NAIBU Katibu
Mkuu (Tanzania Bara) wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mwigulu Mchemba,
ameambulia patupu baada ya mikakati yake ya kutaka kukwamisha mkutano wa
Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibrod Slaa, kushindikana.
Tukio hilo
lilitokea juzi jimboni Iramba Magharibi ambalo analiongoza Mwigulu,
ambapo Dk. Slaa alifanikiwa kuwahutubia mamia ya wananchi katika
mchakato wa chama hicho kukusanya maoni ya wafuasi wao juu ya rasimu ya
kwanza ya Katiba mpya.
Kwa mujibu
wa vyanzo vyetu vya habari, Mwigulu alijaribu kufanya kila mbinu ili
mkutano wa Dk. Slaa ukose watu wa kumsikiliza lakini ilishindikana.
Tofauti na
mikutano mingine ya CHADEMA ambayo ameihutubia Dk. Slaa katika mchakato
huo, juzi hali ya ulinzi ilikuwa tofauti kidogo kutokana na polisi wengi
kutanda eneo la mkutano la uwanja wa soko la zamani la Kiomboi wilayani
Ilamba wakiwa na silaha za moto.
Askari hao ambao walikuwa wamezunguka eneo alilokuwa akihutubia Dk. Slaa, walivalia
kofia ngumu kama vile wanakwenda katika mapambano, jambo ambalo wananchi walidai kuwa ulikuwa ni mkakati wa kuwatisha wasijitokeze kumsikiliza kiongozi huyo.
kofia ngumu kama vile wanakwenda katika mapambano, jambo ambalo wananchi walidai kuwa ulikuwa ni mkakati wa kuwatisha wasijitokeze kumsikiliza kiongozi huyo.
Pamoja na
jitihada hizo, wananchi walijitokeza kwa wingi kumsikiliza Dk. Slaa na
kisha kutoa maoni yao kwa njia ya kujaza fomu na wengine kwa kuzungumza
mkutanoni.
“Kusema
ukweli usione tumejitokeza hapa ni kutokana na ujasiri wetu vinginevyo
hali hii kwa wananchi wa kawaida lazima waogope maana askari hawa
wanaonekana kama vile wamekuja kupambana,” alisema mmoja wa wakazi wa
Kiomboi ambaye hakutaka jina lake litajwe.
Katika
kuhakikisha wananchi hawahudhurii mkutano huo, siku moja kabla
yalitolewa matangazo ya kuwaalika watu kwenye mashindano ya mpira wa
miguu kati ya timu ya Kiomboi na Simba ya Dar es Salaam ambayo ililetwa
na mbunge huyo, wakielezwa kuwa kiingilio ni bure.
Chanzo chetu
kiliongeza kuwa baada ya viongozi wa CHADEMA kunasa mbinu hiyo,
walijitahidi kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kuhudhuria mkutano huo wa
juzi, wakisema haukuwa wa siasa walizozizoea bali ni kuwataka watoe
maoni yao juu ya rasimu ya Katiba mpya.
Akiwahutumia
wananchi hao, Dk. Slaa alisema kuwa kuna vipengele vingi ambavyo
wanaviunga mkono katika rasimu hiyo ingawa kuna baadhi vinahitaji
marekebisho.
Alifafanua
kuwa vipengele vingi ni vizuri japo CCM wanavipinga, huku akidai kwamba
kitendo cha chama hicho tawala kupinga kipengele cha uwazi katika tunu
za taifa pamoja na rushwa ni hatari katika taifa.
“Tunamuunga
mkono Jaji Joseph Warioba katika vipengele vingi hasa katika kipengele
cha kulinda rasilimali za taifa, uwazi katika mikataba lakini wenzetu wa
CCM wamepinga kwamba uwazi usiwemo katika Katiba mpya sijui malengo yao
nini. Kwa hiyo wananchi mnatakiwa kuamua wenyewe maana chama chenu
hakitaki mambo mazuri yawekwe katika Katiba yenu,” alisema.
