JAJI Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman amefanya mabadiliko makubwa ya majaji katika kanda mbalimbali nchini, huku akiwahamisha wengine na kuwapandisha baadhi kuwa Majaji Wafawidhi.
Habari kutoka kwa vyanzo mbalimbali ndani ya
Mahakama Kuu, zinaeleza kwamba Majaji wote watatu waliokuwa wa Kanda ya
Moshi wamehamishwa huku aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Stella Mugasha
akihamishiwa Kanda ya Arusha kuendelea na wadhifa wake.
Majaji wengine waliokuwa chini yake, Crecensia
Makuru amehamishiwa Kanda ya Dodoma kuwa Jaji Mfawidhi na Jaji Moses
Mzuna naye amepandishwa cheo na kuhamishiwa Kanda ya Mtwara kushika
nafasi hiyo.
Habari za uhakika zimeeleza kuwa katika mabadiliko
hayo, Jaji Aisha Nyerere aliyekuwa Mfawidhi Kituo cha Arusha
amehamishiwa Moshi kuendelea na wadhifa huo.
Hata hivyo, bado majaji watakaosaidiana na Jaji Nyerere katika Kituo cha Moshi hawajatajwa.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji na kuhamishiwa jijini
Dar es Salaam, Nyerere aliwahi kuwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mkoa wa
Kilimanjaro.
Katika mabadiliko hayo, Jaji Shaban Lila aliyekuwa
Jaji Mfawidhi Mtwara sasa anahamia Dar es Salaam kuwa Jaji Mfawidhi wa
Kanda Maalumu ya Ilala ambayo inaanzishwa.
Wengine walioguswa na mabadiliko hayo ni Jaji
Maryam Shangali anayetoka Dodoma kwenda Iringa kuendelea na wadhifa wake
na Jaji Sekieti Kihiyo anatoka Iringa kwenda Kanda ya Dar es Salaam
kuwa Mfawidhi.
Pia Jaji Kakusulo Sambo aliyekuwa Kanda ya Arusha
chini ya Jaji Nyerere, amehamishiwa Sumbawanga kuwa Jaji Mfawidhi na
Jaji Mwanaisha Kwariko akihamishwa kutoka Dodoma kwenda Songea kuwa Jaji
Mfawidhi.
Haikuweza kufahamika mara moja sababu za kufanyika
kwa mabadiliko hayo, lakini wafuatiliaji wa medani ya sheria nchini
wanaamini uteuzi huo una lengo la kuongeza ufanisi katika idara hiyo
ambayo katika siku za karibuni ilitajwa na Taasisi ya Utafiti ya
Synovate kuwa miongoni mwa asasi zinazolalamikiwa kwa rushwa.
Polisi ndiyo walikuwa vinara kwenye utafiti huo baada ya
asilimia 33 ya walioulizwa kuwataja. Idara za Mahakama na Afya zilipata
asilimia 16.
Msajili wa Mahakama Kuu nchini, Ignass Kitusi
hakupatikana kwa siku mbili mfululizo tangu juzi na jana kuthibitisha
mabadiliko hayo, lakini baadhi ya Wasajili wa Wilaya wa Mahakama Kuu
wamethibitisha.
Msajili wa Mahakama ya Rufaa Tanzania, Pantrine
Kente alipoulizwa kuhusu suala hilo, alishauri atafutwe Katibu wa
Mahakama, Hussein Katanga akisema ndiye katibu wa mhimili huo kama
alivyo Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefu Sefue na Katibu wa
Bunge, Dk Tommy Kashililah.
Hatahivyo alipotafutwa Katanga, alitaka aulizwe maswali kwa
kutumiwa ujumbe mfupi wa simu na alipotumiwa, aliahidi kutoa majibu
ambayo hadi tunakwenda mtamboni alikuwa hajayatoa.
“Ni kweli kuna mabadiliko na wala si ya siri kwa
sababu tayari ni rasmi. Ni uhamisho uliogusa majaji wafawidhi tu kwa
hiyo tunasubiri duru ya pili ya wale watakaosaidiana nao,” alidokeza
msajili mmoja.
Habari zilizowakariri baadhi ya wasajili wa Wilaya
wa Mahakama Kuu ambazo zimeguswa na mabadiliko hayo, zinasema majaji
waliohamishwa wametakiwa kumalizia viporo vya kazi zao na kuripoti vituo
vipya vya kazi Mei mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment