YANGA YAILAZA MTIBWA 2-0 TAIFA LEO, NGASSA, `KAVU`, BALAA, SASA WAIPUMILIA SIMBA KILELENI, PRISONS YAONA MWEZI MKWAKWANI!!

YANGANAMTIBWAAGOSTI420139 

Mabingwa watetezi wa ligi kuu soka Tanzania bara, klabu ya Yanga SC  leo hii wameibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya wakata miwa wa mashamba ya Manungu Turiani Mkoani Morogoro, Mtibwa Sugar Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kupunguza pengo la pointi dhidi ya watani wao wa jadi, Simba SC  hadi kubaki tatu.

 Wanajangwani sasa wamefikisha  pointi 12 kibindoni na kupanda hadi nafasi ya pili, wakati  wekundu wa Msimbazi, Simba SC wanaendelea kubarizi kileleni kwa kujikusanyia mzigo wa pointi 15, lakini timu zote zimeshuka dimbani mara saba.
Yanga waliandika bao la kuongoza mapema dakika ya 6 kupitia kwa Mrisho Ngassa aliyepokea pasi ndefu kutoka kwa `Kaka Mkubwa` wa Yanga, Athuman Iddi `Chuji` na kumzidi akili beki wa Mtibwa sugar, Salvatory Ntebe na kuachia shuti kali lililomshinda kipa Hussein Sharrif `Casillas`.
Bao ya Ngassa kuzamisha gozi kambani, alishangalia na kuelekea kwa mashabiki wa Simba Sc akiwatambia kuwa anajua kazi yake,huku wenzake wakimfuata na kucheza kwa staili ya Ngololo ya msanii Diamond.
Yanga waliandika bao la pili dakika ya 24 kupitia kwa Didier Kavumbagu `Kavu` aliyemalizia krosi murua iliyochongwa na Mrisho Ngassa baada ya kumtoka kiufundi beki wa pembeni wa Mtibwa Sugar ambaye msimu uliopita alikuwa anakilia kuti Simba, Paul Ngalema.
Vijana wa Ernie Brandts wenye kazi kubwa ya kutetea ndoo yao msimu huu walicheza vizuri sana kipindi cha kwanza, huku Mtibwa wakijaribu kupambana lakini ngome imara ya Yanga chini ya nahodha, Nadir Haroub `Canavaro` ilikuwa imara zaidi.
Kipindi cha pili Mtibwa walikuja juu wakitafuta njia za kusawazisha mabao hayo, lakini walishindwa kupenya ngome imara ya Yanga na kushindwa hata kupata bao la kufutia machozi.
kikosi cha Yanga SC leo:  Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul dk77, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva/Nizar Khalfan dk59, Frank Domayo, Didier Kavumbangu, Mrisho Ngassa na Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk80.
Mtibwa Sugar:  Hussein Sharif, Hassan Ramadhan, Paul Ngalema, Salvatory Ntebe/Dickson Daud dk33, Salim Abdallah, Shaaban Nditi, Ally Shomary, Awadh Juma, Mussa Mgosi/Juma Luizio dk66, Shaaban Kisiga na Vincent Barnabas/Masoud Mohamed dk37.
Mbali na mchezo huu, mechi nyingine ilikuwa katika dimba la CCM Mkwakwani Tanga baina ya Mgambo JKT  dhidi ya Prisons na kushuhudia `Wajelajela`  wakipata ushindi wa kwanza wa bao 1-0.
Ni ushindi wa kwanza kwa Prisons tangu kuanza ligi kuu msimu wa 2013/2014 na bao pekee katika mchezo wa leo limefungwa na Peter Michael dakika ya 62.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment