(Kanuni ya
86(6) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, 2013)
UTANGULIZI
Mheshimiwa
Spika,
Huu
ni Muswada wa marekebisho ya pili ya Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya Sheria za Tanzania. Kama Bunge lako
tukufu litakavyokumbuka, Sheria hii ilifanyiwa marekebisho ya kwanza kwa
kupitishwa kwa Sheria ya Marekebisho ya
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Na. 2 ya mwaka 2012, mwezi Februari ya
mwaka jana. Mabadiliko hayo ya kwanza yalihusu Sehemu ya Tatu na ya Nne ya
Sheria hii, na yalilenga vifungu mbali mbali vinavyohusu Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na utekelezaji wa majukumu yake.
Muswada
huu wa sasa unalenga kufanya marekebisho katika Sehemu ya Tano ya Sheria
inayohusu ‘Kuitisha Bunge Maalum.’ Sambamba na mapendekezo haya, kuna
mapendekezo ya kufanya marekebisho katika Sehemu ya Sita kwa kufuta vifungu vya
32 hadi 36 vya Sheria vinavyohusu utaratibu wa kura ya maoni kwa ajili ya
kuhalalisha ‘Katiba Inayopendekezwa.’ Marekebisho haya yamewekwa katika aya ya
57 ya Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni,
2013. Mapendekezo ya Muswada huu ni muhimu lakini yana utata mkubwa.
Mheshimiwa
Spika,
Katika
kutekeleza majukumu yake ya kuuchambua Muswada huu, Kamati ya Bunge lako tukufu
ya Katiba, Sheria na Utawala ilikutana na wadau wengi mbali mbali. Hivyo, kwa
mfano, Kamati ilipata maoni ya taasisi za kidini na za kiraia; taasisi za elimu
ya juu na za kitaaluma; vyama vya siasa na asasi nyingine. Kwa sababu ambazo
Kamati haikuelezwa vizuri na uongozi wa Bunge hili tukufu, mapendekezo ya
Kamati kwenda Zanzibar kwa lengo la kukusanya maoni ya wadau wa Zanzibar juu ya
Muswada huu muhimu kwa mustakbala wa Jamhuri ya Muungano yalikataliwa.
Kwa
maana hiyo, ni muhimu Bunge lako tukufu lifahamu ukweli huu kwamba wadau pekee
walioshirikishwa kutoa maoni yao juu ya Muswada ni Watanzania Bara tu.
Wazanzibari hawakupatiwa fursa hiyo na hawakushirikishwa kabisa, licha ya
Sheria yenyewe kuwa na mambo mengi yanayoihusu Zanzibar. Kwa vile wadau wa
Zanzibar walishirikishwa kikamilifu kutoa maoni yao kuhusu Muswada uliopelekea
Sheria hii kutungwa mwaka 2011, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua
ni kwa nini uongozi wa Bunge na wa Serikali umeona si busara na sahihi
kuwapatia Wazanzibari fursa ya kutoa maoni yao kuhusu Muswada huu wa
kurekebisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo inawahusu pia Wazanzibari na
nchi yao.
URAIS
WA KIFALME KWA MARA NYINGINE TENA!!!!
Mheshimiwa
Spika,
Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni imepigia kelele jitihada za serikali hii ya CCM
kudhibiti mchakato wa Katiba Mpya kwa kuendeleza kile tulichokiita miaka miwili
iliyopita, “... kivuli kirefu cha Urais
wa Kifalme katika mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.”[i]
Hapo tulikuwa tunazungumzia mamlaka ya Rais ya uteuzi wa Wajumbe na watendaji
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, na tulisema kwamba mamlaka hayo yalikuwa na
lengo moja tu: “kuhakikisha kwamba
matokeo ya kazi ya Tume hiyo ni yale tu yanayotakiwa na Rais na Serikali yake
na chama chake cha CCM.”
Mheshimiwa
Spika,
Katika
Maoni yetu wakati wa kutungwa kwa Sheria hii mwezi Novemba mwaka 2011, Kambi
Rasmi ya Upinzani ilipinga vikali mapendekezo ya kumwezesha Rais kuteua Wajumbe
wa Bunge Maalum wasiotokana na Bunge lako tukufu na Baraza la Wawakilishi
Zanzibar. Tulisema yafuatayo kuhusiana na jambo hili: “... wajumbe ... wanaopendekezwa kuteuliwa kwenye Bunge la Katiba kwa
mujibu wa ibara ya 20(2)(e) na (4) ya Muswada Mpya sio, na hawawezi kuwa,
wawakilishi wa wananchi. Kwanza, hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala taasisi
zao kuwawakilisha katika Bunge la Katiba kwa sababu Muswada Mpya unapendekeza
wateuliwe na Rais.”
Kwa
sababu ya upinzani huo, mapendekezo ya kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa
Bunge Maalum wasiokuwa wabunge na Wawakilishi yaliondolewa katika Muswada huo
wa Sheria hii. Badala yake, kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria iliyotungwa na
Bunge lako tukufu kiliweka wazi kwamba “wajumbe mia moja sitini na sita [watateuliwa]
kutoka ...” taasisi zilizotajwa katika kifungu hicho.
Mheshimiwa
Spika,
Ni
kweli kwamba kifungu cha 22(1)(c) kama kilivyotungwa kilileta giza badala ya
mwanga katika suala la uteuzi wa wajumbe hao. Kama tulivyoieleza timu ya
wataalamu wa Serikali kufuatia mkutano wetu na Rais Jakaya Kikwete uliofanyika
Ikulu tarehe 26 Novemba, 2011: “Toleo la
Kiswahili la Sheria linasema kwamba wawakilishi wa makundi mengine
‘watakaoteuliwa kutoka’ kwenye makundi yaliyoorodheshwa. Toleo la Kiingereza
linasema wajumbe hao watakuwa ‘drawn from’ (kwa tafsiri ya Kiswahili
‘watachukuliwa kutoka’). Maana za maneno haya hazifanani na wala hayako wazi
kuhusu nani ‘atakayewateua’ au ‘kuwachukua’ wajumbe hao kutoka kwenye taasisi
zao.”[ii]
Kwingineko
katika mkutano wetu na Rais Kikwete tulimweleza kwamba: “Wajumbe 166 wengine wanaowakilisha taasisi nje ya Wabunge na
Wawakilishi hawajachaguliwa na mtu yeyote na wala na taasisi zao kwani Sheria
haisemi ni nani atakayewateua na/au kuwachagua.” Kwa sababu hiyo,
tulipendekeza kwamba “Sheria iweke wazi
kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata
juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi.”[iii]
Bonyeza Read More Kuendelea
Mheshimiwa
Spika,
Mapendekezo
ya marekebisho yaliyoko kwenye Muswada huu yanaonyesha wazi kwamba ushauri wetu
kwa Rais Kikwete na kwa timu yake ya watalaamu umepuuzwa. Badala yake, serikali
hii sikivu ya CCM imeamua kuturudisha nyuma kwa zaidi ya miaka miwili kwa
kuibua tena pendekezo la kumfanya Rais kuwa mteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum
wasiotokana na Wabunge au Wawakilishi wa Zanzibar. Hii ni kwa sababu aya ya 3
ya Muswada inapendekeza kwamba wajumbe hao sasa wateuliwe Rais. Hiyo ni sawa na
kusema kwamba kilichokuwa hakifai miaka miwili iliyopita sasa kinafaa; na
kilichokataliwa wakati ule sasa kinakubalika!
