MJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, Khamis Kigwangala, amemtuhumu
Mwenyekiti wa bunge hilo, Samuel Sitta, kuliendesha kwa upendeleo,
uonevu na ushabiki.
Kigwangala alisema Sitta, amekuwa na tabia ya kupendelea wachache
huku akidai kufanya hivyo ni kutenda haki, jambo ambalo si sahihi.
Kigwangala alitoa tuhuma hizo jana asubuhi alipotaka mwongozo wa
Mwenyekiti juu ya muda wa dakika 16 alizopewa Msemaji wa wachache,
Tundu Lissu, kumalizia hotuba yake iliyokatishwa wiki iliyopita baada
ya TBC kukatisha matangazo ya moja kwa moja.
Kigwangala alisema Lissu, alikuwa amebakiza dakika mbili, lakini
alishangazwa na uamuzi wa Sitta kuwa mjumbe huyo amebakiza dakika 16.
“Mimi pia niliambiwa wakati nasoma hoja ya kamati yangu, lakini TBC
walikuwa wakikata matangazo lakini nilipokuandikia kuhusu jambo hili
hukunisikiliza, lakini kwa Lissu naona unafanya hivyo, sasa unaona
kuwapendelea wachache ndiyo kutenda haki?” alihoji.
Akijibu mwongozo huo, Sitta alisema tuhuma hizo zimemsikitisha kwa
kuwa mambo mengi anayoyafanya anategemea wataalamu waliopo bungeni
hapo.
“Nasikitika kutuhumiwa nafanya upendeleo, mimi nategemea wataalamu
wao ndiyo wanashika saa na wao ndiyo wanasema umebaki muda fulani, mimi
sitazami saa yangu na kuamua.
“Ikiwa hawa watatu wamekosea basi ni bahati mbaya wao ndiyo
wamesema hizo dakika 16 si mimi, ni kweli jana Jumapili, uliniletea
barua nyumbani kulalamikia kuhusu kutopewa nafasi kama Lissu,” alisema.
Sitta alisema baada ya kuipata barua ya Kigwangala alimpa maelekezo
Katibu wa Bunge afuatilie TBC, kujua kama lina ukweli ndani yake na
baadae ilithibitika kuwa wakati wa Kigwangala akiwasilisha maoni
hakukuwa na tatizo la kukatika kwa matangazo.
“Jamani hili la Lissu halikuwa langu, nilitahadharishwa na
Mheshimiwa Freeman Mbowe, wote tukafuatilia tukabaini ni kweli, sasa
hili la Kigwangala, halikutolewa tahadhari,” alisema.
0 comments:
Post a Comment