Mwanamke akiwa amepanda bodaboda huku amembeba mtoto wake . |
Zinaitwa bodaboda, kule Nigeria wanaziita okadas kwa jina
jingine ni pikipiki. Hiki ni chombo cha usafiri ambacho katika miaka ya
hivi karibuni kimeiteka miji mingi ya Afrika ikiwamo Tanzania.
Licha ya kutumika katika uhalifu, kusababisha vifo
kwa kiasi kikubwa, utafiti uliofanywa na mwandishi wetu katika maeneo ya
jiji la Dar es Salaam ambako kuna matumizi makubwa ya bodaboda ulibaini
kuwa usafiri huu unapendwa zaidi na wanawake.
Dereva wa bodaboda katika maeneo ya Tabata
Relini, Ayubu Msigala anasema idadi kubwa ya abiria wake ni wanawake.
Anasema wanawake wajawazito pia wanatumia usafiri huo kwa kiasi kikubwa.
“Zamani wanawake walikuwa wanaogopa bodaboda,
lakini sasa hata wajawazito wanatumia zaidi, hawaogopi kama ilivyokuwa
zamani,” anasema Msigalla.
Akizungumzia suala la wanawake kupenda bodaboda,
Msigala anasema wanawake waliokuwa wakiziogopa bodaboda sasa ndiyo
wanaozipanda kwa wingi huku wanawake wajasiriamali wakiongoza kuzitumia.
Anasema mamalishe, wauza nguo, vocha, hata wafanyakazi wa maofisini wamekuwa wapandaji wakubwa wa bodaboda.
“Hata akina mama wanaokwenda hospitali kupeleka
watoto hutumia zaidi usafiri huu ili kuwahi, wakati mwingine naweza
kumpakia mama na watoto wake wawili na mzigo,” anasema.
Hata wajawazito wenye kipato cha chini wameelezwa kuzitumia pindi inapowabidi na wengine zimekuwa zikiwapeka kujifungua.
Hata hivyo, idadi kubwa ya majeruhi katika wodi za MOI na Sewahaji ni wanaume jambo lililozua maswali.
Suria Mungi, mkazi wa Bunju anasema analazimika kupanda usafiri huo ili kurahisisha shughuli zake.
“Sina uwezo wa kukodi teksi halafu hapohapo nataka
kuwahi kazini inanibidi nichukue bodaboda. Cha muhimu namdhibiti
asikimbize,” anasema Suria.
Kutokana na shida ya usafiri, baadhi ya wazazi wameona kuwa usafiri rahisi kwa ajili ya watoto wanaokwenda shule ni bodaboda
“Hali ya hatari zaidi inayotuogopesha hata sisi
waendesha bodaboda wenyewe, ni pale mzazi anapokodi bodaboda kuwapeleka
shule watoto wake watatu, kila siku asubuhi na jioni,” anasema Masawe
Mkandemia.
Kati ya waendesha bodaboda 10 waliohojiwa, sita kati yao walikiri kuwa wanafunzi wanadanganyika kiurahisi na madereva hao.
“Kwanza unaweza kumpeleka shule bure na kwa fedha tunayopata ni rahisi kumhonga na akadanganyika,” anasema Mwika Marwa.
Wengine walikiri kuwa sasa wanafunzi wanazitumia ili kuepuka manyanyaso katika mabasi ya abiria.
Tatizo kubwa madereva wengi wana elimu ndogo kwani wengi wao wameishia darasa la saba.
Kwa mfano, utafiti uliofanywa na Emmanuel
Mwakapasa wakati wa kutimiza taratibu za Shahada ya Uzamili ya Unesi
mwaka 2011 katika Chuo cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (Muhas),
ilibainika kuwa asilimia 64.8 ya madereva 273 waliohojiwa jijini Dar es
Salaam, walikuwa wana elimu ya msingi na wote walikuwa wanaume.
Utafiti huo ulioitwa ‘Mtazamo juu ya matumizi ya
kofia ngumu miongoni mwa waendesha bodaboda za biashara jijini Dar es
Salaam’ ulibainisha kuwa kundi kubwa la madereva hao ni lile lenye umri
kati ya miaka 18 hadi 24.
Kundi hilo ni miongoni mwa asilimia 54 ya watu
wasio na ajira nchini wenye umri chini ya miaka 25 katika taifa la 10
duniani kuwa na kundi kubwa la vijana, taasisi isiyo ya kiserikali ya
Restless Development, yenye makao yake nchini Uingereza, imebainisha.
Mwandishi wetu pia alizungumza na wakazi wa Dar es Salaam
ambao ni watumiaji wakubwa wa usafiri huo, pamoja na madereva wa
bodaboda. Wengi walikiri kuwa bodaboda ina sura nyingi za kimanufaa kwao
licha ya kuwa na upungufu pia.
Kwanza, wasafiri walisema ni mbadala wa mabasi ya abiria na teksi kutokana na unafuu na uharaka wake wakati madereva walikiri kuwa ni ajira tosha.
Kwanza, wasafiri walisema ni mbadala wa mabasi ya abiria na teksi kutokana na unafuu na uharaka wake wakati madereva walikiri kuwa ni ajira tosha.
Hapo zamani, bodaboda ilitumiwa kama usafiri
binafsi, kwa wengine ulitumika kama sehemu ya starehe lakini kwa sasa
ongezeko la matumizi ya bodaboda unatajwa kusababishwa na kukithiri
kwa foleni, ubovu wa barabara na uhaba wa mabasi ya abiria.
Hapa nchini, bodaboda zimekuwa kimbilio la watu
wa aina zote kuanzia wenye kipato cha kati, cha chini, jinsi na rika
zote. Lakini pamoja na hayo, bodaboda zimekuwa kinara wa ajali za
barabarani.
Akitoa taswira halisi ya ajali za bodaboda,
Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga anasema ajali
hizo ni nyingi.
Kwa mfano, takwimu za mwaka 2008 hadi Oktoba 2014
zinaonyesha kuwa ajali zilizosababishwa na bodaboda zilikuwa 31,498 na
katika kipindi hicho hicho vifo 5266 vilitokea.
“Kwa idadi ya ajali hadi Oktoba mwaka huu
tunakwenda vizuri lakini kwa madhara ya vifo na majeruhi bado hali siyo
nzuri sana,” anasema Kamanda Mpinga.
Kwa mfano, kutoka Januari mwaka huu hadi Oktoba, tayari kuna vifo 799 vilivyosababishwa na usafiri huo.
Mwaka uliokumbwa na jinamizi la bodaboda kwa kiasi kikubwa ni 2013 ambapo vifo 1,098 vilitokea na ajali 6,831.
Msemaji wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI),
Patrick Mvungi anasema asilimia 55 ya majeruhi katika wodi za MOI na
Sewahaji ni za watu waliopata ajali za pikipiki.
Mwananchi ilifika hadi katika wodi ya Sewahaji
na kushuhudia wagonjwa wakiwa wamefurika hadi katika korido karibu
kabisa na mlango wa kuingilia.
Licha ya ajali hizo, idadi ya pikipiki
zinazosajiliwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga na Majini,(Sumatra),
inaendelea kuongezeka na msemaji wa mamlaka hiyo, David Mziray anasema
idadi ya pikipiki zilizosajiliwa kwa mwaka 2013 hadi Juni 30, 2014 ni
2,254. Pia katika kipindi hicho, zilisajiliwa bajaji 5,041.
Hata hivyo utengenezaji wa bodaboda na uingizaji nchini umefanya
vifaa hivyo kuongezeka na hivi karibuni gazeti dada la The Citizen
lilibainisha kuwa hadi mwishoni mwa mwaka jana kulikuwa na bodaboda 589,
936 huku asilimia 70 zikisemekana kuwapo Dar es Salaam pekee.
Pia, ytafiti ulibainisha kuwa kutoka Januari
hadi Oktoba mwaka jana zilikuwapo bodaboda 118, 047 na bajaji 27,000
karibu mara tatu ya usafiri wa daladala.
Uhalisia mwingine unaonyesha kuwa umaarufu wa
vyombo hivyo unaendelea kuongezeka na ni bahati nasibu ambazo mara
nyingi zinatoa zawadi ya bodaboda.
Kwa mfano Promosheni ya Jishindie Bodaboda kutoka
kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom, Promosheni ya Weka na Ushinde
ambapo washindi walijipatia bodaboda, baiskeli na bajaji kutoka Benki ya
NMB na NBC.
Katika Barabara ya Mandela zilizopo ofisi za
gazeti hili, ajali tano za bodaboda hutokea kila siku na kati ya hizo,
majeruhi hupatikana na wengine kufariki dunia.
Askari wa Usalama Barabarani kituo cha Tabata
Relini, Jackson Watalima anasema ajali za bodaboda ni nyingi katika
eneo hilo na kila siku idadi inaongezeka hasa nyakati za usiku.
Kutokana na kukua kwa biashara ya usafiri wa
bodaboda wauzaji pia wanazidi kuvuna faida baada ya bei ya vifaa hivyo
kupaa licha ya kuongezeka kwa ushindani.
Mfanyabiashara wa pikipiki eneo la Kariakoo, Mussa
Mtenguka anasema kuwa biashara kwa sasa imekuwa ya wastani kutokana na
kuongezeka kwa wauzaji japo ina faida kubwa kama awali.
