SPIKA WA BUNGE LA KATIBA MH.SAMWELI SITTA KUPULIZA TENA KIPENGA AGOSTI 5 2014!!

 

Dar es Salaam.
Agosti 5 mwaka huu ‘kipenga’ kinatarajiwa kupulizwa tena na Spika wa Bunge la Katiba Samwel Sitta. Atawataka tena wajumbe wa Bunge hilo kufika Dodoma ili waendelee na ng’we waliyoacha katika kukamilisha kazi ya kupitia Rasimu ya Pili ya Katiba na kuiboresha.


Vikao hivyo vitaendelea, baada ya kushindwa kukamilika ndani ya siku 67 zilizomalizika tangu vilipoanza Februari mwaka huu.

Wakati Bunge hilo likiwa linaendelea, kuliibuka makundi mawili yanayopingana kimtazamo; Kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) linaloundwa na wajumbe wengi kutoka vyama vya upinzani na kundi la Tanzania Kwanza linaloundwa na wajumbe wengi kutoka chama Tawala CCM.

Katika mwendelezo wa vita hiyo nje ya Bunge, makundi hayo yameendelea kuendesha mikutano mbalimbali katika kile kinachoweza kuelezwa kuwa ni kushinikiza, kujitetea na hata kushtaki kwa wananchi wenzao wanaoamini kuwa wanavuruga mchakato huo.

Makundi mbalimbali ya kijamii zikiwamo asasi za kiraia kupitia Kongamano la Muungano wa Asasi za Kiraia (Azaki), lililofanyika wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, wanasema kabla ya kufikia hatua hiyo, Rais Kikwete aliyumbishwa na chama chake kuharibu mchakato wa Katiba.

Mwanaharakati wa masuala ya kijinsia, ambaye pia ni Mkurugenzi mstaafu wa Tamwa Ananilea Nkya anasema kama ni hivyo basi rais amekosea kwani ujasiri wake unapaswa kutoka kwa Watanzania badala ya chama chake.

“Kwa kuwa mamlaka yake yanatokana na nguvu ya Watanzania, ni vyema akakubali kukiri udhaifu uliojitokeza kuwa umesababishwa na chama chake, halafu atengeneze ushawishi kwa wajumbe wote kuwarejesha ndani ya mjadala wa Katiba ya Watanzania na Katiba ya Wanasiasa,” anasema Nkya.

Magige Makuli ambaye ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) anasema Rais Kikwete anaonekana kuzidiwa nguvu na chama chake, pale alipokubali kubadili mtazamo wake kuhusu mchakato wa katiba.

“Mwanzoni tuliona Rais alikuwa anakubaliana na kila hatua ya mchakato na tuliona alikuwa akikutana na Tume mara nyingi, huku akionyesha dalili za kupokea vizuri rasimu. Sasa inawezekana kuwa tofauti na chama chake ndiyo chanzo cha yeye kubadilika,” anasema Makuli.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Deus Kibamba anasema ni dhambi kubwa kuruhusu mchakato huo kutekwa na wanasiasa.

“Huu ni mchakato wa Katiba ya Watanzania, kwani katiba zote zilizopita ziliandikwa na wanasiasa. Naomba tuendelea kutumia fursa za makongamano kama haya ili kushinikiza upatikanaji wa Katiba ya Wananchi,” anasema.

Akizungumza katika kongamano hilo, aliyekuwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Profesa Mwesiga Baregu anasema kuwa mchakato ulianza kupata dosari tangu Rasimu ya Kwanza ilipozinduliwa.

Kuharibika huku kwa mchakato kuliendelea katika hatua Mabaraza la Katiba ya wilaya ambako kulikuwa na vurugu kubwa zilizotokana na shinikizo la wanasiasa.

“Mbaya zaidi, rasimu ya pili ilitokana na maoni yale yale yaliyovurugwa. Pia Kitendo cha Rais Kikwete kulihutubia Bunge la Katiba kulichangia pia dosari katika mchakato huo, kwani alionekana kuwaelekeza wajumbe hao waliochaguliwa, nini cha kufanya,” anasema na kuendelea;

“Sasa kinachosikitisha na kuhojiwa zaidi ni kwa nini Rais afanye hivyo wakati yeye ndiye anayehusika na mchakato? Ninavyofahamu Rais alikuwa anapata taarifa mara kwa mara za mchakato jinsi unavyokwenda. Lakini akahutubia Bunge kama kiongozi wa CCM, badala ya kiongozi wa nchi. Aliweka msimamo wa chama chake wa kutaka Muundo wa Serikali mbili.”

Anachotakiwa kufanya
Mwenyekiti wa Chama cha Sheria Zanzibar, Awadhi Ally Saidi ambaye ni pia ni miongoni mwa waliokuwa Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, anasema kuwa inafaa Rais awahutubie wajumbe na kuwakumbusha kuwa jukumu lao ni kujadili Rasimu ya Katiba na kuipitisha na siyo kuondoa vipengele.

“Rais apate ujasiri akiwa kama kiongozi wa nchi na siyo kama kiongozi wa CCM. Awahutubie Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na kuwataka wajadili Katiba ya wananchi na siyo ya chama wala yake binafsi,” anasema Awadh.
Anaongeza kuwa kama Rais hatalinusuru Bunge hilo na kila mtu akafanya anavyotaka au kwa masilahi ya chama chake kama ambavyo ameonyesha mfano, demokrasia nchini haitawezekana.

“Wajumbe watumie miezi miwili iliyobaki kujipanga upya iwapo wana nia ya dhati ya kuendelea na mchakato huo, ili ipatikane Katiba bora ya wananchi, vinginevyo Watanzania hawatakuwa tayari kukubaliana na hatua hiyo.

Nkya anaongeza kuwa mbali na hatua hiyo, asasi zote nchini kwa kushirikiana na Wajumbe wa Tume ya Katiba , waanzishe mikutano nchi nzima katika vijiji na wilaya kwa lengo la kuelimisha juu ya mchakato unavyokwenda.

“Baada ya hapo tutakuja na majibu juu ya dira inayotakiwa kutumika kabla ya Bunge la Katiba lijalo Endapo watashindwa kutekeleza maagizo ya Watanzania ni vyema kuanzisha maandamano ya kutangaza hali ya hatari,” anasema Nkya.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment