibar
mwaka 2010 na alishindwa na Rais Dk Ali Mohammed Shein katika uteuzi wa
CCM.
Rais
Kikwete baadaye alimpendekeza kuwa Mgombea Mwenza na aliposhinda awamu
yake hiyo ya pili kuiongoza nchini, akawa Makamu wa Rais.
Dk
Magufuli amekuwa akitajwa kuwa mmoja wa wanaCCM wanaofaa kwa urais wa
Tanzania, na hajawahi kutangaza nia yake, ingawa vyombo vya habari
vimekuwa vikimtaja kuwa miongoni mwa wanaofikiria nafasi hiyo.
Awali
jana, wagombea wanne waliokwisha kutangaza nia, walifungua pazi la
uchukuaji fomu za uteuzi wa CCM ambazo zitatolewa hadi Julai 2, mwaka
huu.
Wa kwanza
aliyekabidhiwa fomu na Dk Khatib alikuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya akifuatiwa na Waziri wa Kilimo,
Chakula na Ushirika, Stephen Wassira, Balozi wa Umoja wa Afrika (AU)
Marekani, Amina Salum Ali na Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki,
Charles Makongoro Nyerere.
Profesa
Mwandosya akifuatana na mkewe Lucy, aliwaambia waandishi wa habari kuwa
baada ya kushika nafasi ya tatu nyuma ya Rais Kikwete na Dk Salim Ahmed
Salim mwaka 2005, anaamini sasa zamu ni yake.
“Uamuzi
wa kuchukua fomu ni uamuzi mzito sana, inabidi ujiandae kisaikolojia kwa
maana ya kiakili, kiafya, kimaono, dhamira na dhima. Lakini kubwa zaidi
huwezi kuwa na kiburi kama hutokani na wananchi wenyewe au
huwawakilishi, kwa hiyo ni dhima kubwa,” alisema.
Profesa
Mwandosya aliongeza, “Chimwaga nilikuwa wa tatu, huko sio kushindwa.
Nikasema nimepata shaba si haba, sasa yule wa pili hayupo, kwa hiyo,
naamini ni wakati wa kupata dhahabu.
Ofisi
yangu sasa iko ghorofa ya chini, ninachoomba ni kupanda ngazi.” Kwa
upande wake, Wassira naye akifuatana na mkewe, alisema uzoefu wa muda
mrefu serikalini pamoja na uchapakazi na uadilifu wake, ni miongoni mwa
sababu zinazomfanya aombe ridhaa ya uteuzi huo.
“Kwa
hiyo, naomba nianze safari, siyo safari kama ile nyingine, hii ni safari
ya uhakika ya kutafuta fursa, kwa nia, kwa uwezo, na sababu ninao
uzoefu, hili sio jambo la bahati mbaya.
Nimeandaliwa
na niko tayari,” alisema. Balozi Amina akifuatana na waliowahi kuwa
viongozi wenzake wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Anna Abdallah na
Halima Mamuya, alisema atajenga uchumi imara wa kuiwezesha Tanzania
ijitegemee.
Alisema
chini ya kaulimbiu yake ya ‘Matumaini Mapya kwa Kizazi Kipya,’
atazingatia mambo makuu matatu ambayo ni kuongeza kasi ya ukuaji wa
uchumi kwa kupanga upya vipaumbele vya maendeleo kwa kutumia vizuri
rasilimali za nchi ili ziwanufaishe wananchi.
Alisema
anayo nia thabiti, uwezo na uzoefu wa kutosha kuizusha Tanzania kutoka
ilipo sasa, huku akiahidi kuanzisha Mahakama Maalumu ya kushughulikia
rushwa kwani alikiri ni rushwa na ufisadi ni tatizo kubwa sasa.
Kuhusu
kama Tanzania iko tayari kwa Rais mwanamke, alisema, “takwimu zinaonesha
kuwa nusu ya Watanzania ni wanawake, na kwa sababu hiyo, wanao uwezo wa
kutoa rais.
Lakini
kubwa wanawake ni waadilifu na waaminifu, wanao uwezo wa kupambana na
rushwa na ufisadi, na hata katika matukio haya, ni nadra kuwakuta.”
Aliyefunga
pazia jana alikuwa Charles Makongoro Nyerere, ambaye ni mtoto wa Baba
wa Taifa, Mwalimu Nyerere na sasa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
Makongoro
alizungumzia kwa kirefu rushwa ilivyo tatizo sasa ndani ya CCM na
kutaka zichukuliwe hatua kukabiliana na tatizo hilo haraka iwezekanavyo.
“Rushwa
ikitawala katika chama ni hatari sana, kwani kwa kuwa kina uhusiano na
serikali, basi hata huko hali itakuwa mbaya. Rushwa inaleta heshima
mbaya.
“Mwenyekiti
wetu wa CCM, Rais Kikwete amewaambia waache rushwa, lakini hawaachi.
Rais wetu siyo dhaifu, ila mstaarabu na mwenye huruma, lakini
wanamuangusha sana.
Nasema
turudishieni chama chetu,” alisema. Makongoro aliyewahi kuwa Mwenyekiti
wa zamani wa Mkoa wa Mara, alifuatana na wazee tisa kutoka Zanzibar, na
kueleza kuwa mdhamini wake wa kwanza Zanzibar atakuwa Rais wa Awamu ya
Tano, Salmin Amour Juma maarufu kwa jina la Komandoo.
Baada ya
kukabidhiwa fomu hizo, wagombea hao walianza kusaka saini za wadhamini
450 katika mikoa ya 15 ya Tanzania Bara na mikoa mitatu ya Tanzania
Zanzibar, ikiwamo ya Unguja na Pemba.
Wakati
huo huo, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja atatangaza nia ya kugombea
urais katika ukumbi wa Benki Kuu (BoT) mjini Mwanza leo.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment