HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO PETER PINDA (MB), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI WA KUHITIMISHA SHUGHULI ZA MKUTANO WA 13 WA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA TAREHE 09 NOVEMBA, 2013!!




  UTANGULIZI  
            
a)        Masuala ya Jumla

Mheshimiwa Spika,
1.    Leo tunahitimisha shughuli za Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge lako Tukufu.  Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa kutufikisha salama siku ya leo.

Mheshimiwa Spika,
2.     Mkutano huu ulijumuisha kazi kubwa zifuatazo:

Kwanza: Kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2014/2015; 

Pili: Kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria mbalimbali wa Mwaka 2013, [The Written Laws (Miscellaneous Amendments (No. 3) Bill 2013]; 

Tatu: Kujadili Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu wa Mwaka 2013 [The GEPF Retirement Benefit Bill, 2013]; na

Nne: Kujadili Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (The Constitutional Review Act) sura ya 83.



3.    Nitumie nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa kushiriki katika Kamati ya Mipango hapa Bungeni kwa kujadili kwa kina mapendekezo yaliyowasilishwa na Serikali kuhusu Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2014/2015.  Napenda kuwahakikishia kuwa, maoni na ushauri kama yalivyotolewa na Waheshimiwa Wabunge yatazingatiwa na Serikali kila moja kwa uzito wake wakati wa maandalizi ya Bajeti ya 2014/2015. Vilevile niwashukuru kwa kujadili na kupitisha Muswada wa Sheria ya Mfuko wa Akiba wa GEPF wa Mafao ya Wastaafu. 

b)    Maswali

Mheshimiwa Spika,
4.    Pamoja na kukamilisha kazi hizo muhimu, pia katika Mkutano huu, jumla ya maswali 120 ya msingi na 305 ya nyongeza ya Waheshimiwa Wabunge yalijibiwa na Serikali.  Aidha, Maswali 6 ya msingi na 6 ya nyongeza yalijibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.

c)    Kauli za Mawaziri/Maazimio

Mheshimiwa Spika,
5.    Mkutano huu pamoja na kazi za msingi zilizopangwa, Waheshimiwa Wabunge walipata 
fursa ya kujadili Azimio la Kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu msimamo wake katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

(d)    Hotuba ya Mheshimiwa Rais,

Mheshimiwa Spika,
6.    Katika Mkutano huu pia, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kumsikiliza Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akizungumza na Wananchi kupitia Bunge lako Tukufu.  Mtakubaliana nami kwamba hotuba ya Mheshimiwa Rais ilikuwa nzito na yenye kuonesha umakini, umahiri na busara ambazo ni sifa mojawapo za Rais wetu kati ya nyingi nzuri alizonazo. Tunachotakiwa ni kutumia maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuyafikisha kwa Wananchi katika maeneo yetu ili nao waweze kuelewa hali halisi ya yanayotokea katika Jumuiya yetu. Aidha, Hotuba ya Rais imegusa maeneo mengine ambayo sisi Wabunge tunatakiwa kushirikiana na Wananchi katika kujipanga vizuri namna ya kukabiliana na matatizo yaliyojitokeza.

II:    UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA MWAKA 2013/2014

(a)    Mwenendo wa Mapato na Matumizi  ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya Mwaka 2013/2014

Mheshimiwa Spika,
7.    Hotuba yangu kwa leo imejikita zaidi kuelezea utekelezaji wa Mpango wa Bajeti ya Mwaka 2013/2014 na maeneo machache katika Sekta ya Kilimo na Nishati. Lakini kabla ya kuelezea mwenendo wa Mapato na Matumizi ya Serikali katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014, naomba kueleza kwa muhtasari kuhusu mwenendo wa baadhi ya viashiria muhimu vya uchumi hususan Ukuaji wa Uchumi na Mfumuko wa Bei. Taarifa za awali zilizotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu zinaonesha kwamba Ukuaji wa Pato la Halisi la Taifa katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2013, ulikuwa Asilimia 7.0 ikilinganishwa na ukuaji wa Asilimia 6.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2012.  Sekta zilizoonesha kuwa na Viwango vikubwa vya ukuaji ni pamoja na Sekta ya Mawasiliano na Usafirishaji ambayo imekua kwa Asilimia 18.4, Sekta ya Fedha Asilimia 14.6 na Sekta ya Ujenzi Asilimia 8.7.
    
Mheshimiwa Spika,
8.    Kwa upande wa Mfumuko wa Bei, takwimu zinaonesha kuwa kasi ya upandaji bei imepungua kutoka Wastani wa Asilimia 13.5 Mwezi Septemba, 2012 hadi Asilimia 6.1 Mwezi Septemba, 2013. Kushuka kwa Mfumuko wa Bei kumechangiwa zaidi na upatikanaji wa chakula cha kutosha ndani ya Nchi. Mwenendo huu mzuri wa viashiria vya uchumi jumla unatupa matumaini makubwa kwamba jitihada za Serikali za kuimarisha usimamizi wa Uchumi na kuleta Maendeleo endelevu ya Wananchi wetu zinaanza kuzaa matunda.

Mheshimiwa Spika,

9.    Katika Robo ya Kwanza ya mwaka 2013/2014 kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba 2013, Mapato yote yaliyokusanywa na Hazina yalifikia Shilingi Trilioni 3.08; sawa na Asilimia 85.7 ya makadirio ya Shilingi Trilioni 3.59. Pamoja na mwenendo huo wa ukusanyaji mapato, changamoto kubwa zinazokabili eneo la Mapato ya Serikali ni kuchelewa kuanza kwa wakati kwa ukusanyaji wa Mapato katika baadhi ya vyanzo vya mapato. Changamoto nyingine ni Miundombinu isiyokidhi mahitaji ya usafirishaji endelevu hasa reli ya kati, bandari, usafiri wa Anga na barabara.  Miundombinu Bora ni muhimu katika kuchochea ukuaji wa Uchumi na Kukuza Ajira; na hivyo kuiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi kutokana na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi. Serikali inafanyia kazi changamoto hizo ili kuzipatia ufumbuzi mapema.

Mheshimiwa Spika,
10.    Kwa upande wa matumizi, hadi kufikia mwezi Septemba 2013; matumizi yalifikia Shilingi Bilioni 3,806.5, sawa na Asilimia 98.5 ya lengo la kutumia Shilingi Bilioni 3,854.2. Kati ya matumizi hayo, Shilingi Bilioni 3,058 ni Matumizi ya Kawaida na Shilingi Bilioni 747.9 ni Matumizi ya Maendeleo.  Katika kipindi hiki, sehemu kubwa ya matumizi ya Serikali ya Kawaida na Maendeleo imeelekezwa katika maeneo yenye kuleta ufanisi na tija kubwa kama vile kuboresha miundombinu ya barabara, ambayo mgao wake ulikuwa Shilingi Bilioni 182.5 za Matumizi ya Kawaida na Maendeleo, Sekta ya Elimu Shilingi Bilioni 229.2; Sekta ya Nishati, Shilingi Bilioni 159.9; Sekta ya Kilimo Shilingi Bilioni 119.6 na Sekta ya Maji Shilingi Bilioni 51.3. Vilevile, Serikali imelipa Mishahara ya Watumishi wa Umma kwa wakati. Changamoto kubwa iliyopo kwenye matumizi ya Serikali ni kuwepo kwa mahitaji makubwa ya matumizi yasiyowiana na mapato; jambo ambalo linailazimu Serikali kukopa kutoka Mabenki ya Ndani. Serikali itaendelea kuoanisha Matumizi na ukusanyaji wa Mapato, hasa yale ya ndani pamoja na kuzingatia viwango vya Matumizi vilivyoidhinishwa na Bunge. Aidha, Serikali itaendelea kuweka msisitizo wa kuelekeza Matumizi kwenye vipaumbele vilivyoainishwa katika Bajeti ya Serikali ambavyo ni vyanzo muhimu vya kuongeza Mapato, Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini.

III:    UTEKELEZAJI WA MFUMO MPYA WA TEKELEZA KWA MATOKEO MAKUBWA SASA (BIG RESULTS NOW - BRN)

(a)    Muundo wa Mfumo

Mheshimiwa Spika,
11.    Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa Serikali ilianzisha Mfumo mpya wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa  au Big Results Now (BRN) ili kuongeza ufanisi katika usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mipango yetu ya Maendeleo, hususan, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016).  Hatua hii ilichukuliwa baada ya kuona namna Mfumo kama huo ulivyoziwezesha Nchi kadhaa, na hasa Nchi ya Malaysia, kupiga hatua kubwa za kimaendeleo kiuchumi na kijamii katika kipindi kifupi. Kwa ukumbusho tu, Mfumo huo unatekelezwa katika Maeneo Sita ya Matokeo muhimu Kitaifa (National Key Results Areas) katika awamu yake ya kwanza, ambayo ni Nishati ya Umeme; Uchukuzi; Kilimo; Elimu; Maji na Ukusanyaji wa Mapato;

Mheshimiwa Spika, 
12.    Katika Hotuba yangu ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Mbili wa Bunge, tarehe 6 Septemba 2013, nilitoa taarifa ya awali kuhusu utekelezaji wa Mfumo huu Mpya kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013. Katika taarifa hiyo, nilieleza kuwa tumepiga hatua za kuridhisha katika uundaji wa Mfumo wa  kuleta matokeo ya haraka, ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuteua Uongozi wa juu wa Taasisi Maalum yaani "President’s Delivery Bureau (PDB)” inayomsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia ipasavyo utekelezaji wa Miradi na Programu zilizoainishwa.  Hivi sasa zoezi la kuajiri Watumishi wa Taasisi ya "President’s Delivery Bureau” na Vitengo vya Wizara vya Ufuatiliaji yaani Ministerial Delivery Units (MDUs) watakaochukua nafasi za Watumishi walioazimwa kutoka kwenye Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali, Sekta Binafsi, na Asasi Zisizo za Kiserikali ambao walikuwepo katika hatua zake za maandalizi limeanza. Ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru wote waliotumika katika chombo hiki tangu kilipoundwa kwa uzalendo na weledi waliouonesha katika kipindi hiki cha mwanzo na cha mpito;

Mheshimiwa Spika, 
13.    Napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba hadi sasa vitengo vya ufuatiliaji katika Wizara zote sita (6) zinazosimamia utekelezaji chini ya Mfumo huu mpya vimeanzishwa na vinaandaa Taarifa za utekelezaji za kila wiki na kila mwezi, na kuziwasilisha kwenye Chombo cha President’s Delivery Bureau. Aidha, Kamati Maalum za kusimamia utekelezaji zinazoongozwa na Mawaziri husika zinakutana kila mwezi kujadili mwenendo wa utekelezaji na kushughulikia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika utekelezaji. Baraza la Kusimamia Mageuzi na Utekelezaji (Transformation and Delivery Council – (TDC)) limeundwa na lilikutana tarehe 11 Oktoba, 2013. Katika Kikao hicho, Baraza lilipokea na kujadili muhtasari wa Taarifa ya utekelezaji wa Mfumo mpya wa Kusimamia, Kufuatilia na Kutathmini Miradi ya Kipaumbele katika Maeneo Sita ya Matokeo ya Kitaifa. Baraza liliridhika na hatua za awali za utekelezaji na lilitoa mwongozo stahiki wa hatua za kuchukuliwa pale ilipohitajika. Baraza litaendelea kukutana mara kwa mara ili kutathmini na kutoa mwelekeo wa utekelezaji wa Mikakati iliyowekwa ya Mfumo huu mpya;

(b)    Utekelezaji wa Mikakati katika Maeneo Makuu Sita ya Matokeo Kitaifa;

Mheshimiwa Spika, 
14.    Utekelezaji wa mikakati katika maeneo makuu sita ya matokeo kitaifa ulianza mara baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika. Mafanikio ya kuridhisha yamepatikana katika kila moja ya maeneo yale sita, hasa ikizingatiwa kwamba Mfumo huu ni mageuzi makubwa sana katika utendaji Serikalini. Katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya mwaka huu wa fedha, kuanzia mwezi Julai hadi Septemba, 2013; baadhi ya matokeo yaliyopatikana ni pamoja na yafuatayo:
(a)    Katika Sekta ya Kilimo, Serikali inatekeleza miradi 26 ya umwagiliaji kwa Wakulima wadogo na pia imekarabati  maghala 26 ya mpunga kati ya 39 yanayotumiwa na wakulima katika maeneo yaliyopewa kipaumbele hasa katika eneo la SAGCOT.
(b)    Katika Sekta ya Nishati ya Umeme, jumla ya Wateja wapya 27,494 wameunganishwa na kupatiwa umeme, ikiwa ni Asilimia 18.3 ya lengo la kuunganisha wateja wapya 150,000 hadi mwisho wa mwaka 2013/2014. Aidha, vipande vya Bomba la Gesi 20,491 vinavyotosheleza ujenzi wa Kilomita 243.8 za Bomba la Gesi tayari vimewasili Nchini, na uchomeleaji wa Bomba la Gesi Asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umekamilika kwa Kilomita 124.3. Vilevile, Kilomita 447 za njia ya Bomba la Gesi zimesafishwa;

(c)    Katika Sekta ya Elimu, Shule za msingi 5,916 zilipatiwa mitihani ya marejeo na mazoezi, sawa na Asilimia 100 ya lengo la mwaka. Aidha, Mafunzo Kazini kuhusu ufundishaji yametolewa kwa Walimu katika Shule 1,325 sawa na Asilimia 65 ya lengo la Shule 2,048 kwa mwaka huu wa fedha;

(d)    Kwa upande wa huduma za maji, wananchi wapatao 752,000 waishio Vijijini wamepatiwa huduma ya maji. Mafanikio haya yanafanya idadi ya Wananchi waishio Vijijini ambao wanapata majisafi na salama kufikia takribani Milioni 15.9. Kasi hii ya upanuzi wa huduma za Maji Vijijini imewezekana baada ya Wizara ya Maji kugatua madaraka ya usimamizi wa miradi husika kwa Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za Wilaya, jambo ambalo limewafanya Watendaji kuwajibika na kuharakisha utendaji wao wa kazi. Aidha, hatua zilizochukuliwa zimeiwezesha Wizara ya Maji kuongeza ufanisi katika masuala ya ununuzi wa huduma, ikiwemo ujenzi na vifaa vyake, kutoka wastani wa siku 265 za hapo awali hadi siku 90 za sasa.

Mheshimiwa Spika,
15.    Mafanikio haya na mengine mengi ambayo sikuyataja hapa yameonyesha kuwa tukidhamiria, tunaweza kubadilisha kabisa matokeo ya juhudi zetu na kuifikia dhamira yetu ya kuwa ni Taifa la Kipato cha Kati ifikapo mwaka 2025;

Mheshimiwa Spika, 
16.    Kufuatia mafunzo yaliyotolewa mapema mwezi Juni, 2013 kwa Watendaji wa Wizara husika, Wakuu wa Mikoa wote, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya zote Nchini, mnamo Mwezi Septemba 2013 nilikutana na Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa yote Tanzania Bara ili kujadili kwa kina Taarifa za utekelezaji wa Miradi ya kipaumbele chini ya Mfumo huu. Aidha, katika Vikao hivyo, nimezielekeza Wizara, Mikoa na Halmashauri zote Nchini kufanya yafuatayo:-
    
(a)    Kuchambua miradi iliyopangwa kutekelezwa katika mwaka huu wa fedha ambayo ipo nje ya Mfumo  wa “Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa” kwa kutambua manufaa yanayotarajiwa baada ya kukamilika na mahitaji halisi; 

(b)    Kuipanga miradi hiyo kwa kipaumbele ili kuweka mkazo katika miradi itakayokamilika haraka na kuwa na manufaa makubwa kwa Wananchi; na,

(c)    Kuweka utaratibu wa Kimfumo na Kitaasisi wa kufuatilia utekelezaji wa miradi ya kipaumbele.

Mheshimiwa Spika, 
17.    Ninafurahi kutoa taarifa kuwa Wizara na Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeupokea mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa kwa hamasa kubwa. Ili kuhakikisha azma yao ya kutekeleza majukumu yao katika Mfumo huu kikamilifu, iliamuliwa kuwa Viundwe Vitengo vya kusimamia utekelezaji katika Ngazi ya Mkoa (Regional Delivery Units (RDUs), sambamba na vile Vitengo vya ufuatiliaji vya Wizara ili utekelezaji katika Maeneo Makuu ya Matokeo Kitaifa ufanyike kwa ufanisi na umakini stahiki. Hatua hii inazingatia umuhimu wa kuhakikisha kuwa maeneo kama Elimu na Maji ambayo Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa zina mchango mkubwa katika utekelezaji yanapata msukumo wa kutosha. Kazi hii imeshaanza, na taarifa zilizowasilishwa ni za kutia moyo sana.

Mheshishimiwa Spika,
18.    Kwa kuzingatia mafanikio ya awali yaliyopatikana, Serikali imetoa maelekezo kwa Wizara, Idara na Taasisi ambazo bado hazijaingia katika Mfumo wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa zisisubiri hadi zitakapoingia rasmi bali zianze kujipanga na kutekeleza mipango, miradi na program zao kwa kutumia mbinu ambazo zinatumika katika Mfumo huo pamoja na Rasilimali fedha na Wataalam waliopo.  Msisitizo ni kwamba Wizara zote na Mikoa ijipange upya na kuongeza ubunifu na kufanya vizuri zaidi katika kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha kwamba Taifa letu linafikia malengo ya maendeleo tuliyojiwekea katika Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025. Aidha, napenda kutumia fursa hii kutoa wito kwa Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha usimamizi wa Watendaji wao kwa kuzingatia taratibu za uwajibikaji zilizowekwa chini ya mfumo huu mpya ili kuleta ufanisi na tija ya utendaji Serikalini pamoja na kupata matokeo makubwa tarajiwa ya Kukuza Uchumi na kuondoa umaskini;


IV:    MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO YA TAIFA WA MWAKA 2014/2015

Mheshimiwa Spika,
19.    Mwanzoni mwa Mkutano huu wa Bunge Serikali iliwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo 2014/2015. Napenda kutumia fursa hii tena kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na michango yao mizuri ambayo itatuwezesha kuboresha Mpango na Bajeti ya Mwaka ujao wa Fedha 2014/2015. Aidha, namshukuru Mheshimiwa Stephen Wasira (Mb.) pamoja na Waheshimiwa Mawaziri wa Kisekta waliotoa maelezo fasaha ya ufafanuzi wa Hoja zilizojitokeza wakati wa Mjadala wa Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo. Kwa kuzingatia michango mizuri na yenye tija iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Mawaziri wakati wa kujadili Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2014/2015, nami naomba uniruhusu kusisitiza mambo machache kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Spika,
20.    Kama Waheshimiwa Wabunge watakavyokumbuka katika majadiliano yaliyokuwa yanaendelea, moja ya jambo ambalo Waheshimiwa Wabunge wamelizungumzia kwa kina, ni juu ya wingi wa vipaumbele vya Taifa. Aidha, imeonekana  pia kuwa miradi ya maendeleo ni mingi sana kiasi kinachosababisha  miradi hiyo kutotekelezeka kutokana na ufinyu wa rasilimali fedha. Napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa Vipaumbele vilivyopendekezwa na Serikali vinategemeana na vinalenga kutanzua vikwazo vikuu vya kiuchumi Nchini ili kufungua fursa za ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuharakisha maendeleo na ustawi wa Wananchi wa Tanzania. Pendekezo la Serikali ni kuwa njia bora si kupunguza vipaumbele hivi sasa, bali ni kupanga vizuri mtiririko wa utekelezaji wa miradi ndani ya kila kipengele ili kuongeza jitihada za kuongeza Mapato, na kusimamia nidhamu ya matumizi. 

Mheshimiwa Spika,
21.    Kwa kuwa Mpango huu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 - 2015/2016) ni wa kwanza unaojenga msingi wa mipango mingine ya maendeleo  ya miaka mitano itakayoandaliwa, ni dhahiri kuwa kasi ya utekelezaji wake itarahisisha utengenezaji wa mipango mingine na kupunguza vipaumbele vya msingi katika mipango ijayo. Hivyo, ninawaomba Waheshimiwa Wabunge washirikiane kwa karibu na Serikali kuhakikisha kuwa miradi iliyopangwa katika ngazi zote  inatekelezwa kwa ufanisi ili Mpango huu wa mwanzo utekelezeke kama ilivyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika,
22.    Mjadala na Hoja nyingine zilijielekeza katika changamoto za upatikanaji wa Ajira  kwa Vijana Nchini. Kulingana na Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, Asilimia 34.7 ya nguvu kazi ya Tanzania ni Vijana wa umri wa kati ya miaka 15 - 35. Kundi hili la Vijana ndilo lenye kiwango kikubwa cha ukosefu wa ajira cha Asilimia 13.4 hapa Nchini. Pamoja na kuwa Vijana hawa wamekuwa wakipata kazi hususan katika Sekta za Ujenzi, Kilimo na Hoteli, ajira zao nyingi zimekuwa za muda.   

23.    Katika kukabiliana na changamoto hii, Serikali imeandaa Programu ya Ajira kwa Vijana itakayotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu. Malengo ni kupatikana fursa za ajira 840,000 kwa kuwezesha jumla ya Miradi 10,000 ya Wahitimu wa Elimu ya Juu wapatao 30,000 kutoka Vyuo mbalimbali  ambao watatoa ajira za moja kwa moja kwa wahitimu wengine 270,000 na ajira zisizo za moja kwa moja 540,000. Programu hii itajengea Vijana uwezo katika stadi za kazi; ujasiriamali; na kuwapatia Vijana mitaji, nyenzo na vifaa vya kufanyia kazi; na kuwapatia Vijana maeneo ya uzalishaji na biashara. Serikali inatarajia kuelekeza fedha zaidi katika kipindi husika ili kuwezesha utekelezaji wa Programu hiyo. Aidha, naipongeza Sekta Binafsi kwa mchango wao mkubwa katika kukuza uchumi wa Nchi na kuongeza ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Spika, 
24.    Kilimo ni moja ya maeneo ya kipaumbele katika Mpango wa mwaka 2014/2015. Hili ndilo eneo kubwa kwa maana ya kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Wananchi wanaoishi Vijijini, kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa namna ambayo ni shirikishi ili kupunguza umaskini.  Hivyo, ili kujibu matatizo ya msingi ya umasikini wa kipato Mpango wa Maendeleo  2014/2015 utatoa kipaumbele katika mambo muhimu yafuatayo: 
(i)    Utafiti wa kilimo cha mazao, hususan katika uzalishaji wa mbegu bora, mifugo na uvuvi; 

(ii)    Kuimarisha huduma za ugani kwa kilimo, mifugo na uvuvi  na kuimarisha upatikanaji na matumizi ya mbolea kwa ajili ya kilimo; 

(iii)    Kuimarisha Ushirika wa Wakulima na Wafugaji;

(iv)    Kuongeza fursa za mikopo kwa wakulima, wafugaji na wavuvi ikiwa ni pamoja na kukamilisha uanzishwaji wa Benki ya Kilimo mwezi Januari 2014; 

(v)    Kuwezesha upatikanaji wa masoko ya mazao ya kilimo, na mifugo; 

(vi)    Kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji; 

(vii)    Upatikanaji wa ardhi kwa kilimo na mifugo kwa kuongeza kasi ya upimaji wa ardhi;  na 

(viii) Kuendeleza shughuli za kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi;

Mheshimiwa Spika, 
25.    Mpango wa Maendeleo huandaliwa katika ngazi zote Tano za Utawala kulingana na majukumu ya Serikali ambazo ni: 
Moja:    Vijiji na Mitaa; 
Pili:    Kata; 
Tatu:    Mamlaka za Serikali za Mitaa (Halmashauri); 
Nne:    Mikoa; na 
Tano:         Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali. 

Mamlaka husika katika ngazi zote zinatakiwa kuandaa Mipango yao kwa kuzingatia maeneo ya vipaumbele kama yalivyoainishwa katika Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2014/2015. Mipango lazima ilenge katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka hususan katika kuchochea maendeleo ya maeneo mengine na Programu nyingine katika ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini.  

Katika kila ngazi, Wadau wengine kama vile Sekta Binafsi, Asasi Zisizo za Kiserikali, Mashirika ya Dini na Washirika wa Maendeleo washirikishwe kikamilifu. Wizara, Idara zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali ziandae Mpango na kuuwasilisha Ofisi ya Rais, Tume ya Mipango Wiki ya Nne ya mwezi Januari, Mwaka 2014. 

Katika ngazi za Mikoa na Wilaya, uandaaji uanze katika ngazi ya Kijiji na Mtaa, Kata, Halmashauri na hatimaye kwenye Mkoa. Mpango uliopitishwa na Mkoa uwasilishwe Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Wizara ya Fedha, Wiki ya Nne ya Mwezi Januari, 2014.  Mpango wa Maendeleo wa Taifa utajadiliwa na Bunge kuanzia Mwezi Aprili hadi Juni, 2014 na utekelezaji wake utaanza Mwezi Julai 2014 hadi Juni 2015;

Mheshimiwa Spika, 
26.    Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2014/2015 ndiyo yatatumika katika utayarishaji wa Mipango ya Maendeleo ya Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala wa Serikali, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka ujao wa fedha 2014/2015. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge kutumia taarifa zilizotolewa hapa Bungeni kutoa ufafanuzi kwenye Vikao vya Baraza la Madiwani katika Halmashauri zao wakati wa kujadili Mipango yao. Aidha, napenda kutumia fursa hii kuzihimiza Mamlaka za Serikali za Mitaa kuainisha vipaumbele vinavyolenga katika maeneo yenye kuleta matokeo makubwa na ya haraka ya Kiuchumi na Kijamii; na pia yenye kuchochea maendeleo ya maeneo mengine. Vilevile, vipaumbele vya Halmashauri vilenge kufungulia fursa za ajira, kuongeza mapato ya ndani na kuvutia uwekezaji wa Sekta Binafsi katika maeneo yao.

V:    SEKTA YA KILIMO
a)    Hali ya chakula Nchini

Mheshimiwa Spika,
27.    Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa Chakula Nchini hadi kufikia Mwezi Oktoba 2013 ni ya kuridhisha kufuatia mavuno mazuri ya msimu wa kilimo wa 2012/2013 ambapo mazao yake yanaendelea kuingia sokoni kutoka maeneo mbalimbali hapa Nchini. Tathmini ya awali iliyofanyika mwezi Julai/Agosti, 2013 inaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya chakula katika Msimu wa kilimo wa 2012/2013 utafikia Tani 14,383,845 za chakula zikiwemo Tani 7,613,221 za mazao ya nafaka na Tani 6,770,624 za mazao yasiyo ya nafaka. Kiasi hicho cha chakula kilichozalishwa ni ongezeko la Tani 2,234,726 za chakula, ikilinganishwa na mahitaji ya chakula kwa mwaka 2013/2014 ya Tani 12,149,120. Kiwango hicho kinajumuisha Tani 354,015 za mahindi na Tani 466,821 za mchele. Hivyo napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla kuwa tutakuwa na chakula cha kutosha Nchini kwa Asilimia 118.


Mheshimiwa Spika, 
28.    Vilevile, tathmini hiyo inaonesha kuwa, pamoja na kuwepo kwa chakula cha kutosha na cha ziada, Halmashauri 61 katika Mikoa ya Manyara, Shinyanga, Simiyu, Arusha, Dodoma, Lindi, Tanga, Singida, Mara, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Pwani, Mtwara, Kigoma na Tabora zinatarajiwa kuwa na uhaba wa chakula.

29.    Natoa wito kwa Halmashauri zinazohusika katika Mikoa hiyo kufuatilia kwa karibu utaratibu wa kupata chakula kinachotolewa kutoka maeneo yenye ziada na kuhakikisha kuwa kinafika mapema kwenye maeneo yao kabla Wananchi wa maeneo hayo hawajaanza kulalamika. 

(b)    Mwenendo wa Bei za Vyakula Nchini

Mheshimiwa Spika, 
30.    Kutokana na hali ya upatikanaji wa chakula kuwa nzuri, Bei za wastani za vyakula hasa mahindi na mchele katika Soko Nchini zimeendelea kushuka. Kwa mfano, bei ya mahindi ilishuka kutoka Shilingi 774.30 kwa kilo mwezi Februari, 2013 hadi Shilingi 535.40 kwa Kilo mwezi Septemba 2013. Kwa upande wa mchele, bei kwa kilo moja imeshuka kutoka Shilingi 1,825.45 mwezi Februari, 2013 hadi kufikia Shilingi 1,206.70 mwezi Septemba 2013, na bei ya mchele imeshuka zaidi hadi kufikia Shilingi 1,146.70 katika mwezi Oktoba, 2013. 

(c)    Hali ya Ununuzi na Akiba ya Chakula ya Taifa

Mheshimiwa Spika, 
31.    Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula imepanga kununua Tani 250,000 za nafaka katika msimu wa 2013/2014. Hadi kufikia tarehe 23 Oktoba, 2013, Wakala alikuwa amekwishanunua kiasi cha Tani 218,412 za nafaka sawa na Asilimia 87.37 ya lengo lililowekwa ambapo Tani 217,919 kati ya hizo ni za Mahindi na Tani 493 ni za mtama. Aidha, hadi kufikia tarehe 23 Oktoba 2013, maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yalikuwa na jumla ya Tani 232, 921 za nafaka, kati ya hizo Tani 232,419 ni za mahindi na Tani 493,103 ni za mtama. Kiasi hiki cha nafaka kinajumuisha albaki ya Tani 25,452 za mahindi kutoka msimu uliopita wa 2012/2013. 

Mheshimiwa Spika, 
32.    Serikali inaendelea na tathmini ya kina ya hali ya chakula na lishe katika Halmashauri 61 zilizoainishwa kuwa na hali tete ya chakula kwa lengo la kubainisha idadi ya watu wenye uhaba wa chakula ili kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili. Nitumie fursa hii kwa mara nyingine tena kuwaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuwahimiza Wakulima hasa walioko katika maeneo yenye chakula cha ziada kuhifadhi Chakula cha kutosha kwa mahitaji ya Kaya zao. Aidha, Wakala wa Taifa na Hifadhi ya Chakula wajipange vizuri kuhamisha Chakula kutoka maeneo yenye ziada na kupeleka kwenye maeneo yaliyoainishwa kuwa na hali tete mara taarifa ya upungufu itakapotolewa.

Mheshimiwa Spika,
33.    Pamoja na juhudi za Serikali za kuhakikisha kwamba kuna chakula cha kutosha, natambua Changamoto zilizopo katika ununuzi wa Chakula kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula. Natambua kuwepo kwa madeni yanayotukabili kwenye ununuzi wa nafaka kwa ajili ya Wakala yaani NRFA.  Hata hivyo, Mikoa inayohusika na madeni hayo ni Arusha, Dodoma, Njombe, Shinyanga, Ruvuma, Rukwa na Tanga. Serikali itahakikisha deni hilo hilo linalipwa ndani ya mwaka huu wa fedha 2013/2014.

(d)    Mpango wa Pembejeo za Ruzuku

Mheshimiwa Spika, 
34.    Kama nilivyoeleza katika Mkutano wa 12 wa Bunge, katika msimu wa 2013/2014 Serikali imetenga jumla ya Shilingi Bilioni 112.564 kwa ajili ya ruzuku ya mbolea, na pembejeo. Aidha, nilielezea kuhusu utaratibu mpya wa kutoa ruzuku utakaohusisha uwiano wa Asilimia 80 kwa Vocha na Asilimia 20 mikopo.  Ili kuhakikisha Mfumo huu mpya unatekelezwa kikamilifu na kuleta matokeo yaliyotarajiwa, Serikali imetoa mafunzo ya utoaji pembejeo kwa njia ya mikopo kwa Washauri wa Kilimo wa Mikoa, Maafisa Ushirika wa Mikoa na Wilaya na Maafisa Kilimo wa Wilaya kwa awamu mbili. Awamu ya kwanza ikihusisha Mikoa ya Shinyanga, Geita na Manyara; na Awamu ya Pili inahusu Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Mbeya na Iringa. Aidha, uchambuzi wa takwimu za Vyama vya Ushirika na Vikundi vya Wakulima watakaokopeshwa pembejeo za Kilimo mwaka 2013/2014 umefanyika katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Njombe, Mbeya, Geita na Manyara.  Takwimu zinaonesha kuna SACCOS 214, AMCOS 163 na Vikundi vingine 51 vyenye Wakulima 88,290 watakopeshwa pembejeo za Kilimo. Natoa Wito kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendeleza mafunzo haya kwa Mikoa iliyobaki.

(e)    Hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo
Mheshimiwa Spika, 
35.    Kuhusu hali ya Usambazaji wa Vocha za Pembejeo katika Msimu wa 2013/2014 napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, jumla ya Vocha 2,796,300 kwa ajili ya Kaya 932,100 zikiwemo Vocha 932,100 za mbolea ya kupandia, 932,100 za mbolea ya kukuzia, Vocha 441,100 za mbegu za mahindi chotara; Vocha 432,000 za mahindi ya OPV na Vocha 60,000 za mbegu za mpunga zilisambazwa katika Mikoa yote hapa Nchini. Nitoe wito kwa Viongozi wa Mikoa na Wilaya kwa kushirikiana na Waheshimiwa Madiwani na Viongozi wengine kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata na wanatumia Vocha hizi kupata pembejeo kama ilivyokusudiwa. Aidha, tushirikiane kuhakikisha kuwa wale watakaokwenda kinyume na utaratibu huu wa usambazaji wa Vocha hizo wanashughulikiwa kwa mujibu wa Sheria.

(f)    Changamoto za Mbolea ya Minjingu

Mheshimiwa Spika,
36.    Juhudi za Serikali katika kuhakikisha upatikanaji wa Pembejeo za ruzuku ziko dhahiri.  Hata hivyo, imebainika kwamba katika mahitaji ya mbolea, kilio kikubwa cha Wakulima ni kupatiwa mbolea kwa wakati.  Aidha, wapo Wananchi wanaolalamikia mbolea ya Minjingu Mazao ambayo ni kweli hapo awali ilikuwa na matatizo.  Lakini sasa, mbolea hii imeboreshwa kwa kiwango kikubwa kwa kuongezewa virutubisho.

Mheshimiwa Spika,
37.    Mbolea ya Minjingu ya awali ilikuwa na virutubisho vya udongo viwili tu vya Kalisiumu na Fosfeti. Mbolea ya Minjingu Mazao imeboreshwa kwa kuongezwa virutubisho vinne zaidi na kufanya virutubisho hivyo kuwa sita yaani Kalisiumu, Fosfeti, Naitrojeni, Salfa, Boroni na Zinki. 

38.     Kwa msingi huo, Mbolea ya Minjingu mazao inaweza kutumika katika aina mbalimbali za udongo tofauti na ilivyokuwa awali. Aidha, Mbolea ya Minjingu Mazao ni ya chengachenga (granulated) tofauti na ya awali ambayo ilikuwa katika mfumo wa unga (dust) ambapo pengine matumizi yake hayakuwa rafiki kwa mkulima. Baada ya kuboreshwa, kwa sasa Mbolea hii ya Minjingu inatumika kwa mazao mengi hususan mahindi, mpunga na alizeti katika sehemu mbalimbali na aina mbalimbali za udongo. 

Mheshimiwa Spika    
39.    Mkulima anahitaji kutumia mifuko miwili ya mbolea ya Minjingu Mazao ya kilo 50 kila mmoja kwa wakati mmoja ikilinganishwa na mfuko mmoja wa kilo 50 wa mbolea ya DAP.  Hata hivyo, ukilinganisha na mbolea ya DAP, mkulima anayetumia Minjingu Mazao anawezesha shamba lake kupata virutubisho zaidi. Kwa hiyo, Mbolea ya Minjingu Mazao ni nafuu ikilinganishwa na Mbolea ya DAP. 

40.     Bei ya mbolea  ya Minjingu Mazao kwa mfuko mmoja ni Shilingi 32,500/= hivyo kwa mifuko miwili ni Shilingi 65,000 katika Wilaya zote Nchini ikilinganishwa na bei ya wastani ya Shilingi 75,000/= ya mfuko mmoja wa DAP. Aidha, kwa aina zote mbili za mbolea zinapotumika kupandia, lazima mkulima aweke mbolea nyingine ya kukuzia ambayo ina virutubisho vingi vya  Naitrogeni kama CAN au UREA.

41.    Majaribio ya kutumia Mbolea ya Minjingu yalianza mwaka 1977 kuendelea hadi mwaka 2006 ikiwa katika hali ya unga. Mwaka 2007 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuiweka katika hali ya chenga chenga (granulation) ingawa virutubisho havikuboreshwa. Mbolea hiyo iliendelea kutumika katika hali hiyo hadi mwaka 2009. Hivyo, mwaka 2010 Mbolea hiyo iliboreshwa kwa kuongezea virutubisho ambavyo baada ya utafiti wa kuihakiki (validation) iliingizwa  Sokoni mwaka 2012.

42.    Kwa sasa, Mbolea ya Minjingu Mazao inatumika katika Mikoa ya Iringa, Ruvuma, Rukwa, Mbeya, Njombe, Katavi, Kigoma na Morogoro. Aidha, kuna mikoa mingine ambako mbolea hii imepelekwa pamoja na mbolea nyingine kwa ajili ya Wakulima wenyewe kufanya maamuzi ya kuchagua.

Mheshimiwa Spika
43.    Matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao katika mwaka 2012/2013 yamewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa mahindi, mpunga na alizeti kwa ekari hususan katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini. Changamoto kubwa ni elimu juu ya matumizi sahihi ya Mbolea hiyo kwenye baadhi ya maeneo.

44.    Katika kutatua changamoto hii, Wizara inashirikiana na Mmiliki wa Kiwanda cha Mbolea cha Minjingu kuendesha mashamba darasa katika Wilaya mbalimbali Nchini.  Vilevile, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo, inaendelea kufanya utafiti katika maeneno mbalimbali ya Nchi ili kuboresha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo katika aina mbalimbali za udongo (site specific validation trials). 

45.    Changamoto zinazohusiana na Mbolea ya Minjingu katika Wilaya ya Mbozi zitaangaliwa kwa namna yake. Kitendo hicho ni cha udanganyifu kwani Mbolea ya aina nyingine ni bei kubwa ikilinganishwa na ya Minjingu Mazao. Kutokana na kitendo hicho kuwa kinyume na Sheria ya Mbolea ya 2009, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea kwa kushirikiana na Wakaguzi wa mbolea wa Wilaya ya Mbozi ilimkamata Wakala husika na kumchukulia hatua za kisheria. Naagiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya kuchunguza mbolea inayopelekwa katika maeneo yao isije ikachakachuliwa.

Mheshimiwa Spika,
46.    Kwa kuzingatia Changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mbolea ya Minjingu katika maeneo mbalimbali Nchini Serikali itaendelea kuzitafutia ufumbuzi kwa kuchukua hatua zifuatazo:
(a)    Kutoa elimu kwa Wakulima kuhusu namna bora ya kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao kuongeza uzalishaji wa mazao kwa kuzingatia ushauri wa kitaalam kuhusu aina ya udongo na mazao yanayofaa kwa mbolea hiyo. Vilevile, kuwaelimisha Wananchi kuhusu ubora wa Mbolea ya Minjingu Mazao ikilinganishwa na Mbolea za aina nyingine hasa kutokana na virutubisho vilivyoongezwa katika mbolea.

(b)    Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea imeagizwa kufuatilia na kufanya uchunguzi wa madai ya Wakulima kuhusu changamoto za matumizi ya mbolea ya Minjingu Mazao hasa katika Wilaya ya Mbozi na sehemu nyingine zenye matatizo ya matumizi ya mbolea hiyo Nchini.

(c)    Naomba kuiagiza Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuendelea kushirikiana na Wadau kufanya utafiti katika maeneo mbalimbali Nchini. Kutokana na utafiti huo itoe ushauri na mwongozo kwa Wakulima wote Nchini kuhusu njia sahihi za kutumia Mbolea ya Minjingu Mazao katika aina mbalimbali za udongo na mazao yanayofaa kulimwa. Lengo ni kuongeza tija katika uzalishaji wa mazao ya kilimo kwa eneo.  Kwa Wilaya ya Mbozi Wizara itoe mwongozo kuhusu nini kifanyike kwa sasa wakati hatua za utafiti na uchunguzi wa matumizi sahihi ya Mbolea hiyo zinaendelea. 

(g)    Uzalishaji na Ununuzi wa Mazao ya Biashara

Mheshimiwa Spika,

47.    Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na Changamoto mbalimbali za uzalishaji na ununuzi wa baadhi ya mazao ya biashara hapa Nchini ikiwemo Kilimo cha zao la Pamba, Korosho, Tumbaku na Kahawa. Kwa kuzingatia ufinyu wa muda, leo naomba mniruhusu nizungumzie kidogo kuhusu kilimo cha mazao mawili ya Pamba na Korosho.

(h)    Uzalishaji na Ununuzi wa Zao la Pamba
Mheshimiwa Spika,
48.    Serikali inaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa Wakulima wa Pamba wanazalisha kwa tija  kwa kutumia mbegu bora, utumiaji wa pembejeo  (Viuadudu na Mbegu),  kutoa huduma za ugani kupitia Maafisa  wa Kilimo  katika Halmashauri za Wilaya na pia kuhamasisha Kilimo cha pamba kwa kushirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali ikiwemo Sekta Binafsi. 

49.    Katika kilimo hiki cha Pamba, Zana za kilimo zinazotumika kwa sasa ni majembe ya kukokotwa na wanyama kazi kwa ajili ya kulima nah ii ni dhahiri haiwezi kuongeza tija. Ttahakikisha tunatumia Zana za Kisasa.

(i)    Mkakati wa Wizara kupata masoko ya uhakika ya pamba

50.    Serikali pia inaendelea kuhakikisha kwamba pamba inaongezwa thamani hapa Nchini kwa kuhamasisha uwekezaji katika ujenzi wa viwanda vya nyuzi na nguo. Uwekezaji mpya unafanyika kwa kujenga kiwanda cha nyuzi na nguo cha Dahong Mkoani Shinyanga na pia Mradi mkubwa wa kuzalisha pamba, kuchambua, kutengeneza nyuzi, kutengeneza vitambaa na nguo unaotarajiwa kutekelezwa  na Kampuni ya Kijapani (NITORI) katika Wilaya ya Handeni. Kwa sasa mradi huo uko katika hatua ya umilikishwaji wa Ardhi.

51.    Vilevile, Serikali imeanzisha mafunzo ya Uhandisi na Ubunifu katika Viwanda vya Nyuzi na Nguo. Pia tumeanzisha kozi ya ubunifu wa mitindo katika mitaala ya VETA na Mafunzo ya Shahada ya uzamili katika “Textile” katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Lengo ni kuhakikisha kuwa kuna watalaamu wa kutosha katika mchakato wa kuongeza thamani ya pamba. 

(j)    Tofauti za ubora wa mbegu za pamba manyoya na De – linted
Mheshimiwa Spika,
52.    Sina shaka Watanzania wameshasikia kuwa kwa sasa tunazo aina mbili za mbegu za Pamba zinazotumika hapa Nchini.  Tunayo mbegu yetu ya asili ya Pamba Manyoya na Mbegu mpya na ya kisasa ya Pamba isiyo na manyoya (De-linted).  Aina hizi zinatofautiana sana kwa ubora na bei. Mbegu ya manyoa ina uotaji wa chini ya Asilimia 50 wakati ile ya De –linted ni zaidi ya Asilimia 90. Mbegu ya manyoya hutumika nyingi kwa eneo (kilo 25 kwa Ekari), wakati De – linted ni kilo 6 tu kwa Ekari, sawa na Shilingi 7,200 kwa Ekari kwa bei ya Shilingi 1,200 kwa kilo. Mbegu ya manyoya ina tija ndogo (inazalisha kati ya kilo 250 na 300 kwa Ekari) ikilinganishwa ya mbegu ya De-linted inayozalisha Kilo 450 – 1200 kwa Ekari. Mbegu ya manyoya ina uwiano mdogo wa pamba nyuzi (Asilimia 33) ikilinganishwa na mbegu De-linted ambayo uwiano wake ni  Asilimia 36.

(k)    Jitihada za Wizara kupunguza bei ya mbegu bora
Mheshimiwa Spika,
53.    Ili kuwawezesha Wakulima kutumia mbegu bora (de-linted) Serikali imetoa ruzuku ya Shilingi Billioni 4.8 ili kufanya mbegu hiyo ipatikane kwa Shilingi 600 kwa kilo kwa mkulima badala ya Shilingi 1,200 kwa kilo iliyotumika mwaka 2012/2013.

54.    Serikali pia inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kutoa elimu kwa wakulima wa pamba kuhusu mbegu bora. Kwa mfano, Viongozi wa maeneo yanayolima pamba (Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na baadhi ya Madiwani)  wamepelekwa katika kiwanda cha kuchakata mbegu bora  za Pamba cha Kampuni ya Quton  ili kupata maelezo na kujionea hali ya utendaji wa mbegu bora katika kilimo. 

55.    Kupitia programu ya kuendeleza zao la pamba wakulima wawezeshaji (Lead Farmers) 3000 wa vikundi vya Kilimo cha Mkataba wanaendelea kupewa mafunzo ya kilimo bora na matumizi ya mbegu bora ili watumike kupeleka elimu hii kwa wakulima wenzao.

Mheshimiwa Spika,
56.    Katika msimu huu wa Kilimo wa 2013/14, Serikali imejipanga kusimamia utekelezaji wa Kilimo cha Mkataba kwa lengo la kuleta ufanisi katika Kilimo cha Pamba Nchini. Hatua hii inahusisha pia  kutoa elimu ya kutosha na  kushirikisha kwa karibu  Wadau katika  kuzipatia ufumbuzi changamoto zilizopo kwenye utaratibu mzima wa kilimo hicho ambacho kina manufaa makubwa iwapo kitaeleweka na kutekelezwa vyema kwa misingi ya haki miongoni wa wadau. Baadhi ya manufaa hayo ni:
(i)    Uhakika wa upatikanaji wa pembejeo kwa mkulima kwa mkopo. 
(ii)    Kuongeza tija kutokana na kupata pembejeo na huduma za ugani. 
(iii)    Kuongeza ubora wa pamba kutokana  na matumizi makubwa ya pembejeo na huduma za  ugani pamoja na vikundi kutumika kama Mawakala wa kununua Pamba ya wanachama wake hivyo kusimamia ubora
(iv)    Uhakika  wa soko la pamba ya mkulima 
(v)    Kupunguza wizi kupitia mizani ya mawakala 
(vi)    Wakulima kupata teknolojia kupitia uwekezaji
(vii)    Kujenga na kuimarisha mfumo wa Ushirika kupitia vikundi vya wakulima.

(l)    Elimu ya kilimo cha mkataba kwa wakulima
Mheshimiwa Spika,
57.     Kupitia programu ya kuendeleza zao la pamba, wakulima Wawezeshaji zaidi ya 3,000 wamekwisha pokea mafunzo ya kilimo cha Mkataba wanao tumika kupeleka elimu hii kwa vikundi vya wakulima. Wagani wa Halmashauri wapatao 560 wameshapata mafunzo haya.  Chini ya Mpango huu kila mgani anaweza kuhudumia vikundi hadi 20.

58.    Napenda kuwaagiza Viongozi na Wataalamu wa Kilimo waendelee kutoa elimu ya matumizi na faida ya mbegu bora za De-linted au mbegu zisizokuwa na manyoya kwa Wakulima wa Pamba Nchini.  Aidha,  mashamba darasa yatumike ipasavyo kuonesha tija inayotokana na aina hiyo ya mbegu za Pamba inapolinganishwa na mbegu zenye manyoya.  Vilevile, Viongozi na Wataalamu wa Kilimo waendelee kuwakumbusha Wakulima wa Pamba na Watanzania kuwa utaratibu mpya wa Kilimo cha Mkataba una manufaa mengi na makubwa.  Tuendelee kuwashawishi Wakulima kujiunga na Kilimo cha Mkataba bila kuwashurutisha isipokuwa tuwape elimu hasa kupitia mashamba darasa.  Wale watakaoshawishika kuingia katika utaratibu huu wasaidiwe kwa kila hali ili wanufaike na kilimo hicho huku wakisaidia kutoa elimu kwa Wakulima wengine ili wajiunge na aina hii ya kilimo. Ni matumaini yangu ndani ya muda mfupi Wakulima watafahamu faida ya kilimo cha mkataba.

(m)    Zao la Korosho

Mheshimiwa Spika,
59.    Kuhusu Zao la Korosho, azma ya Serikali ni kuimarisha Viwanda vya Korosho na kufufua vile vilivyopobinafsishwa ili viweze kusaidia kukuza Soko kwa wakulima wa Korosho. Ili kutekeleza azma hiyo, Serikali imefanya tathmini na kubaini kuwa Wawekezaji wengi katika Viwanda vya Korosho vilivyobinafsishwa wameshindwa kutekeleza Mikataba ya Ubinafsishaji wa viwanda hivyo kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo ukosefu wa fedha za uendeshaji, ukosefu wa nishati ya uhakika na Viwanda kutumia teknolojia zilizopitwa na wakati. Ili kukabiliana na hali hiyo, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kwa kushirikiana na Shirika Hodhi la Mali za Mashirika ya Umma (CHC) pamoja na Wadau wengine inaandaa mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya Wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda hivyo. Dhamira ya Serikali ni kwamba Mwekezaji ambaye ameshindwa kuendeleza kiwanda alichonunua kwa kuzingatia Makubaliano ya ununuzi na Serikali, mali hiyo irudishwe Serikalini na ifanyiwe tathmini na itangazwe upya ili kupata Wawekezaji mahiri na wenye nia thabiti ya kuendeleza Viwanda husika. 

