EURA YASHUSHA BEI YA MAFUTA!!
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), jana imetangaza kushuka kwa bei za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kuanzia leo.
Mabadiliko hayo yametokana na kushuka kwa bei za mafuta katika soko la dunia.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Bw. Felix Ngamlagosi, alisema kwa Dar es Salaam petroli imeshuka kutoka sh. 1,955 hadi sh.1,768 ikiwa ni punguzo la sh. 187 kwa lita moja, dizeli kutoka sh. 1,846 hadi sh.1,708 sawa na punguzo la sh. 138 kwa lita moja.
Alisema mafuta ya taa nayo yameshuka kutoka sh. 1,833 hadi sh. 1,657 ikiwa ni punguzo la sh. 176 kwa lita na kusisitiza kuwa, kampuni za mafuta zipo huru kuuza bidhaa hizo kwa bei ya ushindani bila kuvuka bei kikomo.
Punguzo la mafuta hayo ni tofauti kwa kila mkoa ambapo vituo vyote vya mafuta vinatakiwa kuchapisha bei za mafuta katika mabango yanayoonekana yakionesha bei ya mafuta, vivutio vya biashara au promosheni zinazotolewa na kituo husika na wanunuzi kuhakikisha wanapewa stakabadhi.
"Bei ya mafuta ya ndani ingeweza kupungua zaidi kama thamani ya shilingi ya Tanzania isingeendelea kudhoofu, wastani wa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji (CIF), huchagia asilimia 60 ya bei ya mafuta katika soko la ndani.
"Kutokana na hali hiyo, kiwango cha ushukaji bei ya mafuta katika soko la ndani hakiwezi kuwa sambamba na asilimia ya ushukaji katika soko la dunia," alisema.
0 comments:
Post a Comment