Hatua hiyo ilibainika jana wakati wa
kuwasilisha taarifa hiyo kwa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
iliyokutana na Msajili wa Vyama vya Siasa na CAG.
Msaidizi wa ofisi ya CAG, Benja Majura
alivitaja vyama vilivyopata hati zenye mashaka baada ya hesabu zake kuwa
na mapungufu ya kiuhasibu kuwa ni CCM, CHADEMA, CUF, TLP na
NCCR-Mageuzi.
Ukaguzi huo ulifanyika kwa mujibu wa
sheria namba 5 ya mwaka 1992 ya vyama vya siasa, iliyofanyiwa
marekebisho na sheria namba 7 ya mwaka 2009, unampa CAG mamlaka ya
kukagua hesabu za vyama vya siasa.
Katika mwaka wa fedha 2012/13 Msajili wa
Vyama vya siasa alitoa ruzuku ya sh.16.8 bilioni kwa vyama nane vya
siasa ambavyo ni CCM, CHADEMA, CUF, NCCR-Mageuzi, UDP, TLP,
APPT-Maendeleo na DP.
Vyama hivyo ni kati ya 12 vilivyowasilisha hesabu zake kwa CAG, ambapo vipo pia ambavyo vimepata hati mbaya na chafu.
Majura alivitaja vyama vilivyopata hati
chafu kwa kuwa hesabu zake hazikueleweka kuwa ni NRA, UMD,
APPT-Maendeleo, NLD, ADC, SAU na Chaumma.
Alivitaja vyama ambavyo havijawasilisha
hesabu zake na kufanyiwa ukaguzi kuwa ni pamoja na Tadea, UPDP, UDP,
Demokrasia Makini, Chausta, DP, Jahazi Asilia, AFP na CCK.
Alisema kuwa ukaguzi huo umekumbana na
changamato mbalimbali ikiwemo kukosa muongozo wa muundo wa kuandaa
taarifa za kifedha kwa vyama hivyo, kutoa karatasi moja ya mahesabu,
vyama kutokuwa na ofisi, ukosefu wa vitendea kazi.
Naye Jaji Francis Mutungi, alisema kuwa
kati ya vyama hivyo vilivyokaguliwa UMD, NLD, APPT-Maendeleo, ADC, CCM
na CUF vimewasilisha ukaguzi huo katika ofisi yake.
Alisema kuwa vyama vya NCCR-Mageuzi, CHADEMA na TLP havijawasilisha ukaguzi huo katika ofisi yake licha ya kukaguliwa.
Jaji Mutungi alivitaka vyama ambavyo havijawasilisha taarifa hizo katika ofisi yake kuhakikisha wanawasilisha taarifa hiyo kabla ya Oktoba 31 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment