KATIBU Mkuu
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa,
pamoja na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho wanatarajia kufanya
mkutano mkubwa wa hadhara Gongo la Mboto, Dar es Salaam kesho Jumamosi.
Akizungumza
na Tanzania Daima ofisini kwake Dar es Salaam jana, Katibu wa CHADEMA
Jimbo la Ukonga, Jumaa Mwipopo, alisema mkutano huo utakaofanyika katika
viwanja vya Kampala utaanza saa tisa alasiri, na kuwataka wananchi wote
bila kujali itikadi za vyama vyao kuhudhuria kwa wingi, wakiwamo
viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.
Mwipopo alisema lengo la ujio wa kiongozi huyo wa kitaifa wa chama hicho ni kuhutubia mkutano huo kuhusu mabaraza ya Katiba.
Viongozi
wengine wanaotarajiwa kufuatana na Dk. Slaa ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo
na Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa chama hicho, John Mnyika, Mbunge
wa Jimbo la Kawe, Halima Mdee, Mjumbe wa Kamati Kuu na Mwanasheria wa
chama hicho, Mabere Marando na wengine wengi.
Vilevile
Mwipopo alisema katika mkutano huo uongozi wa CHADEMA Jimbo la Ukonga
utagawa rasimu za Katiba bure kwa wananchi wote watakaohudhuria na
vijitabu vinavyohusu mapendekezo ya Katiba mpya ya CHADEMA.
Akizungumzia
kuhusu mkutano mkuu wa jimbo uliofanyika Agosti 18, 2013 ambao ulihusu
mapendekezo ya CHADEMA kuhusu Katiba waitakayo Watanzania, alisema
ulikuwa wenye mafanikio, kwa sababu watu mbalimbali bila kujali itikadi
za vyama vyao maoni yao yalisikilizwa na kuzingatiwa.
Mwipopo
alisema katika mkutano huo aliwahimiza Watanzania kuchangia maoni yao
kwa kina kuhusu Katiba mpya, akibainisha kuwa umaskini tulionao
umetokana na ubovu wa Katiba.
Alishutumu
sera mbovu zilizopo za ‘kuwabeba’ wageni (wawekezaji), kwa serikali
kuwamilikisha ardhi na kuwaacha wananchi wanyonge wakiteseka bila kuwa
na sauti kuhusu ardhi yao inayochukuliwa.
“Mwekezaji
anapokuja kutoka nje na anataka kuwekeza katika ardhi, aje moja kwa moja
kwa mwananchi mwenye ardhi hiyo na aingie naye mkataba mwananchi
mwenyewe. Huu ndio moja ya mipango ya CHADEMA ili kumpa mwananchi uwezo
wa kumiliki rasilimali ya nchi yake. Lakini tutafanya hivyo kwa kufuta
kipengele cha kusema ardhi ni mali ya serikali,” alisisitiza Mwipopo.
0 comments:
Post a Comment