Bunge la Jamhuri ya Muungano leo limejadili kitendo cha uvunjifu wa amani uliotokea kwenye maandamano ya CUF yaliyoongozwa na Profesa Ibrahimu Lipumba jijini Dar es Salaam.
Katika mjadala huo Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi Mathias Chikawe aliomba suala hilo kupewa muda wa kufanyiwa
uchunguza yakinifu na vyombo husika, wakati Mwanasheria Mkuu George
Masaju akitaka suala hilo lisijadiliwe bungeni kwa kuwa tayari
limeshafikishwa Mahakamani.
Kabla ya mjadala huo Waziri Chikawe alisoma
taarifa yake ya kile kilichotokea kwenye vurugu hizo huku akieleza kuwa
taarifa za uchunguzi wa ndani ndizo zililishawishi jeshi la Polisi
kuwaomba Cuf kutofanya maandamano yao.
Waziri Chikawe amelieleza Bunge kuwa baada ya
taarifa za polisi kutolewa wafuasi wa Chama hicho hawakutaka kutii amri
hiyo, hivyo ili kunusuru uvunjifu mkubwa wa Amani ambao ungeweza kutokea
walilazimika kutumia nguvu kuwatawanya wafuasi hao wa CUF waliokuwepo.
“Nchi yetu inaongozwa kwa mujibu wa sheria na
kanuni, haitakuwa busara kila mtu kujifanyia mambo yake anayotaka bila
kuzingatia sheria, nimeagiza vyombo husika kuchunguza suala hili, na
ikibainika kuwa polisi walitumia nguvu kubwa watawajibishwa kwa mujibu
wa sheria. Amesema Chikawe.
Baada ya kauli hiyo ndipo Mwanasheria Mkuu wa
Serikali alipolieleza bunge kuwa tayari kesi hiyo imeshafikishwa
mahakamani, hivyo kujadili suala hilo bungeni ni kukiuka sheria ya
mgawanyo wa madaraka katika mihimili ya dola,jambo ambalo lilipingwa na
idadi kubwa ya wabunge.
Pamoja na hayo Spika Anna Makinda alitoa muda wa
dakika 10 kwa wabunge kujadili suala hilo huku mbunge Tundu lissu
akilaani vikali kutokea kwa vurugu hizo na akitaka kuwajibika kwa Waziri
Mkuu Mizengo Pinda, Mwanasheria Mkuu pamoja na waziri Chikawe kwa kuwa
vitendo vinavyoendelea vinashabihiana kabisa na kauli yake ya ‘wapigwe
tu’.
Aidha wabunge wengi wa kambi ya upinzani
wakichangia hoja hiyo kwa jazba walionyesha kukerwa na kuzilaani vurugu
hizo, huku wabunge wa CCM wakitaka kusimamiwa kwa sheria bila kupendelea
mtu yeyote.
Pamoja na hayo mtoa hoja ambaye ni Mbunge na
Mwenyekiti wa chama cha NCCR-Mageuzi James Mbatia amesema kuwa suala la
Amani ya nchi ni suala la kitaifa na halitakiwi kuingizwa kwenye siasa,
hivyo aliwasihi wabunge kuwa makini na suala hilo.
“Amani na usalama wa nchi yetu ni kitu muhimu sana
katika ustawi wa taifa letu, kila siku tunashuhudia kuendelea
kuporomoka kwa amani na usalama, ninawasihi wabunge wenzangu,
tunapojadili suala kama hili lazima tuweke kando itikadi zetu, lengo
likiwa kuliponya taifa, Amesema Mbatia.
Naye Spika Makinda alihitimisha kwa kusema kuwa
anaiagiza Serikali kufanya uchunguzi kupitia vyombo vyake, pia bunge
litachunguza sheria ambazo zinatoa mwanya wa vurugu ili kudhibiti
vitendo hivyo.
0 comments:
Post a Comment