MBUNGE wa Bukombe, Profesa Kulikoyela
Kahigi (CHADEMA) amembana Naibu Waziri Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,
Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (Tamisemi), Aggrey Mwanri, aeleze
takwimu za upatikanaji wa maji safi na salama kwa asilimia 52 amezipata
wapi wakati shule nyingi za msingi, sekondari na vijiji hakuna maji.
Profesa Kahigi alitaka maelezo hayo jana
bungeni alipokuwa akiuliza swali la nyongeza na kumtaka naibu waziri
huyo aeleze ni jinsi gani amepata takwimu hizo wakati katika maeneo
mengi ya wilaya ya Bukombe kuna uhaba mkubwa wa maji.
Aidha Mbunge huyo alitaka serikali
ieleze ni lini miradi ya maji itakamilika katika mji mdogo wa Ushirombo
na maeneo ya Iyovvu yaliyoko katika wilaya hiyo.
Awali katika swali la msingi la Profesa
Kahigi, alitaka kujua serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi
wa Bukombe katika mji mdogo wa Ushirombo na vijiji vyake wanapata maji
safi na salama katika kipindi cha miaka mitano.
Akijibu maswali hayo Mwanri alikiri kuwa
wilaya hiyo inakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji lakini takwimu
alizopata zinatoka katika ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
Mwanri alisema kuwa upatikanaji wa maji
katika wilaya ya Bukombe na Mbogwe kwa wakazi 525,746 umefikia asilimia
52 kwa Julai, mwaka huu, huku asilimia 40 ilifikiwa Desemba mwaka 2012
kwa vijiji vya wilaya hiyo.
Alisema kuwa ongezeko hilo kwa kiasi
kikubwa limechangiwa na utekelezaji wa program ya maji vijijini na usafi
wa mazingira (RWSSP).
Aidha Mwanri alisema kuwa ifikapo
Desemba 2013 inakadiriwa kuwa asilimia 60 ya wakazi wa maeneo ya vijiji
watakuwa wanapata maji safi na salama chini ya program ya matokeo
makubwa sasa (Big Results Now).
Mwanri alisema kuwa katika mwaka wa
fedha 2013/14 wilaya hiyo imeidhinishiwa sh bilioni 1.083 kwa ajili ya
kujenga na kukarabati miundombinu ya maji.
0 comments:
Post a Comment