Ili
kuficha ukweli kwamba mwenye mamlaka ya uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum
wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi ni Rais, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Muswada
unapendekeza kuongezwa kwa vifungu vidogo vipya viwili katika kifungu cha 22.
Kwanza, inapendekezwa kuwe na kifungu kidogo cha (2A) ambacho kitamruhusu Rais
kualika kila kundi lilioainishwa katika kifungu kidogo cha 1(c) “kuwasilisha kwake orodha ya majina ya watu
wasiozidi watatu ili kuteuliwa kuwa wajumbe.” Pili, inapendekezwa kuwe na kifungu
kidogo cha (2B) kitakachomlazimu Rais kuzingatia sifa na uzoefu wa watu
waliopendekezwa, na usawa wa jinsia wakati wa kufanya uteuzi wa wajumbe hao.
Mheshimiwa
Spika,
Mapendekezo
ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge Maalum hayakubaliki na Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliomba Bunge lako tukufu lisiyapitishe kuwa
Sheria. Kwanza, mapendekezo haya yanarudisha dhana kwamba wajumbe hawa watakuwa
watu wa Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Rais Kikwete na chama
anachokiongoza ni wadau wakubwa wa mchakato wa Katiba Mpya na wana maslahi
halisi na makubwa ya kuhakikisha kwamba matakwa ya chama chao ndio yanakuwa
Katiba Mpya ya nchi yetu.
Ushahidi
wa maslahi haya ya CCM ni kile kinachoitwa Ufafanuzi
Kuhusu Rasimu ya Kwanza ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa
Wanachama na Viongozi wa CCM uliotolewa na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya
Taifa ya CCM tarehe 10 Juni, 2013. Katika Ufafanuzi huo, CCM imekataa
mapendekezo yote muhimu yaliyoko kwenye Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume. Needless to say, Rais Kikwete ni
Mwenyekiti wa vikao vyote vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM.
Kumpa Rais, na Mwenyekiti wa CCM Taifa, mamlaka ya kuteua wajumbe wa Bunge
Maalum litakaloijadili – na kuikubali au kuikataa – Rasimu ya Katiba ambayo
chama chake kimekwishaikataa ni sawa na kuipa CCM fursa nyingine ya kujaza
Bunge hilo na makada wake kwa lengo la kutekeleza matakwa ya chama hicho.
Pili,
hata bila wajumbe hawa kuteuliwa kwa namna inayopendekezwa, tayari CCM peke yake
ina zaidi ya 72% ya wajumbe wote wa Bunge Maalum wanaotokana na Wabunge na
Wawakilishi. Kumpa Mwenyekiti wa CCM mamlaka ya kuteua wajumbe wengine zaidi,
kama inavyopendekezwa katika Muswada huu, ni kutoa mwanya kwa CCM kutumia
kivuli cha makundi ya kiraia, taasisi za kidini na makundi mengine ili kujiongezea
wajumbe wengine zaidi, na hivyo kuhakikisha kwamba Bunge Maalum litatekekeleza
matakwa ya kuendeleza status quo.
Kwa
maneno mengine, Serikali hii ya CCM na Wabunge wake inataka Mwenyekiti wao wa
Taifa ayachagulie makanisa na awachagulie Wakristo wawakilishi wao katika Bunge
Maalum; awachagulie Waislamu wa BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA na taasisi nyingine
za Kiislamu wawakilishi wao katika Bunge hilo; avichagulie vyama vya siasa vinavyoipinga
CCM wawakilishi wao; awachagulie wafanyakazi, wakulima, wafugaji, wahadhiri,
wanafunzi, wafanyabiashara, walemavu na makundi mengine ya kijamii wawakilishi
wao katika Bunge Maalum! Kama ni hivyo, hilo halitakuwa Bunge Maalum la
Watanzania, bali litakuwa Bunge Maalum la CCM na Mwenyekiti wao. Hili
halikubaliki kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na, tunaamini, halitakubalika
kwa wananchi wa Tanzania katika ujumla wao.
Tatu,
kwa jinsi yalivyo kwa sasa, mapendekezo haya hayawezi kutekeleza matakwa ya
kifungu cha 22(1)(c) cha Sheria kinachotaka wajumbe wa Bunge Maalum wasiotokana
na wabunge au wawakilishi kuwa mia moja sitini na sita. Hii ni kwa sababu, hata
kama watu wote waliopendekezwa na makundi yaliyoainishwa na kifungu hicho
watateuliwa kuwa wajumbe, bado idadi yao itakuwa wajumbe ishirini na saba kwa
kuwa makundi yenyewe yako tisa tu! Muswada uko kimya juu ya wajumbe wengine mia
moja thelathini na tisa watatoka wapi na watateuliwa na nani na kwa utaratibu
upi.
Kuna
hoja kwamba utaratibu wa uteuzi wa wajumbe unaopendekezwa na Muswada unafanana
na uteuzi wa wajumbe wa Tume ulioko kwenye kifungu cha 6(6) cha Sheria ambapo
Rais alialika vyama vya siasa, jumuiya za kidini, asasi za kiraia, n.k.,
kuwasilisha orodha ya majina ya watu ili kuteuliwa kuwa wajumbe wa Tume. Hoja
hii sio sahihi. Kwanza, Tume ya Katiba sio sawa na Bunge Maalum. Tume ni chombo
cha kitaalamu chenye majukumu ya kitaalamu ya kukusanya maoni ya wananchi,
kuandaa ripoti pamoja na Rasimu ya Katiba. Uhalali wa Tume unatokana na
utaalamu wa wajumbe wake na weledi katika kutekeleza majukumu yao ya kitaalamu.
Kwa
upande mwingine, Bunge Maalum ni chombo cha uwakilishi ambacho wajumbe wake
wana majukumu ya kisiasa ya kuwakilisha wananchi wa makundi mbali mbali kwenye
kazi ya kisiasa ya kuandika Katiba Mpya. Uhalali wa Bunge Maalum unatokana na
upana na ubora wa uwakilishi wake wa makundi mbali mbali ya kisiasa na kijamii.