Mheshimiwa Spika,
60.    Sambamba na hatua hiyo, Bodi ya Korosho Tanzania imeandaa Mpango wa Ubanguaji wa miaka mitatu kuanzia mwaka 2012/2013 ambao umelenga kuwasaidia wabanguaji wadogo na wa kati kuendesha shughuli za ubanguaji kwa ufanisi kwa kuwapatia mafunzo, vifaa vya kubangulia, na kuwatafutia masoko ya ndani, masoko ya kanda na masoko ya nje;

61.    Hatua iliyofikiwa kwa sasa ni kwamba, Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Zao la Korosho kwa kushirikiana na Bodi ya Korosho Tanzania umetenga fedha kwa ajili ya kujenga viwanda vitatu katika Mikoa ya Ruvuma, Mtwara, na Pwani kwa ajili ya kuwawezesha Wabanguaji wadogo na wa kati kumalizia baadhi ya hatua za ubanguaji katika viwanda hivyo kwa ajili ya kukidhi matakwa ya masoko makubwa ya korosho duniani.

Mheshimiwa Spika,
62.    Ili kuboresha kilimo cha Korosho, katika mwaka 2013/2014, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya madawa kutoa huduma za ugani na kuhamasisha wakulima wahudumie mikorosho na kupuliza madawa mapema.

Mheshimiwa Spika,
63.    Kuhusu ununuzi wa Korosho, katika msimu huu wa 2013/2014 ununuzi wa Korosho utaendelea kwa kutumia mfumo wa Stakabadhi za mazao Ghalani. Ukusanyaji wa Korosho kutoka kwa wakulima umeanza katika maeneo mbalimbali Nchini. Kwa mfano, katika Mkoa wa Mtwara, mnada wa kwanza wa Korosho ulianza tarehe 25 Oktoba, 2013 ambapo ulihusisha Vyama vya Msingi vya Mkoa wa Mtwara. Korosho zote zilizokuwa zimekusanywa na kutangazwa katika kila mnada zilinunuliwa. Bei ya Korosho katika Mnada wa kwanza ilikuwa kati ya Shilingi 1,402/= na 1,520/=  kwa kilo ikilinganishwa na bei dira ya Shilingi 1,000/= kwa kilo. Mnada uliofuatia bei ziliongezeka na kuwa kati ya Shilingi 1,481/= na 1,570/= kwa kilo.

Mheshimiwa Spika,
64.    Kwa upande wa Mkoa wa Lindi, Vyama vya Msingi vilivyobaki chini ya ILULU vilifanya Mnada wa kwanza tarehe 2 Novemba, 2013 ambapo jumla ya Tani 783.593 ziliuzwa. Vyama vingine 51 vya kutoka Wilaya ya Ruangwa, Nachingwea na Liwale ambavyo vilijiondoa kutoka usimamizi wa Chama Kikuu cha ILULU vitafanya mnada baada ya taratibu za kupata Kamati itakayowasimamia zitakapokamilika. Vyama hivyo vimeomba kufanyiwa Minada yake katika Wilaya ya Nachingwea ambako ndiko walikoweka Ofisi yao.

Mheshimiwa Spika,
65.    Kwa upande wa Wilaya ya Tunduru, bado haijapata mkopo mpaka sasa na juhudi za kufuatilia zinaendelea. Taarifa kutoka Benki ya NMB inaonyesha kuwa kuna uwezekano mkubwa wa Vyama vya Msingi vya TAMCU kupata mkopo msimu huu kwani deni ambalo TAMCU walikuwa wanadaiwa na Benki hiyo ya NMB limelipwa na Serikali.

Mheshimiwa Spika,
66.    Kwa upande wa Mkoa wa Pwani, uwezekano wa Vyama vilivyo chini ya Chama Kikuu cha Coast Region Cooperative Union (CORECU) kupata Mkopo ni mdogo kutokana na kudaiwa fedha nyingi zaidi ya Shilingi Bilioni 7 za msimu wa mwaka 2010/2011. Serikali imefanya Ukaguzi Maalum katika Vyama hivyo na kubaini kwamba madeni hayo kwa kiwango kikubwa yamesababishwa na ubadhirifu wa Viongozi na Watendaji wa Vyama hivyo. Hivyo, kupitia Ofisi ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika hatua za kisheria zimechukuliwa ikiwa ni pamoja na kuwataka wahusika wa ubadhirifu huo kufidia hasara hiyo. Kwa upande mwingine, Wahusika wamekata rufaa, lakini Mamlaka yenye dhamana imezitupilia mbali rufaa hizo zote 434, na kuwataka Wahusika walipe kiasi cha fedha kinachodaiwa na Vyama vyao. Kutokana na hali hiyo, Wakulima wa Mkoa wa Pwani wanashauriwa kupeleka mavuno ya Korosho katika maghala yaliyoteuliwa. Minada ya Korosho itafanyika katika maghala hayo na wakulima watalipwa mara moja baada ya minada kufanyika.

Mheshimiwa Spika,
67.    Kutokana na jitihada za Serikali zinazoendelea natoa wito kwa Bodi ya Korosho na Wakuu wa Mikoa husika kuendelea kusimamia kikamilifu taratibu wa ununuzi wa Korosho ili kuhakikisha kwamba Wakulima wanauza Korosho zao walizovuna na kulipwa malipo yao halali kwa wakati.

(n)    Hali ya mwenendo wa Mvua za vuli mwaka 2013 na athari kwa mazao ya vuli

Mheshimiwa Spika,
68.    Taarifa ya utabiri wa mwelekeo wa hali ya hewa hususan mvua katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2013 iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini inaonesha kuwa mvua za vuli zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Kaskazini mwa Morogoro, Kilimanjaro, Arusha, Manyara na baadhi ya maeneo katika mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga Kagera, Geita na Mara. Pamoja na kwamba mvua za msimu wa vuli zimechelewa kuanza katika maeneo mengi ambayo yalitarajiwa kupata mvua za vuli, mvua hizi hazitarajiwi kuwa na mtawanyiko wa kuridhisha.

(o)    Athari za mvua za vuli zinazonyesha chini ya Wastani

Mheshimiwa Spika,
69.    Kutokana na utabiri huo wa Hali ya Hewa, tathmini ya awali iliyofanyika katika maeneo yaliyotarajiwa kupata mvua za vuli inaonesha kuwa:
i.    Hali ya mazao hasa katika Nyanda za juu Kaskazini na ukanda wa Pwani Kaskazini si ya kuridhisha,

ii.    Mategemeo ya mavuno ya vuli ni kidogo isipokuwa katika baadhi ya maeneo ya ukanda wa Ziwa Viktoria hususan katika Mikoa ya Kagera na Geita ambayo yamepata mvua za wastani hadi chini ya wastani,

iii.    Mchango wa mavuno ya vuli ambao ni kati ya Asilimia 28-30 ya Chakula kinachozalishwa katika maeneo yanayopata mvua hizo au Asilimia 18 Kitaifa hauwezi kufikiwa katika hali hii ya mvua.

iv.    Hali hii inaashiria kuwa kutakuwepo na upungufu wa Chakula katika maeneo hayo niliyotaja hapo juu.

Mheshimiwa Spika,
70.    Kutokana na hali hii, natoa wito kwa Wakulima katika maeneo haya kuzingatia ushauri wa kupanda mazao yanayostahimili ukame na yanayokomaa kwa muda mfupi. Wakuu wa Mikoa na Wilaya katika Halmashauri husika wasimamie suala hili kwa ukamilifu; ili kuepusha upungufu wa Chakula unaotarajiwa. 

