Habari za uhakika zilizopatikana jana zilieleza
kuwa kiini cha mgogoro huo ni ujumbe mfupi (SMS) ambao unamtuhumu Mkono
kula njama za kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini.
Gazeti hili limedokezwa kuwa, SMS hiyo inadaiwa
kutumwa na Waziri Muhongo kwenda kwa baadhi ya wabunge akimtuhumu Mkono
kuwahonga baadhi ya wabunge Sh3 milioni kila mmoja ili kukwamisha bajeti
hiyo.
Ujumbe huo unasomeka ”Mhe Spika wa Bunge la
Jamhuri, Sisi wabunge waadilifu tunakiri kwamba Mhe Mkono ametufuata na
kutupatia fedha kila mmoja milioni 3 ili tukwamishe bajeti ya Nishati na
Madini.
Ujumbe huo umeanza pia kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Jamii Forums .
Mkono
Mkono ambaye pia ni Mwanasheria mashuhuri nchini,
alipoulizwa jana kama ni kweli amelalamika kwa Spika juu ya jambo hilo,
alikiri na kusema alichofanya ni kulalamika kwa Spika na amemwachia
alishughulikie.
“Ni kweli nimelalamika kwa Spika. Unajua taratibu
za Bunge ni kuna any complaint (lalamiko) unaliwasilisha officially
(rasmi) kwa Spika… hilo jambo lipo nimelifikisha kwa Spika wao ndiyo
watafuatilia kwa taratibu zao,”alisema.
Profesa Muhongo
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili alitolee
ufafanuzi suala hilo, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
Muhongo alituma ujumbe kwa simu ukisema:
“Tutavuka tukiwa na ushindi wa maskini na wanyonge
wa nchini mwetu. Tutaendelea kujenga uchumi imara utakaotoa ajira mpya
na matumaini mapya kwa vijana, maskini na wanyonge wa nchini mwetu.
Watanzania wamechoshwa na wizi, udalali, ubabaishaji na rushwa.”
Mkurugenzi wa shughuli za Bunge, John Joel
alipotafutwa jana alisema yeye hana taarifa juu ya jambo hilo akisema
kama lipo, basi huenda likawa mikononi mwa Spika mwenyewe.
Mvutano huo unakuja siku chache baada ya Sakata la IPTL
lililoibuliwa Bungeni Ijumaa iliyopita na mbunge wa Kigoma Kusini, David
Kafulila ambaye alisema kuna ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni katika
akaunti ya Escrow iliyopo chini ya Benki kuu ya Tanzania (BoT).
Akaunti hiyo ilikuwa ni ya pamoja kati ya IPTL na
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhifadhi malipo ya kila mwezi kwa
IPTL katika kipindi chote cha mgogoro kati IPTL na Tanesco ambao
uliishia mahakamani.
Tayari Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
limemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza sakata
hilo.
Alhamisi wiki hii, Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Jaji Frederick Werema aliliambia Bunge kuwa wapo watu wanaonunua
mashahidi kuhusiana na sakata hilo ingawa hata hivyo hakuwataja kwa
majina.
Serikali yahaha kutafuta fedha
Wakati mvutano huo ukiendelea, Serikali inahaha
kutafuta fedha ili kuinusuru bajeti ya Serikali na sasa kamati ya Bunge
ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake, Andrew Chenge imekuwa ikikutana na
Hazina karibu kila siku.
Habari zilizopatikana jana, zilidokeza kuwa bajeti
inayoiumiza kichwa zaidi ni ile ya Wizara ya Maji ambayo baadhi ya
Wabunge wameapa kuikwamisha endapo Serikali haitakuja na majibu ya
kuridhisha.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali, Wabunge wamepania
kukwamisha bajeti hiyo baada ya kugundulika kuwa wizara hiyo ilipatiwa
asilimia 30 tu ya bajeti yote ya maji iliyopitishwa na Bunge mwaka jana.
Bajeti za wizara nyingine zinazoiumiza kichwa
Serikali ni Wizara ya Ujenzi ambayo inasemekana inadaiwa mabilioni na
makandarasi na pia baadhi ya miradi hasa ya barabara haijakamilika.
Habari zinasema Serikali inaumiza kichwa kuongeza
fedha za kutoka katika Wizara hiyo ili imalize kutekeleza miradi ya
barabara ikiwamo barabara zilizoahidiwa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa
kampeni 2010.
“Unajua uchaguzi mkuu ni mwakani… Serikali ina
kibarua kigumu cha kutekeleza miradi ya barabara na inahofu CCM itakuwa
na wakati mgumu endapo kama ahadi za Rais hazitatimia,”alidokeza mbunge
mmoja.
“Kwa hiyo wabunge wengi tunachachamaa kwa sababu
tusipopata majibu katika Bajeti hii tumeliwa takuwa na wakati mgumu
majimboni na hili hatutalikubali kabisa,”alisisitiza mbunge mmoja kutoka
kanda ya Ziwa.
Kuhusu Wizara ya Maji, wabunge wanadai pamoja na kupitisha
bajeti ya ya ziada ya Sh184 bilioni mwaka jana, lakini bajeti
iliyokwenda kutekeleza miradi ni kati ya asilimia 30 na 40 tu.
Mbunge wa Ubungo, John Mnyika aliituhumu Serikali
kuwa ililidanganya Bunge kwa kushindwa kuongeza Sh184 bilioni
zilizotakiwa kuongezwa katika bajeti yake ya mwaka 2013/14.
Mnyika aliongeza kusema “Kati ya Sh184 bilioni,
Serikali imeongeza Sh86 bilioni tu…Maana yake ni kwamba Sh98 bilioni
hazijatoka mpaka sasa kwenda kwenye miradi ya jamii”.
Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Serikali za
Mitaa (Laac), Rajabu Mmbaruk, jana aliliambia gazeti hili kuwa kwa jinsi
bajeti za wizara zinavyopigwa panga, ni dhahiri Serikali inapitia
wakati mgumu.
Hata hivyo, mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles
Mwijage, alisema inavyoonekana Serikali imekuja na mapinduzi makubwa ya
bajeti kiasi kwamba haitaki tena kuwasilisha bajeti zisizotekelezeka.
“Wewe unakumbuka mwaka jana bajeti ya maji
ilikwama hadi Serikali ikaongeza fedha, lakini hizo fedha zilienda zote?
Na hili ndilo linaloleta shida hata kwenye bajeti ya mwaka huu,”alisema
Mwijage.
Mwijage aliongeza kusema” huko nyuma Serikali
ilikuwa inapitisha bajeti kuwafurahisha wabunge ili wapitishe bajeti,
lakini kwa kweli nyingine hazitekelezeki na hilo limeleta mgogoro mkubwa
kwa bajeti ya Maji”.
Kutokana na upepo huo mbaya, Serikali kupitia
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Uratibu na Bunge), William
Lukuvi aliandika barua kwa Spika akiomba bajeti ya wizara hiyo isogezwe
mbele.
Katika barua hiyo ambayo Lukuvi alilithibitishia
gazeti hili kuiandika, alipendekeza bajeti ya Wizara ya Maji na ile ya
Nishati na Madini, zote zisogezwe mbele hadi mwezi Juni badala ya kusoma
mwezi huu.
“Kwa kuwa Wizara hizi bado zipo katika mazungumzo
na Wizara ya Fedha kuhusu bajeti zao, ninaomba ukubali wizara hizi
kubadilishiwa tarehe za kuwasilisha ili ziwasilishe mwezi Juni,”inasema
barua hiyo.
Barua hiyo ya Lukuvi ya Mei 10,2014 yenye
kumbukumbu 1/CEB.274/420/02 iliyotumwa kwa Spika, Anne Makinda, ilitumwa
pia kwa Waziri mkuu, Waziri wa Maji na Waziri wa Nishati na Madini.
Hata hivyo, taarifa
iliyopatikana jana, zinasema katika kujaribu kukokoa jahazi, kamati ya
bajeti, juzi ilikutana na walipa kodi wakubwa nchini ikiwamo Kampuni ya
Bia Tanzania (TBL) kubadilishana mawazo.Taarifa zisizo rasimi zinasema
Serikali inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha na hiyo inasababishwa na
bajeti nyingi za wizara kupunguzwa, mfano ukiwa wizara ya Mambo ya Ndani
iliyopunguzwa kwa Sh500 bilioni.
0 comments:
Post a Comment