Chombo cha uwakilishi cha aina hii lazima kitokane na wananchi na/au makundi ya
kijamii kinachoyawakilisha ili kiwe na uhalali wa kisiasa. Dhana ya Rais – na Mwenyekiti
wa CCM – kuteua Wajumbe wa Bunge Maalum inavuruga au kuondoa kabisa dhana ya
uwakilishi wa wananchi na uhalali wa kisiasa katika mchakato wa Katiba Mpya.
Pili,
kumpa Rais mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa Wabunge au Wawakilishi wa
Zanzibar kunaleta dhana ya ubaguzi. Hii ni kwa sababu, Rais hana mamlaka ya
kuteua wajumbe wa Bunge Maalum watakaotoka kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano
na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Hawa wataingia katika Bunge Maalum kwa
mujibu wa nafasi zao Bungeni au katika Baraza na sio kwa fadhila ya Rais. Swali
la kujiuliza hapa ni kwa nini Rais awe na mamlaka ya kuteua wajumbe wasiokuwa
Wabunge au Wawakilishi wakati hana mamlaka hayo kuhusu Wabunge na Wawakilishi? Needless to say, ubaguzi huu unaenda
kinyume na matakwa ya ibara ya 13(2) ya Katiba ya sasa na, kwa hiyo,
haukubaliki.
Tatu,
uteuzi wa wajumbe wa Tume uliofanywa na Rais na ambao unatumiwa kama mfano
wenyewe ulikuwa na walakini kubwa. Katika hili, kuna ushahidi wa wawakilishi wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Kikristo Tanzania (CCT)
na asasi mbali mbali za kiraia zikiwemo za walemavu waliowasilisha maoni ya
taasisi zao kwa Kamati juu ya Muswada huu. Wawakilishi hao waliiambia Kamati
kwamba ijapokuwa waliandikiwa na Rais kuwasilisha majina ya wajumbe wao kwa
ajili ya kuteuliwa kwenye Tume, na walifanya hivyo, hakuna hata moja ya majina
waliyopendekeza aliyeteuliwa na Rais kuwa wajumbe wa Tume.
Badala
yake, Rais aliteua watu aliowaona yeye na washauri wake wanafaa. Kama taarifa
za wadau hawa ni za kweli maana yake ni kwamba Rais na Mwenyekiti huyu wa CCM
Taifa hawezi kuaminika tena kuteua wajumbe halisi wa taasisi hizi katika Bunge
Maalum ambalo ndilo litakalojadili na kuipitisha – au kuikataa - Rasimu ya
Katiba Mpya ambayo tayari CCM na wapambe wao wametamka wazi kwamba wanaikataa!
WAJUMBE
WA BUNGE MAALUM WAONGEZWE
Mheshimiwa
Spika,
Ili
kutatua mkanganyiko huu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza Bunge
lako tukufu lirejee na kukubali mapendekezo yetu kwa Timu ya Wataalamu wa
Serikali ya Januari mwaka jana:
Ø “Sheria iweke wazi
kwamba wajumbe hawa ‘watateuliwa na’ taasisi zilizotajwa. Hii itaondoa utata
juu ya uwakilishi wao na juu ya mamlaka yao ya uteuzi;
Ø “Sheria itaje
kwamba idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum watakaotokana na kila taasisi
iliyoorodheshwa katika kifungu cha 22(1)(c) itakuwa 354 kama walivyoorodheshwa
hapa chini:
(a)
“Asasi
zisizokuwa za kiserikali zilizotajwa katika aya (i) zifafanuliwe kuwa ni
makundi yanayounganisha asasi hizo, yaani, ANGOZA, TANGO, TACOSODE na Jukwaa la
Katiba na kila moja ya makundi hayo itakuwa na wajumbe watano kwa jumla ya
wajumbe 20;
(b)
“Asasi
za kidini zilizotajwa katika aya (ii) zifafanuliwe kuwa ni makundi
yanayounganisha asasi hizo, yaani, BAKWATA, Baraza Kuu, JUMAZA, TEC, CCT na PCT
na kila moja ya makundi hayo itakuwa na wajumbe watano kwa jumla ya wajumbe 30.
Aidha, Waadventista wa Sabato (SDA), Hindu, Shia Ithnaasheri na Sikh watakuwa
na mjumbe mmoja mmoja, kwa jumla ya wawakilishi 35 wa taasisi za kidini;
(c)
“Vyama
vya siasa vyenye usajili wa kudumu vilivyotajwa katika aya (iii) vitakuwa na
wajumbe 72 watakaogawanywa katika makundi mawili: 1) vyama vyote vya siasa vyenye
usajili wa kudumu vitakuwa na wajumbe 42 ikiwa ni wajumbe wawili kwa kila
chama; 2) vyama vya siasa vyenye uwakilishi Bungeni vitakuwa na wajumbe 30
ikiwa ni CCM 18, CHADEMA 7, CUF 3 na NCCR-Mageuzi, TLP na UDP 3 kwa ujumla wao.
Hii ni kufuatana na uwiano wa kura zote za Wabunge ambazo vyama hivyo
vilizipata kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2010;
(d)
“Taasisi
za elimu ya juu zilizotajwa katika aya (iv) zifafanuliwe kuwa ni vyuo vikuu 28
vinavyotambuliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na vyuo vya elimu ya juu
16 vinavyotambuliwa na Baraza la Elimu ya Ufundi la Taifa (NACTE). Taasisi hizi
zitakuwa na mjumbe mmoja kwa kila moja kwa jumla ya wajumbe 44;
(e)
“Taasisi
za elimu ya juu zinahusisha pia vyama vya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambavyo
vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa chama cha wanafunzi kwa jumla ya wajumbe 44;
(f) Taasisi za elimu ya
juu zinahusisha pia vyama wahadhiri/wakufunzi wa vyuo vya elimu ya juu ambavyo
vitakuwa na mjumbe mmoja mmoja kwa kila chama kwa jumla ya wajumbe 44;
(g)
“Makundi
yenye mahitaji maalum yaliyotajwa katika aya (v) yafafanuliwe kuwa ni mashirika
yanayowakilisha wenye ulemavu wa macho, ngozi, viziwi/bubu, viwete na walemavu
wa aina nyingine ambayo yatakuwa na wajumbe 10 kwa ujumla wao;
(h)
“Vyama
vya wafanyakazi vilivyotajwa katika aya (vi) vifafanuliwe kuwa ni vile
vilivyosajiliwa na vitakuwa na wajumbe 40 ikiwa ni wajumbe wawili kutoka kila
chama cha wafanyakazi kilichosajiliwa;
(i) “Jumuiya ya
wakulima iliyotajwa katika aya (vii) itakuwa na wajumbe 10 watakaotokana na
vyama vya wakulima wa mazao kama vile pamba, kahawa, korosho, chai, katani,
karafuu, miwa na wavuvi;
(j) “Jumuiya ya
wafugaji iliyotajwa katika aya (viii) itakuwa na wajumbe 10 watakaotoka Baraza
la Mashirika yasiyo ya Kiserikali ya Wafugaji na Wawindaji/wakusanya matunda ya
porini (PINGOS Forum);
(k)“Vikundi
vingine vya watu wenye malengo yanayofanana vilivyotajwa katika aya (ix)
vifafanuliwe kumaanisha Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha Wenye
Viwanda Tanzania (CTI), Chama cha Wafanyabiashara, Viwanda na Kilimo Tanzania
(TCCIA), Chama cha Wafanyabiashara Wanawake Tanzania (TWCC); Chama cha
Wafanyabiashara ya Madini na Nishati (TCME); vyama/mashirika ya wachimbaji
madini wadogo wadogo; Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOWAT), Chama
cha Waandishi Habari/Jukwaa la Wahariri Tanzania, Chama cha Mawakili Tanganyika
(TLS), Chama cha Mawakili Zanzibar (ZLS), Chama cha Madaktari Tanzania (MAT),
Taasisi ya Wahandisi Tanzania (IET) na Chama cha Wakandarasi Tanzania (CATA).
Makundi haya yatakuwa na wajumbe wawili kwa kila moja kwa jumla ya wajumbe 26.”
Mheshimiwa Spika,
Kwa
mujibu wa kifungu cha 22(1) cha Sheria kama ilivyo sasa, Bunge Maalum litakuwa
na jumla ya wajumbe 604, yaani Wabunge 357, Wawakilishi 81 na wajumbe 166
wanaowakilisha makundi mbali mbali. Mapendekezo haya ya Kambi Rasmi ya Upinzani
Bungeni yatafanya uwakilishi katika Bunge Maalum kupanuka hadi wajumbe 792 kwa
Tanzania yenye idadi ya watu milioni 45 kwa takwimu za sensa ya watu na makazi
ya mwaka 2012.
Hili,
kwa vyovyote vile, ni ongezeko kubwa la wajumbe wa Bunge Maalum. Hata hivyo,
ukubwa huu unaopendekezwa hauna tofauti kubwa sana na Mabunge Maalum ya nchi
nyingine ambazo zimekamilisha utungaji wa Katiba Mpya kwa kutumia utaratibu
huu. Kwa mfano, Bunge Maalum la Jamhuri ya Nepal la mwaka 2011 lilikuwa na
wajumbe 601 kwa nchi yenye idadi ya watu milioni 26; Bolivia (2009) lilikuwa na
wajumbe 255 katika nchi yenye watu milioni 9; Kenya (2005) lilikuwa na wajumbe
629 kwa idadi ya watu milioni 31; Eritrea (1997) lilikuwa na wajumbe 527 kwa
idadi ya watu milioni 3.2, wakati Bunge Maalum la Ufaransa ya Mapinduzi ya 1789
lilikuwa na wajumbe 1145 katika nchi iliyokuwa na idadi ya watu milioni 28.[iv]
Kikubwa
na muhimu zaidi, kwa mapendekezo haya, ni kwamba Bunge Maalum la Katiba
litakuwa na sura ya Kitanzania zaidi badala ya utaratibu wa sasa unaolifanya
Bunge Maalum kuonekana la kiCCM zaidi. Kwa kuongezea tu, Mheshimiwa Spika,
wadau karibu wote waliotoa maoni yao kwenye Kamati walipendekeza kuongezwa kwa
idadi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Kwa kigezo chochote kile, kwa hiyo, mapendekezo
haya ni ya kidemokrasia na tunaliomba Bunge lako tukufu liyaunge mkono ili
kuiwezesha nchi yetu kujipatia Katiba Mpya yenye sura halisi ya kitaifa kuliko
inavyopendekezwa sasa.
UWAKILISHI
WA ZANZIBAR KATIKA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa Spika,
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba imekwishatoa Rasimu ya Katiba kwa mujibu wa kifungu cha
19(1)(d) cha Sheria. Rasimu hiyo imepndekeza mabadiliko makubwa katika muundo
wa Jamhuri ya Muungano kwa kupendekeza muundo wa shirikisho lenye serikali
tatu. Baada ya kukamilika kwa mchakato wa kutoa maoni juu ya Rasimu hii kwa
mujibu wa kifungu cha 18, Tume itawasilisha ripoti kwa Rais na kwa Rais wa
Zanzibar kwa mujibu wa kifungu cha 20(1). Baada ya hapo, Rais, “... atachapisha Rasimu ya Katiba katika
Gazeti la Serikali na kwenye magazeti mengine pamoja na maelezo kwamba Rasimu
ya Katiba itawasilishwa kwenye Bunge Maalum kwa ajili ya kupitishwa Katiba
inayopendekezwa.”[v]
Mheshimiwa
Spika,
Ili
kutimiza matakwa haya ya Sheria na kwa kuzingatia mapendekezo ya Rasimu ya
Katiba iliyotolewa na Tume, Bunge lako tukufu linahitaji kuangalia upya suala
la uwakilishi wa Zanzibar katika Bunge Maalum. Kwa mujibu wa kifungu cha 22(2)
cha Sheria, idadi ya wajumbe wa Zanzibar katika Bunge Maalum watakaotokana na
makundi yaliyoainishwa katika kifungu cha 22(1)(c) “... haitapungua theluthi moja ya wajumbe hao.” Hii ina maana
kwamba, kwa uchache kabisa, wajumbe hao wa Zanzibar hawatapungua 55.
Rasimu
ya Katiba itakayojadiliwa na Bunge Maalum inahusu Katiba ya Jamhuri ya Muungano
peke yake. Rasimu hiyo imependekeza kwamba masuala yote yasiyo ya Muungano ya
Washirika wa Muungano, yaani Tanzania Bara na Zanzibar, yashughulikiwe na
Katiba za Washirika hao.[vi]
Kwa
sasa Wabunge wanaotoka Zanzibar katika Bunge la Jamhuri ya Muungano ni 83,
wakati Baraza la Wawakilishi Zanzibar lina wajumbe 76. Kwa ujumla, kwa hiyo,
ili kutekeleza matakwa ya kifungu cha 22(1) na (2) cha Sheria, Zanzibar itakuwa
na wajumbe 219 katika Bunge Maalum lenye wajumbe 604, sawa na takriban 36% ya
wajumbe wote. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inataka kujua: kama ilikuwa
busara na sahihi kwa nusu ya wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutoka
Zanzibar, kwa nini isiwe busara na sahihi vile vile kwa nusu ya wajumbe wa
Bunge Maalum litakaloijadili na kuipitisha Katiba Mpya hiyo kutoka Zanzibar? Au
ndio kusema kwamba hoja za usawa kati ya nchi Washirika wa Muungano huu ni
kelele za majukwaani tu?
Mheshimiwa
Spika,
Profesa
Palamagamba J.A.M. Kabudi wa Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na
mjumbe wa Tume aliwahi kusema kwenye Semina
ya Wabunge Juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba iliyofanyika hapa
Dodoma tarehe 12 Novemba 2011 kwamba: “Katika
kuandika katiba mpya, wabia wa Muungano wanarudi kwa usawa.” Kwa sababu
hiyo, na kwa kuzingatia mapendekezo ya ‘hadhi na haki sawa’ baina ya Washirika
wa Muungano yaliyoko katika Rasimu ya Katiba,[vii]
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba idadi ya wawakilishi wa
Zanzibar katika Bunge Maalum iongezwe hadi kufikia nusu ya wajumbe wote wa
Bunge Maalum.
Hili
linawezekana kwa namna mbili. Kwanza, kwa kuongeza idadi ya wajumbe waliotajwa
katika kifungu cha 22(1)(c) hadi 354 kama tulivyopendekeza katika Maoni haya.
Na pili, kwa kurekebisha kifungu cha 22(2) ili kisomeke kwamba idadi ya wajumbe
kutoka Zanzibar ‘haitapungua asilimia hamsini na tano ya wajumbe hao.’ Kama
pendekezo hili litakubaliwa na Bunge lako tukufu, wajumbe wa Bunge Maalum kutoka
Zanzibar wataongezeka kutoka 214 kwa mujibu wa Sheria ilivyo sasa, hadi 323.
Muhimu zaidi, Bunge Maalum litakuwa limetimiza matakwa ya usawa wa Washirika wa
Muungano kwa kuwa na idadi sawa ya wajumbe katika Bunge hilo. Hili litaondoa
manung’uniko yanayoweza kujitokeza baadae kwamba Wazanzibari hawakutendewa haki
sawa katika Bunge la Katiba.
WATUMISHI
WA BUNGE MAALUM
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho mengine katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Hivyo
basi, aya ya 4 inapendekeza marekebisho ya kifungu cha 24(4) kama ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum baada ya kushauriana
na Naibu wake na taasisi husika,
atateua kutoka katika Bunge, Baraza la Wawakilishi na taasisi husika idadi ya watumishi kama itakavyoonekana inafaa kwa
utekelezaji wa majukumu na mamlaka ya Bunge Maalum.” Kama kilivyo hivi
sasa, kifungu hicho kinasomeka kama ifuatavyo: “Katibu wa Bunge Maalum baada ya kushauriana na Naibu Katibu wa Bunge
Maalum watateua watumishi kutoka kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi kwa
idadi watakayoona inafaa kwa ajili ya kutekeleza kwa ufanisi majukumu ya Bunge
Maalum.”
Mheshimiwa
Spika,
Kama
inavyoonekana wazi, mabadiliko pekee yanayopendekezwa na Muswada ni maneno
‘taasisi husika.’ Maneno haya hayajatafsiriwa mahali popote katika Sheria, na
Muswada uko kimya juu ya maana yake. Hata Maelezo ya Mheshimiwa Waziri wa
Katiba na Sheria mbele ya Kamati yako kimya juu ya maneno hayo.[viii]
Ukimya
huu una mwangwi mkubwa. Kama pendekezo hili litakubaliwa, kutakuwa na uwezekano
wa watumishi wa Bunge Maalum la Katiba kuteuliwa kutoka katika taasisi na idara
mbali mbali za serikali, au hata taasisi zisizokuwa za kiserikali. Kwa sababu
Bunge Maalum litatekeleza majukumu yake kwa muda maalum unaopendekezwa katika
aya ya 6 ya Muswada huu, ni wazi watumishi hao watatumikia Bunge Maalum on secondment kutoka kwenye taasisi zao
za mwanzo. Kwa maana hiyo, watumishi hao watawajibika kwa taasisi zao na
wanaweza kutumiwa na taasisi zao kutoa taarifa au siri muhimu juu ya shughuli
za Bunge Maalum kwa taasisi zao.
Kwa
upande mwingine, watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wamepewa kinga ya
kikatiba inayowakataza kupokea maelekezo kutoka taasisi nyingine nje ya Bunge.
Kama kifungu cha 4(3) cha Sheria ya
Uendeshaji Bunge, Na. 14 ya 2008, inavyoweka wazi, katika utekelezaji wa
majukumu yao, watumishi wa Bunge “...
hawatapokea maelekezo kutoka mahali popote nje ya Utumishi (wa Bunge).”
Katika mazingira haya, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba
mapendekezo ya kurekebisha kifungu cha 24(4) hayakidhi matakwa ya uhuru wa
Bunge Maalum na, kwa sababu hiyo, yasikubaliwe na Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa
Spika,
Kuna
hoja kubwa zaidi juu ya pendekezo hili. Hoja hii inahusu mamlaka ya Katibu wa
Bunge Maalum na Naibu wake kuteua watumishi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano na
Baraza la Mapinduzi Zanzibar kuwa watumishi wa Bunge Maalum chini ya kifungu
cha 24(4) cha Sheria, na pendekezo la Muswada la kukifanyia marekebisho.
Kwa
mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Bunge,
Katibu wa Bunge hana mamlaka ya kuteua watumishi wa Bunge peke yake. Hayo, kwa
mujibu wa Sheria hiyo, ni mamlaka ya pamoja kati ya Katibu na Tume ya Utumishi
wa Bunge na utekelezaji wake unahitaji mashauriano kati ya vyombo hivyo viwili.[ix]
Kwa sababu hiyo, na kwa kuzingatia utaratibu wa Sheria hiyo, Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni inapendekeza watumishi wa Bunge Maalum wateuliwe kutoka
miongoni mwa watumishi wa Bunge na Baraza la Wawakilishi baada ya mashauriano
kati ya Katibu wa Bunge Maalum na Naibu wake pamoja na Mwenyekiti na Makamu
Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Pendekezo hili lina faida kwamba watumishi wa Bunge
Maalum watakuwa wameteuliwa na watawajibika kwa Bunge Maalum na siyo kwa
taasisi nyingine nje ya Bunge Maalum. Kwa maana hiyo, pendekezo la Muswada juu
ya uteuzi wa watumishi wa Bunge Maalum nje ya Bunge la Jamhuri ya Muungano na
Baraza la Wawakilishi Zanzibar halina umuhimu na linapaswa kukataliwa.
