TAFITI NYINGI ZA WANAFUNZI VYUO VIKUU HUNUNULIWA MITAANI BADALA YA KWENDA SEHEMU ULIYOPANGIWA NA KUZIFANYA TAFITI HIZO!!

jengo_9a969.jpg
Wakati Serikali ikiwa katika hatua za utekelezaji wa Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwenye elimu, imebainika kuwa baadhi ya wanafunzi wa vyuo vikuu wanaohitimu, wanafanya udanganyifu kwenye utafiti kwa kufanyiwa na watu wengine au kununua uliokwisha andikwa.

Kila mwanafunzi anayesomea shahada ya kwanza, uzamili au uzamivu hutakiwa kufanya utafiti ikiwa ni sehemu ya vigezo vya kukamilisha masomo yake.
Hata hivyo, Mwananchi imebaini kuwapo kwa wanafunzi wengi wanaotumia mbinu mbalimbali za kuandika utafiti huo bila kwenda maeneo husika.
Uchunguzi wetu uliofanyika kwa muda mrefu kwenye vyuo mbalimbali jijini Dar es Salaam, umebaini kuwa baadhi ya wanafunzi huchukua tafiti za zamani na kuzinakili upya, huku wengine wakichukua kutoka kwenye mitandao na kuzifanyia marekebisho kidogo ili zifanane na eneo analotaka kufanyia utafiti huo.
Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF), Dk Donatila Kaino anasema ni asilimia 20 tu ya wanafunzi wanaomaliza vyuo vikuu nchini, ndiyo wanaoweza kuandika utafiti kwa ufasaha.
Anasema tatizo hilo linatokana na mfumo wa elimu uliopo nchini ambao haumpi mwanafunzi nafasi ya kujifunza kuandika utafiti tangu akiwa shule ya msingi.
"Tatizo kubwa walimu hawafundishi; mtalaa siyo tatizo sana, kama walimu hawafundishi tangu shule za msingi hadi sekondari unategemea nini?" anahoji.
Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu
Kamishna wa Elimu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Eustella Bhalalusesa, anasema wanafunzi wanaosomea ualimu ambao wamefanya utafiti wao kwa njia ya udanganyifu, wanaweza kukwamisha mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa sababu hawatakuwa na uwezo wa kitaaluma unaotarajiwa.
Anasema alipokuwa Mkuu wa Shule ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, walibaini kuwa baadhi ya wanafunzi walikuwa wanafanyiwa tafiti hizo,
hivyo waliamua kuweka utaratibu wa kumhoji kila mwanafunzi namna ambavyo alikusanya taarifa zake.
"Walikuwa wakishaandika proposal (muhtasari) tuliwaita waje wao wenyewe waeleze, ingawa ilichukua muda mrefu kuwahoji wanafunzi wote, tulilazimika kufanya hivyo. Tulimuuliza sababu zilizomfanya aandike mada aliyoichagua," anasema Bhalalusesa.
Anasisitiza kuwa utaratibu wa kuhifadhi tafiti zote zinazofanywa na wanafunzi kwenye tovuti utasaidia kuwadhibiti watu wasio waaminifu.
Katibu Mkuu
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome (pichani) anasema kuwa watu wanaofanya biashara ya kuwafanyia utafiti wanafunzi wanaichafua sifa ya elimu ya Tanzania.
"Hawa watu wanaifanya elimu ya Tanzania ionekane ni duni wakati siyo kweli," anasema Mchome.
Anabainisha kuwa biashara hiyo ni haramu na kwamba njia pekee ya kuitokomeza ni kwa wananchi kutoa taarifa zitakazowezesha wahusika kukamatwa.
Uchunguzi wetu umebaini kuwa wanafunzi wengi huandikia nyumbani kwao utafiti wao, badala ya kwenda sehemu husika na hivyo kutoa matokeo ambayo hayafanani na eneo tajwa.
Wanafunzi waliohojiwa wanasema kiasi kidogo cha fedha wanachopewa kwa ajili ya kufanyia utafiti, ndiyo sababu kubwa ya wao kushindwa kwenda katika maeneo wanayotakiwa kufanyia utafiti.
Wanafunzi Chuo Kikuu Dodoma
Mwalimu Imani Msengezi aliyehitimu Shahada ya Elimu, Chuo Kikuu cha Dodoma mwaka jana, anasema wao hawakufanya utafiti kama ambavyo wanafanya wanafunzi wanaosomea fani nyingine. Badala yake waliandika andiko (dissertation), ambalo waliandika wakiwa katika makundi.