Naye mjumbe
wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Mabere Marando, alitoa ufafanuzi kuhusu
mapendekezo ya serikali tatu ambazo alieleza kuwa CCM inapinga
mapendekezo hayo.
Marando
alisema kuwa kitendo cha baadhi ya wanasiasa wa CCM kuwapotosha wananchi
kwamba serikali tatu ni mzigo kwa taifa si cha kweli na kwamba serikali
ya sasa ndiyo mzigo kwa taifa.
“Kwa
kuzingatia mapendekezo kuhusu Bunge la Jamhuri ya Muungano katika aya ya
105, kwa idadi ya sasa na mikoa ya Tanzania Bara na Zanzibar, Bunge la
Jamhuri ya Muungano litakuwa na wabunge 75 tu.
“Kwa
mapendekezo ya muundo wa serikali tatu, Bunge la Zanzibar litakuwa na
wabunge 50 wa kuchaguliwa wakati Bunge la Tanganyika litakuwa na wabunge
189 wa majimbo ya uchaguzi,” alisema.
Marando
aliongeza kuwa muundo wa muungano wa serikali tatu utakuwa na wabunge
314 tu; kwamba upo uwezekano wa idadi hiyo kupungua zaidi wakati wa
mchakato wa kuandika Katiba ya Tanganyika na marekebisho ya Katiba ya
Zanzibar.
Kuhusu Bunge
la sasa ambalo linasemekana kuwa na unafuu, Marando alisema lina
wabunge 357 ambapo 189 wanatokana na majimbo ya Tanzania Bara, majimbo
50 ya Zanzibar, Viti maalumu 105, kuteuliwa na rais 10, wanawakilisha
watano wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa
serikali.
Aliongeza
kuwa kwa mabunge mawili ya sasa yana idadi ya wabunge 438 na kwamba
idadi hiyo ni kubwa kuliko idadi ya wabunge wa mabunge matatu
yatakayokuwepo chini ya muundo wa serikali tatu.
Hata hivyo,
baadhi ya wananchi waliopata fursa ya kuchangia walionekana kuchukizwa
na madaraka makubwa ya Rais huku wakipendekeza kipengele cha kupunguza
madaraka ya Rais kiingizwe kwenye Katiba.
Wananchi
wengine walipendekeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi iwe huru ili Rais
asiweke mkono wake badala yake kiundwe chombo huru cha kuwachagua
viongozi wa tume hiyo.
‘CCM imevunja Muungano’
Kutoka
mkoani Kagera, mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, amesema kuwa
CCM tayari imeuvunja Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kutokana na
muundo wa Katiba mbili za Muungano na ile ya Zanzibar.
Akiwahutubia
wanachi waliohudhuria mikutano ya mabaraza ya wazi ya CHADEMA ya
kujadili rasimu ya Katiba mpya mjini Bukoba, Lissu alisema kuwa Katiba
hizo mbili zinaonyesha mkanganyiko wa wazi unaovunja Muungano.
Alisema kuwa
Katiba ya Jamhuri ya Muungano inatamka wazi katika ibara yake ya kwanza
kwamba Tanzania ni nchi moja ya Jamhuri ya Muungano, wakati ile ya
Zanzibar nayo inatamka kuwa Zanzibar ni nchi, hivyo kuzifanya ziwe nchi
mbili zenye madaraka kamili.
“Tanzania si
nchi moja kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar, kwa sababu Muungano
ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Aman Karume,
tayari umekufa na CCM ndiyo imeuua,” alisema.
Lissu
alifafanua kuwa Zanzibar tayari ina alama zake ikiwemo wimbo wa taifa,
rais wake ambaye ni mkuu wa vikosi vya idara maalumu, mahakama yake na
bendera yake.
“Kuna haja
sasa kufufuka Tanganyika kama Tume ya Jaji Warioba ilivyopendekeza kuwa
na serikali tatu. Leo Jamhuri ya Watu wa Zanzibar imefufuliwa, kwa maana
hiyo hakuna budi pia kufufuliwa kwa Jamhuri ya Tanganyika kutoka katika
‘wafu’,” alisema.
0 comments:
Post a Comment