TAFSIRI
YA RASIMU YA KATIBA
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba
inayohusu tafsiri ya maneno mbali mbali. Mapendekezo ya Muswada yanahusu
tafsiri ya maneno ‘Rasimu ya Katiba’ na ‘Kanuni.’ Pendekezo la kutafsiri neno
‘Kanuni’ halina utatanishi wowote na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaliunga
mkono. Kwa upande mwingine, Kambi Rasmi Upinzani Bungeni inapinga tafsiri
inayopendekezwa ya maneno ‘Rasimu ya Katiba.’ Kwa mujibu wa aya ya 2 ya
Muswada, maneno ‘Rasimu ya Katiba’ yatakuwa na maana ya “... Rasimu ya Katiba ambayo imetayarishwa na Tume kutokana na maoni na
mapendekezo ya wananchi chini ya Sheria.”
Pendekezo
hili linapingana na maudhui ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwanza, pamoja
na kwamba maoni ya wananchi ni chanzo muhimu cha ripoti ya Tume na Rasimu ya
Katiba, maoni hayo sio chanzo pekee cha ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba. Kwa
mujibu wa kifungu cha 17(4) cha Sheria, Tume inatakiwa kupitia “na kuchambua michango, mawazo, maoni,
taarifa na mapendekezo yaliyokusanywa na kufanyiwa tathmini siku za nyuma....”
Kifungu hicho kimeorodhesha nyaraka nyingi muhimu na za kihistoria ambazo
zimejenga taswira ya kikatiba ya nchi yetu tangu uhuru wa Tanganyika mwaka
1961. Tume inawajibika kuzipitia na kuzichambua nyaraka zote hizo “katika kutekeleza majukumu yake chini ya
Sheria hii....”
Pili,
Tume pia inawajibika kutumia “tafiti za kiuchambuzi na kitaalam zitakazofanywa
na Tume”,[x]
na “nyaraka nyingine zozote ambazo Tume itaona ni muhimu.”[xi]
Vyanzo vyote hivi vinatakiwa kutumika katika matayarisho ya Rasimu ya Katiba.
Kwa maana hiyo, madhara ya mapendekezo ya Muswada juu ya tafsiri ya maneno ‘Rasimu
ya Katiba’ ni ya wazi na mabaya. Kama yatakubaliwa na kuwa Sheria, vyanzo vyote
hivi vya ripoti ya Tume na Rasimu ya Katiba vitakuwa redundant.
Aidha,
mapendekezo ya Tume na Rasimu ya Katiba yanayotokana na vyanzo hivyo yatakuwa
kinyume cha Sheria na yatabidi yaondolewe kwenye ripoti na Rasimu ya Katiba.
Kwa sababu hizi, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inapendekeza kwamba maneno
‘Rasimu ya Katiba’ yatafsiriwe kumaanisha “... Rasimu ya Katiba ambayo
imetayarishwa na Tume kwa mujibu wa Sheria hii.” Tafsiri hii inayopendekezwa inajumuisha
maoni ya wananchi pamoja na vyanzo vingine vyote vya ripoti ya Tume na Rasimu
ya Katiba vilivyoainishwa kwenye Sheria.
UHALALISHAJI
WA KATIBA MPYA
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
unapendekeza marekebisho katika kifungu cha 31 cha Sheria ya Mabadiliko ya
Katiba kinachohusu ‘uendeshaji wa kura ya maoni.’ Inapendekezwa kwamba kifungu
hicho kifutwe na badala yake kiwekwe kifungu kipya kitakachosema kwamba “masharti yote yanayohusu uendeshaji wa kura
ya maoni utawekwa na Sheria ya Kura ya Maoni.” Kwa vile tayari kuna Muswada wa Sheria ya Kura ya Maoni, 2013,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na pendekezo hili.
Hata
hivyo, kifungu cha 31 sio kifungu pekee katika Sheria hii chenye masharti ya
uendeshaji wa kura ya maoni. Kuna vifungu vingine vinavyotaja au kuweka
utaratibu wa kura ya maoni. Ukweli ni kwamba Sehemu ya Sita yote inayohusu
‘uhalalishaji wa Katiba Inayopendekezwa’ inahusika na masuala mbali mbali ya
kura ya maoni. Vile vile, kifungu cha 4(1)(n) na (2) navyo pia vinataja kura ya
maoni. Kwa maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, vifungu hivi pamoja na
Sehemu ya Sita yote vinahitaji kurekebishwa kwa kufutwa.
Mheshimiwa
Spika,
Muswada
unapendekeza kufanya marekebisho katika kifungu cha 27(2) cha Sheria kinachohifadhi
‘uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge Maalum’ kwa kuweka
kinga ya mashtaka dhidi ya wajumbe wa Bunge Maalum. Zaidi ya hayo, Muswada
unapendekeza muda usiozidi siku sabini kwa Bunge Maalum kujadili Rasimu ya
Katiba. Muda huo unaweza kuongezwa kwa siku nyingine zisizozidi ishirini kwa
ridhaa ya Rais “baada ya kukubaliana na
Rais wa Zanzibar....” Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inakubaliana na
mapendekezo yote haya ya Muswada kwa caveat
kwamba pendekezo la muda wa nyongeza lisiwekewe muda mahsusi. Hii ni kwa lengo
la kuwezesha muda kuongezwa kulingana na hali halisi ya majadiliano ndani ya
Bunge Maalum.
JEDWALI
LA MAREKEBISHO LA SERIKALI
Mheshimiwa
Spika,
Serikali
iliwasilisha Jedwali la Marekebisho ya Muswada huu mbele ya Kamati ikipendekeza
marekebisho kadhaa katika Muswada na katika Sheria mama. Mapendekezo haya ni ya
aina mbili. Kwanza, ni mapendekezo ya marekebisho ya Muswada uliosomwa mbele ya
Bunge lako tukufu katika Bunge la Kumi na Moja, na ambayo yalijadiliwa na
Kamati na wadau mbali mbali. Haya ni marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu
A, B na D ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali. Marekebisho haya yanaenda
sambamba na matakwa ya kanuni ya 84(3) na (4) ya Kanuni za Kudumu na kwa hiyo
yanakubalika kikanuni.