“Hizi pikipiki za Kichina tunaziuza kati ya Sh
1.65 milioni hadi Sh1.7 milioni wakati hizi Boxer za India ni Sh2
milioni. Hata hivyo hizi bei ziliongezeka miaka miwili iliyopita
kutokana mahitaji kuongezeka, bei hazikuwa hivi,” anasema Mtenguka.
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni ya kutengeneza
pikipiki nchini Cruiser Motors Tanzania, ili kutimiza mahitaji yaliyopo
mijini na vijijini, wanatarajia kuanzisha uundaji wa vifaa hivyo vyenye
asili ya Tanzania ambavyo vitakuwa vikisambazwa ndani ya Kanda ya Afrika
Mashariki na Kati.
“Kwa sasa kampuni inazalisha pikipiki 10,000 kwa
mwaka na tunaratajia kuongeza uzalishaji huo hadi pikipiki 50, 000,”
ilieleza sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo yenye kiwanda chake Kiwalani,
jijini Dar es Salaam.
Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Prosper Ngowi
anasema kwa mtazamo wa haraka bodaboda zimesaidia kuongeza ajira,
kupunguza upotevu wa muda na vitendo vya wizi miongoni mwa vijana.
Hata hivyo, anasema serikali imechelewa kufanya
utafiti wa kina wa kubaini faida na hasara zinazoletwa na bodaboda kabla
ya kuendelea kuchochea sera za usafiri huo.
“Mapema tu baada ya usafiri huo kukua kwa kasi na
kuanza kuleta ajali nyingi, serikali ilibidi ikae chini na kufanya
utafiti, je gharama za kupoteza watu na kuwatibu majeruhi wa ajali za
bodaboda zinaendana na faida.
“Hii pia ingesaidia kufahamu kama asilimia kubwa
ya bodaboda zinamilikiwa na vijana wenyewe au mapebari wengine ili
kutambua ufanisi wa kuwasemehe kodi…serikali haina budi kufanya utafiti
huo sasa,” anasema Dk Ngowi.
Dk Ngowi anasema hata kama itabainika zimeleta
hasara, serikali haitakiwi kuzizuia na zaidi zifanyike juhudi za
kuwaelimisha zaidi madereva hao kufuata sheria na kuwa wastaraabu.
Iwapo utaboreshwa, alisema bodaboda ni usafiri
mzuri utakaokuza uchumi mara dufu kwa kuokoa muda na fedha zinazopotea
kutokana na foleni.
Pamoja na ukweli kwamba bodaboda zinaonekana
kurahisisha usafiri jijini hapa na maeneo mengine yasiyofikika na
usafiri wa umma nchini, bado bodaboda ni usafiri ghali kwa kilomita
kuliko daladala katika barabara zenye usafiri wa uhakika.
Utafiti mdogo uliofanywa na gazeti hili katika
mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam ni kwamba kama unatokea External
barabara ya Mandela kuelekea Ubungo unahitajika ulipe Sh1,500 hadi
Sh2,000 kwa bodaboda wakati kwa daladala ni Sh400 na ni ndani ya
kilomita moja na nusu.
Katika siku za hivi karibuni, madereva wengi wa
bodaboda wameonekana kuvaa miwani za jua na makoti. Ukweli ni kuwa
wanaathiriwa kwa kiasi kikubwa na upepo na vumbi.
Daktari wa Macho katika Hospitali ya
Mwananyamala, Agusta Sintale anasema, vumbi na upepo huharibu macho kwa
kiasi kikubwa na hasa iwapo dereva wa bodaboda ataendesha kwa miaka
miwili mfululizo.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka anasema hawezi kuzungumza kuhusu pikipiki katika kuzalisha ajira bali alidai kuwa suala hilo ni la kiuchumi zaidi.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka anasema hawezi kuzungumza kuhusu pikipiki katika kuzalisha ajira bali alidai kuwa suala hilo ni la kiuchumi zaidi.
Ripoti ya hivi karibuni iliyoandikwa na Benki ya
Dunia,(WB) iliweka bayana kuwa usafiri wa bodaboda unarahisisha biashara
na ni msaada mkubwa kwa wakazi wanaoishi katika miji yenye msongamano
katika nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Hata hivyo, Januari mwaka huu, aliyekuwa Waziri wa
Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, aliiagiza Sumatra kuandaa mikakati ya
kuanzishwa kwa benki ya bodaboda ili kuwasaidia wapate mikopo kuboresha
uchumi.
“Biashara ya bodaboda nchini imekuwa ikitoa
mchango mkubwa katika kurahihisha usafirishaji maeneo ya vijijini na
kwenye majiji yenye misongamano ya karibu kila kitu” anasema Dk
Mwakyembe.
Dk Mwakyembe anasema kutokana na ukweli huo,upo
umuhimu mkubwa kuanzisha benki itakayosaidia kutoa mikopo kwa madereva
wa boda boda,ili waweze kuboresha uchumi wao.
0 comments:
Post a Comment