"Kwa kweli sisi hatukufanya research (utafiti), tulifanya dissertation, ambayo tulipewa tufanye kwenye makundi kama assignment ya darasani," anasema Msengezi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, mzazi mmoja ambaye pia ni mfanyakazi katika sekta ya elimu huko Iringa, alielezea namna ambavyo mtoto wake aliandikiwa utafiti na mtu mwingine aliyempata baada ya kushauriwa na mhadhiri wake.
Mzazi huyo ambaye hakupenda kutajwa jina lake, anasema aliambiwa na mhadhiri aliyemsimamia mwanaye utafiti kuwa atoe kiasi kidogo cha fedha ili amtafutie mtu atakayemwaandikia utafiti huo kwa kuwa anashindwa kuiandika inavyotakiwa.
Anasema: "Kwa namna anavyoufahamu uwezo mdogo wa mwanafunzi, ana uhakika kuwa hawezi kuandika utafiti utakaokidhi vigezo vinavyotakiwa.
Muda unakwenda na alichoandika hakieleweki, ni bora amtafutie mtu amsaidie kuiandika (research)... alisema siyo gharama kubwa, ni fedha kidogo tu atatakiwa kutoa."
Pia imebainika kuwa wanafunzi wengine hutoa rushwa kwa wakufunzi wao wasio waaminifu ili kuweza kufanyiwa tafiti, jambo ambalo huwafanya kujikuta kwenye wakati mgumu wanapoambiwa wayatolee maelezo namna ambavyo walifanya utafiti huo.
Tahliso
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO), Donati Salla anasema uwezo mdogo wa kitaaluma wa wanafunzi na changamoto za teknolojia zimechangia kushuka kwa kiwango cha ufanyaji utafiti hapa nchini.
Anasema mitalaa ya vyuo vikuu inatofautiana kwa kiasi kikubwa, hivyo kuwafanya baadhi ya wanafunzi kuwa na ujuzi mkubwa huku wengine wakibaki na uelewa mdogo.
"Kwa mfano, sera ya elimu haijafanya utafiti kuwa somo lenye heshima. Katika nchi nyingine utafiti ni somo linalojitegemea, lakini hapa kwetu kuna vyuo wanafanya utafiti huku sehemu nyingine wanafunzi wanaambiwa waandike project paper (miradi), hakuna uwiano," anasema Salla na kuongeza kuwa:
"Teknolojia nayo imeleta changamoto mpya. Kuna baadhi ya wanafunzi wanategemea kunakili kutoka kwenye intaneti kila kazi wanayoambiwa kufanya."
Mhadhiri Chuo Kikuu Tumaini
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini Dar es Salaam, Ajuaye Mdegela anasema wanafunzi wengi wa vyuo vikuu wanashindwa kufanya utafiti kwa sababu hawataki kutumia muda mwingi katika kusoma.
"Uwezo wa wanafunzi wa kuandika utafiti unapungua kila mwaka, wamekuwa wavivu na wasiopenda kusoma.
Hapa kwetu mwaka huu wanafunzi wawili hawatamaliza chuo kwa sababu wameshindwa kufanya utafiti," anasema Mdegela.
Anafafanua kuwa siku hizi wanafunzi wanasoma kwa ajili ya kufaulu mitihani kwa kukariri na kwamba wanashindwa kufanya vizuri kwenye utafiti kwa sababu wanatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu mada husika na si vinginevyo.
Anaongeza: "Kwa mfano unakuta mwanafunzi ameandika idadi ya watu 90 atakao wahoji kwenye muhtasi wa utafiti wake, lakini anapokwenda kuiandika anaandika watu 50 tu ndiyo aliowahoji. Hili ni tatizo kwa kuwa tofauti haipaswi kuzidi asilimia kumi," anasema.
Pia alibainisha kwamba wakati mwingine mwanafunzi anaweza kuandika taarifa zisizohusiana kabisa na mada anayoitafiti. "Inavyoonekana ni kama vile amenakili kutoka sehemu fulani akabandika huku."
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa, Esau Ntabindi anasema wanafunzi wanaohitimu vyuo vikuu siku hizi wanashidwa kusoma vizuri kwa sababu hawako makini na masomo.
Akizungumzia udanganyifu katika kuandika utafiti, Ntabindi anasema: "Kuna wakati unasoma utafiti aliuofanya mwanafunzi halafu unajiuliza kama ni kweli yeye ndiye aliyefanya."
Uchunguzi wa Mwananchi ulibaini kuwepo kwa mtu mmoja eneo la Kinondoni A, jijini Dar es Salaam, ambaye kwa muda mrefu amekuwa akiwafanyia utafiti wanafunzi wa vyuo vikuu kwa malipo ya kati ya Sh 50,000 hadi Sh 100,000.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment