Walazimishwa kulipa nauli mara mbili
Mamia
ya abiria wamekwama kusafiri kwa siku mbili katika Kituo Kikuu cha
Mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo (UBT), jijini Dar es Salaam
Waandishi wa NIPASHE Jumapili, waliofika
kituoni hapo majira ya saa 2:00 asubuhi jana walikuta abiria wengi
wakiwa wamekaa na mizigo yao na wengine wamesimama wakiwa wamekata tamaa
baada ya kukosa usafiri wa kwenda mikoani na nje ya nchi.
Baadhi ya wasafiri walioongea na waandishi
wa gazeti hili walisema, kwa siku mbili mfululizo hali ya huduma ya
usafiri imekuwa mbaya na hakuna maelezo yoyote yanayotolewa.
Mabasi ambayo yanadaiwa kusitisha huduma zake ni yanayokwenda Dodoma, Tanga, Morogoro na nchi za jirani.
Walisema kinachofanyika kwa sasa, baadhi
ya kampuni zinazoingiza magari machache kituoni hapo na kutoa huduma kwa
masharti ya kulipa nauli mara mbili ya ile iliyoruhusiwa na serikali.
Mmoja wa abiria aliyejitambulisha kwa jina la Pendo Makula, mkazi wa
Dodoma, alisema alifika kituoni hapo jana alfajiri lakini mpaka muda huo
alikuwa hajui hatma yake kutokana na kukosa usafiri.
Alisema, kulikuwa na taarifa zisizo rasmi
kuwa magari mengi yamekodiwa na shule za sekondari na vyuo kwa ajili ya
kusafirisha wanafunzi. Hata hivyo sababu hiyo haitoshi kuamini kwa
sababu hiyo ni mara yao ya kwanza kushuhudia hali hiyo.
"Kama kweli magari yamekodiwa na
wanafunzi, kwa nini wasiache mengine kutoa huduma kwa wananchi au kutoa
matangazo ya tahadhari ili watu wasisumbuke?" alihoji Makula.
Abiria mwingine, Halima Jumatatu (18)
ambaye ni mwanafunzi alisema alifika kituoni asubuhi na kukata tiketi
kwa Sh.15,000 kwenda Tanga, badala ya nauli halali ya Sh. 13,000.
Hata hivyo, mpaka saa 4:00 asubuhi nauli
ya kwenda Tanga iliongezeka na kufikia Sh.30,000, huku watu wanaokwenda
Morogoro walikatiwa tiketi kwa Sh. 15,000 badala ya Sh. 7,000 na Dodoma
ilikuwa Sh.30,000 badala ya Sh.16,000 hadi 18,000.
"Pamoja na kununua tiketi kwa bei ya juu,
lakini basi tuliloambiwa tusafirie hatulioni, kila mtu anamuomba Mungu
pengine tutapata usafiri leo," alisema Halima.
Raia mmoja wa China Tea Yu, alisema kwa
siku mbili mfululizo alikuwa akikata tiketi ya kwenda Dodoma kwa
matumaini ya kupata usafiri, lakini mpaka jana alikuwa kituoni hapo
akisubiri bila mafanikio.
"Inatakiwa watu wafahamu muda ni mali,
lazima tujali na kuthamini watu wanaopewa huduma, tumebaki hapa hatujui
tufanye nini," aliongeza kusema Yu.
Kiongozi mmoja wa chama cha madereva
ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema tatizo kubwa ni
upandaji wa nauli wa ghafla uliofanywa na wamiliki wa magari na
kusababisha watu kushindwa kumudu viwango hivyo vya nauli.
Alisema kwa wale wenye uwezo wamelipa na wameondoka kwenye magari machache yaliyoonekana kituoni hapo.
"Kutokana na vyuo na shule kufunguliwa
kuna wimbi kubwa la watu kusafiri, mabasi mengi yamepandisha nauli na
unaowaona hapa ni watu masikini walioshindwa kulipa nauli inayotakiwa,"
alisema kiongozi huyo.
Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa
Mabasi nchini, (TABOA) Enea Mrutu, kwa kutumia ujumbe mfupi wa maneno
(sms) kupitia simu ya kiganjani, alisema kutokana na shule na vyuo
kufunguliwa jana na leo kutakuwa na shida ya usafiri. "Likizo zimekwisha
shule zinafunguliwa, abiria ni wengi kwa leo na kesho na maonyesho ya
biashara ya sabasaba ndio sababu ya abiria kukwama," ilisema ujumbe huo.
Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Udhibiti wa
Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), David Mziray, alieleza kwamba
hana taarifa ya kuwapo kwa tatizo hilo na kama litakuwapo basi litakuwa
na mahusiano na ufunguaji muhula wa masomo katika shule mbalimbali
nchini.
Hata hivyo, aliahidi kulifuatilia suala
hilo, na kuwataka abiria waliokatiwa tiketi na kukosa usafiri kwenda
kituo cha polisi kilichopo kituoni hapo kutoa taarifa.
0 comments:
Post a Comment