MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), ameeleza kutoridhishwa na majibu yaliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq, kuhusu mgogoro unaoendelea juu ya usafiri wa pikipiki ‘bodaboda’ na bajaj
.Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, amenukuliwa na vyombo vya habari akisema
hawezi kusitisha kwa muda agizo lake la kukataza vyombo hivyo vya
usafiri kuingia katikati ya jiji kwa kuwa si agizo lake bali ni sheria.
Mnyika
alisema jana kuwa mkuu huyo wa mkoa alitoa kauli hiyo kutokana na
kumuandikia ujumbe, akimtaka asitishe kwa muda utekelezaji wa tamko
lake, ili kupisha mazungumzo kati ya serikali, wahusika wa bodaboda,
bajaj na wadau wengine.
“Nimepitia sheria inayohusika ambayo ni The
Surface and Marine Transport Regulatory Authority Act, Sheria namba 9 ya
mwaka 2001, hakuna kifungu chochote kinachokataza pikipiki au bodaboda
na bajaj kuingia katika maeneo ya katikati ya jiji, hivyo mkuu wa mkoa
anapaswa kutoa ufafanuzi kwa umma ni sheria ipi anaitumia,” alisema
Mnyika katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana.
Alisema Sadiq
anapaswa kuzingatia kwamba sheria hiyo kifungu cha 5 imetamka kwamba
wajibu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini
(Sumatra) ni kulinda maslahi ya watumiaji wa huduma na kuhamasisha
upatikanaji wa huduma, ikiwemo kwa wateja wa kipato cha chini.
“Usafiri
wa pikipiki/bodaboda na bajaj sio tu umetoa fursa ya ajira kwa vijana,
bali pia unasaidia wananchi wa kipato cha chini na pia unasaidia katika
mazingira ya foleni katika Jiji la Dar es Salaam, hivyo agizo la kutaka
usafiri huo uishie Buguruni, Ubungo, Tazara na Chuo cha Uhasibu ni suala
ambalo limeibua mgogoro unaostahili ufumbuzi wa haraka,” alisema
Mnyika.
Alieleza
Mnyika kuwa anatambua kwamba vifungu vya 6, 38 na 39 vya sheria hiyo
vimetoa fursa ya mamlaka zinazohusika kutunga kanuni mbalimbali na
kwamba ielewe kanuni hizo sio sheria, hivyo kauli ya mkuu wa mkoa
haiwezi kusitisha sheria.
Aliongeza
hali hiyo inaleta hisia miongoni mwa watumiaji, waendeshaji na wamiliki
wa pikipiki/bodaboda na bajaj, kwamba pengine zipo sababu nyingine za
ziada ambazo mkuu wa mkoa anapaswa kuzieleza wazi badala ya kusingizia
sheria.
Alisema anakusudia kumwandikia barua rasmi kutaka kuitishwe kikao
cha Baraza la Ushauri la Mkoa (RCC) ambalo litakutanisha pamoja
Sekretariati ya Mkoa, Halmashauri ya Jiji, Halmashauri za Manispaa zote
za Jiji la Dar es Salaam, Sumatra na mamlaka nyingine zinazohusika, ili
kupatia ufumbuzi mgogoro huo.
Mbunge huyo ameongeza kuwa tayari ameshawaandikia ujumbe wabunge wenzake wa Dar es Salaam, waweze kuunga mkono ajenda hiyo kujadiliwa na ufumbuzi uweze kupatikana kwa maslahi ya vijana na wasafiri katika jiji hilo.
0 comments:
Post a Comment