Kwa
upande mwingine, marekebisho yanayopendekezwa katika sehemu C na E za Jedwali
la Marekebisho ya Serikali ni mambo mapya ambayo hayakuwepo kwenye Muswada
uliosomwa kwa Mara ya Kwanza katika Bunge lililopita. Marekebisho haya
hayakujadiliwa na wadau wan je ya Bunge, na hayajulikani kwa Wabunge wasiokuwa
wajumbe wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala. Kwa sababu hiyo, marekebisho
haya yanakiuka masharti ya kanuni ya 86(7) ya Kanuni za Kudumu inayoelekeza
kwamba “mjadala wakati wa Muswada wa
Sheria Kusomwa Mara ya Pili utahusu ubora na misingi ya Muswada huo tu.”
Ili kulinda heshima ya Bunge lako tukufu, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inakuomba, Mheshimiwa Spika, utekeleze wajibu wako chini ya kanuni ya 5(2) ya
Kanuni za Kudumu kwa kufutilia mbali sehemu C na E za Jedwali la Marekebisho ya
Serikali kwa sababu zinakiuka matakwa ya kanuni tajwa ya Bunge lako tukufu.
Mheshimiwa
Spika,
Sehemu
C ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali tunaokuomba uifutilie mbali
inapendekeza kuongezwa kwa kifungu kipya cha 22A katika Sheria. Katika
pendekezo la awali kuhusu kifungu hicho, ilikuwa inapendekezwa kumfanya Spika
wa Bunge hili tukufu kuwa Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalum kwa ajili ya
kutengeneza Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum, na kwa ajili ya uchaguzi wa
Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Baada ya Kamati kuhoji na
kuelezwa kwamba Spika/Mwenyekiti wa Muda atakuwa pia na haki ya kugombea kuwa
Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum na hivyo kutengeneza mgongano
wa wazi wa maslahi, Kamati ilielekeza kwamba Katibu na Naibu Katibu wa Bunge
Maalum watasimamia uchaguzi wa Mwenyekiti wa Muda ambaye hatakuwa na haki ya
kugombea nafasi ya Mwenyekiti au Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum. Hata hivyo,
hoja ya msingi kwamba hili ni pendekezo jipya ambalo halikuwepo kwenye Muswada
uliosomwa Mara ya Kwanza inabaki pale pale.
Kuhusu
sehemu E ya Jedwali la Marekebisho ya Serikali, sehemu hiyo inapendekeza
kufifisha matakwa ya kifungu cha 26(2) cha Sheria inayoweka masharti ya
kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa theluthi mbili ya wajumbe wote wa Bunge
Maalum wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka
Zanzibar. Pendekezo jipya ni kupunguza idadi ya uungwaji mkono hadi wingi wa
kawaida (simple majority) ya wajumbe
wote wanaotoka Tanzania Bara na idadi hiyo hiyo ya wajumbe wanaotoka Zanzibar
endapo Bunge Maalum litashindwa kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa theluthi
mbili baada ya kupiga kura mara mbili. Pendekezo hili nalo linakiuka matakwa ya
kanuni ya 86(7) na linapaswa kuondolewa katika mjadala wa Muswada huu.
MENGINEYO
KUITISHWA
TENA BUNGE MAALUM?
Mheshimiwa
Spika,
Kuna
maeneo mengine ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ambayo, kwa maoni ya Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, yanahitaji kufanyiwa marekebisho ili kuwezesha
utekelezaji bora wa Sheria hii. Eneo mojawapo ni masharti ya kifungu cha 28(2) yanayoruhusu
Bunge Maalum kuitishwa tena baada ya kukamilisha majukumu yake kwa mujibu wa
Sheria na kuvunjwa chini ya kifungu cha 28(1) cha Sheria hii.
Kifungu
cha 28(1) kinasema: “Baada ya kutunga
Katiba Inayopendekezwa, masharti yatokanayo na mashrti ya mpito, Bunge Maalum
litavunjwa na mamlaka ya kutunga masharti ya Katiba inayopendekezwa, masharti
yatokanayo na masharti ya mpito yatakoma.” Kwa upande mwingine, kifungu cha
28(2) kinatengua masharti ya kifungu cha 28(1) kwa maneno yafuatayo: "Kuvunjwa na kukoma kwa mamlaka ya
Bunge Maalum hakutachukuliwa kuwa kunaondoa mamlaka ya Rais kuliitisha tena
Bunge hilo kwa lengo la kuboresha masharti yaliyomo kwenye Katiba
inayopendekezwa.”
Mheshimiwa
Spika,
Misingi
mikuu ya tafsiri za kisheria inaelekeza kwamba chombo chenye mamlaka au
majukumu ya kisheria ya kufanya jambo fulani kikishakamilisha kutekeleza mamlaka
au majukumu yake hayo kinakuwa functus
officio katika jambo hilo, yaani kinakuwa hakina mamlaka tena kisheria juu ya
jambo hilo.[xii]
Huu ndio msingi wa kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Athari
ya kifungu cha 28(2) ni kulifufua kutoka katika wafu Bunge Maalum ambalo, kwa
mujibu wa kifungu cha 28(1), linakuwa limekuwa functus officio baada ya kupitisha Katiba Mpya na masharti ya
mpito. Na hii inafanywa na Rais ambaye – na chama cha siasa anachokiongoza – ni
mdau mkubwa wa mchakato wa Katiba Mpya.
Katika
Maoni yetu wakati wa mjadala wa kupitishwa kwa Sheria hii mwezi Novemba 2011,
tulisema yafuatayo juu ya kifungu hiki: “Maana
halisi ya maneno haya ni kwamba Rais atakuwa na mamlaka ya kuita tena Bunge la
Katiba ili lifanye marekebisho ya mambo ambayo yeye au serikali yake au chama
chake hawayapendi katika Katiba Mpya kabla haijapigiwa kura ya maoni na
wananchi! Kama chombo huru cha wananchi, Rais hawezi kujipa madaraka ya
kupingana na kauli ya wananchi kupitia Bunge la Katiba.”
Katika
mapendekezo yake kwa timu ya Wataalam wa Serikali iliyoundwa kufuatia mkutano
wa tarehe 26 Novemba, 2011 kati ya CHADEMA na Rais Jakaya Kikwete, CHADEMA
ilipendekeza kwamba kifungu cha 28(2) kifutwe kabisa.[xiii]
Huu ni wakati muafaka kukiangalia upya kifungu hiki ambacho kinaweza kuleta
mgogoro usiokuwa na sababu endapo Rais ataamua kuliitisha tena Bunge Maalum kwa
sababu Serikali au chama chake hakikubaliani na Katiba Mpya iliyopitishwa na
Bunge Maalum.
MCHAKATO
WA KATIBA YA TANGANYIKA NA ZANZIBAR
Mheshimiwa
Spika,
Tarehe
3 Juni, 2013 Tume ilichapisha Rasimu ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 2013. Kwa kufanya hivyo, na kwa
mujibu wa kifungu cha 18(5) cha Sheria, Tume imekamilisha jukumu lake la kwanza
baada ya kukamilisha zoezi la kukusanya maoni ya Watanzania juu ya Katiba Mpya.
Rasimu hii inapendekeza mambo mengi na muhimu kwa mustakbala mzima wa nchi yetu
na tayari imezua mjadala mkali wa kitaifa. Mwanazuoni mmoja maarufu nchini ameyaita
mapendekezo ya Rasimu ‘Mapinduzi ya Kimya Kimya’[xiv];
wakati mwingine amehoji kama Rasimu hii ni ‘Mwarobaini au Sanduku la Pandora?’[xv]
Aidha, Profesa Issa G. Shivji ambaye pengine ni msomi maarufu wa masuala ya
kikatiba katika sehemu hii ya Afrika, ameonyesha kile ambacho amekiita ‘Utatanishi na Ukimya Katika Rasimu ya Katiba
Mpya.’ [xvi]
Kwa
maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, kama ilivyo kwa wadau wengine ambao
wamezungumzia Rasimu hiyo ya Katiba, eneo muhimu pengine kuliko yote ni muundo
wa Jamhuri ya Muungano kama shirikisho lenye serikali tatu. Kwa sababu hiyo,
Rasimu ya Katiba iliyotolewa na Tume imejikita katika masuala ya Muungano tu. Na
kwa mujibu wa Mwenyekiti wake, Tume haikushughulikia masuala yasiyokuwa ya
Muungano ya Tanganyika na Zanzibar kwa sababu mambo hayo yanatakiwa
kushughulikiwa na Katiba za Washirika wa Muungano.
Kwa
maana hiyo, masuala haya sasa itabidi yashughulikiwe kwa utaratibu mwingine wa
kisheria Zanzibar na Tanganyika vile vile, ambao utakuwa tofauti na utaratibu
uliowekwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kutokana na mapendekezo ya Rasimu ya
Katiba, mchakato wa Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano hautakamilika bila ya kuwepo,
na kukamilika, kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa masuala yasiyokuwa ya Muungano
ya Tanganyika na ya Zanzibar.
Mheshimiwa
Spika,
Kuanza
na kukamilika kwa mchakato wa Katiba Mpya kwa mambo yasiyokuwa ya Muungano ya
Tanganyika na Zanzibar ni suala muhimu kwa muundo wowote wa Serikali ya Jamhuri
ya Muungano au hata bila Muungano kuwepo, kwa sababu zifuatazo. Kwanza, hata
kama muundo wa Muungano utakuwa wa serikali moja, au mbili za sasa, au tatu
zinazopendekezwa na Rasimu, ni lazima masuala yote yanayoihusu Tanganyika yaingizwe
kwenye mchakato wa Katiba Mpya. Hii ni kwa sababu Rasimu inahusu masuala saba
ya Muungano tu, na Zanzibar ina Katiba yake tayari. Pili, hata kama wananchi wa
Tanzania watakataa kuendelea na Muungano wa aina yoyote na kudai uhuru kamili
wa Washirika wa Muungano, bado masuala ya Katiba Mpya ya Tanganyika na Zanzibar
yatahitajika kufanyiwa kazi. Tatu, bila masuala ya Tanganyika kuamuliwa katika
Katiba Mpya, mchakato mzima hautakamilika, na kwa maana hiyo, hakuwezi kukawa
na uchaguzi wowote wa Jamhuri ya Muungano kwa upande wa Tanganyika.
Kwa
vyovyote vile, constitutional gridlock
hii lazima ipatiwe suluhisho. Kwa sababu hiyo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kwamba mchakato wa Katiba Mpya ya Tanganyika na marekebisho ya
Katiba ya Zanzibar, 1984 uanze mara moja ili uendane sambamba na mchakato wa
Katiba Mpya ya Jambhuri ya Muungano. Kwa vyovyote vile, kwa maoni yetu, Sheria
ya Mabadiliko ya Katiba kama ilivyo sasa haiwezi kutumika kwa ajili ya mchakato
huo kwa sababu sheria hiyo ilitungwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba ya
Muungano tu.
Tume
ya Mabadiliko ya Katiba iliundwa kwa ajili ya mchakato wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Na Tume yenyewe imekiri kwamba haikujishughulisha na masuala yasiyokuwa ya
Muungano kwa sababu hayakuwa sehemu ya majukumu iliyokabidhiwa kisheria. Kwa
muundo wake, Tume hiyo haiwezi kujibadilisha na kuwa Tume ya Katiba ya
Tanganyika. Kwa maana hiyo, mchakato wa Katiba ya Tanganyika unatakiwa kuwekewa
utaratibu mpya na tofauti kabisa wa kisheria na wa kitaasisi. Hii itahitaji
kutungwa kwa sheria mpya kwa ajili ya mchakato huo.
Sambamba
na mchakato wa Katiba ya Tanganyika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inapendekeza kuanzishwa kwa mjadala juu ya masuala ya mpito kwa sababu kuna
uwezekano mkubwa kwamba Katiba Mpya, ya Muungano peke yake au ya Muungano na za
Washirika wake, yaani Tanganyika na Zanzibar, zisiwe tayari kabla ya Uchaguzi
Mkuu wa 2015. Au hata kama zitakuwa tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu, kuna
uwezekano mabadiliko makubwa ya kisheria na ya kitaasisi yatakayohitajika kwa
ajili ya utekelezaji wa Katiba Mpya, yasiwe tayari kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao.
Kwa kuangalia mfano wa Kenya, Katiba Mpya ya nchi hiyo ilikamilika mwezi
Agosti, 2010. Hata hivyo, mabadiliko mbali mbali ya kisheria na kitaasisi kwa
ajili ya utekelezaji wa Katiba hiyo yalichukua zaidi ya miaka miwili na nusu
hadi Uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi, 2013.
Ikumbukwe
kuwa Kenya haikuwa na suala la Muungano kama Tanzania. Sisi tuna Muungano wa
muundo ambao upande mmoja wa Muungano huo una dola yenye Katiba na taasisi kamili
za dola, wakati upande mwingine hauna dola wala Katiba na taasisi kamili za
dola. Hii ina maana kwamba maandalizi yetu ya kisheria na kitaasisi yanaweza kuhitaji
muda mrefu zaidi kuliko ilivyokuwa kwa Kenya. Hatuna budi kuanza kuyafikiria na
kuyajadili mambo haya muhimu sasa.
TUNDU A.M.
LISSU
0 comments:
Post a Comment