VI:    NISHATI

(a)    Kuongezeka kwa upatikanaji wa Nishati Vijijni (Miradi ya REA) na hali iliyofikiwa

Mheshimiwa Spika,
71.    Wakati wa Kuhitimisha Mkutano wa 12 wa Bunge nilieleza Mikakati ya Serikali katika kueneza umeme Vijijini na matarajio ya baadaye. Napenda kulieleza Bunge lako Tukufu kwamba tumeweza kupiga hatua katika baadhi ya maeneo katika kuelekea kwenye malengo tuliyojiwekea.  Tayari Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ulitangaza zabuni mwezi Desemba 2012 kwa ajili ya kuwapata Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini na kujenga vituo vya kupoozea umeme. Baada ya tathmini kufanyika, zabuni 15 za kupeleka umeme Vijijini zilipata Wakandarasi. Mikoa ambayo  ilipata  Wakandarasi  katika  awamu  hiyo  ni  pamoja  na Arusha,  Dodoma,  Iringa, Katavi,  Kilimanjaro, Mara, Mtwara, Mwanza, Njombe, Ruvuma, Shinyanga, Simiyu, Singida na Tabora. Aidha  Wakandarasi   kwa  ajili  ya  ujenzi  wa  vituo  vya  kupozea umeme vya msongo wa Kilovoti 11 na 33 vya Ngara, Kibondo, Kasulu, Kigoma,  Tunduru  na  Mbinga  walipatikana.  Kwa sasa Wakala unaendelea na kulipa malipo ya awali (advance payments) na Wakandarasi wanaendelea na ukamilishaji wa taratibu za kuanza kazi.  Miradi hii yenye thamani ya Shilingi Bilioni 430.82 inatarajiwa kukamilika mwezi Juni,  2015.

Mheshimiwa Spika,
72.     Mwezi  Mei,  2013  zabuni nyingine  10  ya Miradi yenye thamani ya Shilingi Bilioni 450 zilitangazwa  kwa  ajili  yakuwapata  Wakandarasi wa kupeleka umeme Vijijini katika  Mikoa ya  Geita,  Kagera,  Kigoma, Lindi,  Manyara, Mbeya, Morogoro, Pwani,  Rukwa na Tanga. Kwa sasa tathmini ya zabuni hizo inaendelea. Inatarajiwa kwamba Wakandarasi kutokana na Tathmini hiyo watajulikana ifikapo tarehe 15 Novemba, 2013.

  (b)     Suala la Fidia, Sera; na Miongozo ya usambazaji Umeme Vijijini:

Mheshimiwa Spika 
73.    Ili kuharakisha maendeleo ya upatikanaji wa Nishati Vijijini, suala la  Wananchi kuchangia nguvu kazi na kutoa njia na maeneo ya kupitisha nyaya za umeme  bila  fidia  pale  inapowezekana limekuwa likisititizwa na Serikali kutokana na ufinyu wa bajeti. Upo ukweli kwamba, Miradi mingi imechelewa kutekelezwa kutokana na Wananchi kudai fidia ya miti na mazao ya msimu yanayokutwa kwenye njia ya umeme.  Kwa mfano miradi ya Awamu ya Kwanza katika Mkoa wa Pwani imechelewa kuanza na kukamilishwa kutokana na Wananchi kudai fidia ilipwe kwanza ndio ujenzi uendelee. Pia, kwa sasa ujenzi umesimama katika maeneo ya Bungu-Nyamisati na Kisiwa cha Mafia kutokana na Wananchi kudai fidia kwanza. 

Mheshimiwa Spika, 
74.    Ni kweli kwamba kulingana na Sheria zilizopo kama katika njia ya kupitisha umeme yapo mazao yanayostahili kulipwa fidia. Hata hivyo kutokana na bajeti finyu Wakala wa Nishati Vijijni unashindwa kutoa fidia inayohitajika na kuona ni bora wale wanaojitolea maeneo yao wapelekewe umeme haraka kuliko kusubiri bajeti kwa ajili ya fidia. Serikali inatoa rai kwa Viongozi na Wananchi kuona umuhimu wa kujitolea maeneo yao ili waweze kupata huduma hii muhimu mapema. Nawaomba Waheshimiwa Wabunge tushirikiane katika kuwahamasisha Wananchi katika maeneo yetu kuhusu umuhimu wa kupata umeme mapema kwa maendeleo ya maeneo yetu.

(c) Utekelezaji wa Ujenzi wa Bomba la Gesi Asilia kutoka   Mtwara hadi Dar es Salaam

Mheshimiwa Spika, 
75.    Shughuli za ujenzi wa Bomba la Gesi kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam zinaendelea vizuri. Mpaka sasa usafishaji wa njia ya kulaza bomba unaendelea na tayari Kilometa 484.17 kati ya Kilometa 517 zimekamilika. Aidha jumla ya mabomba 20,491 yanayotosheleza kulazwa umbali wa Kilometa 243.8 yamekwishawasili Nchini. Kazi ya kuchimba mtaro, kuyapanga mabomba katika mstari mmoja kwenye mkuza na kuyaunganisha pamoja kwa kuchomelea inaendelea na hadi sasa Kilometa 124.3 zimeshaunganishwa. Kazi zinazoendelea ni ujenzi wa kambi, nyumba za wafanyakazi katika maeneo ya Songo Songo na Madimba, pamoja na maandalizi ya ujenzi wa mitambo ya kusafirishia Gesi Asilia. Tutaendelea kutoa taarifa ya hatua iliyofikiwa ya utekelezaji wa Mradi huu muhimu kwa Taifa letu.

76.    Aidha, katika kuhakikisha kwamba miradi hii inatekelezwa na kuleta manufaa katika Nchi yetu, ninayo furaha kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa, Serikali ilipitisha Sera ya Gesi Asilia tangu tarehe 10 Oktoba 2013, Utaratibu wa kuichapisha sera hiyo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza unaendelea. Vilevile Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imeandaa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Sera ya Gesi na imeanza kutayarisha Rasimu ya Sheria ya Gesi. Ni matumaini yangu kwamba vitu vyote hivi vikikamilika Sekta ya Gesi Asilia itaimarika.

VII:    MIFUGO

(a)    Operesheni Ondoa Mifugo Katika Maeneo Mbalimbali Nchini

Mheshimiwa Spika,
77.    Kwa muda mrefu sasa maeneo mbalimbali hapa Nchini yamekuwa yakikumbwa na migogoro inayotokana na matumizi ya Ardhi hususan kwa Wafugaji wanaohama kutoka maeneo yaliyokatazwa kisheria kwenda eneo lingine pasipo na maandalizi ya kutosha ya kuwapokea. Utafiti unaonesha kuwa, migogoro ya ardhi hapa Nchini ina sura nne:

Moja:    Migogoro kati ya Wakulima na Wafugaji, 

Pili:    Migogoro kati ya Wananchi na Wawekezaji,

Tatu:    Migogoro kati ya Wananchi na Serikali, na 

Nne:    Migogoro kati ya Mamlaka moja na Mamlaka nyingine ndani ya Serikali inayotokana na migongano ya kimaslahi. 

Mheshimiwa Spika, 
78.    Kuna ukweli kwamba, kuongezeka kwa idadi ya Watu na kuongezeka kwa matumizi ya ardhi kutaendelea kuongeza kasi na vipaumbele katika kugawa maeneo yaliyoko wazi. Hali hii imeanza kuonekana katika maeneo ya Wafugaji ambayo yameendelea kupungua siku hadi siku. Aidha, shughuli za kilimo, maendeleo ya makazi, na matumizi mengine ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa Vijiji kunakotokana na ongezeko la idadi ya watu kumeendelea kupunguza eneo la malisho. 

Mheshimiwa Spika, 
79.    Kuna ukweli pia kwamba, mabadiliko ya tabianchi na kuongezeka kwa mifugo katika maeneo ya Nchi kwa ajili ya kutafuta malisho na maji kumeendelea kuchangia migogoro mingi kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi. Kati ya mwaka 2005 na sasa, tumeshuhudia uhamiaji wa mifugo kutoka mikoa ya Kaskazini na Kanda ya Ziwa kwenda katika Mikoa ya Kusini na Mashariki mwa Nchi. Uhamiaji huo licha ya kusababisha migogoro kati ya watumiaji wengine pia imesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira kwenye maeneo ya vyanzo vya maji na hifadhi za Taifa. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na hifadhi za Wanyama pori za Burigi, Maswa na Meatu, Bonde la Usangu na Bonde la Kilombero.

Mheshimiwa Spika, 
80.    Ni matumaini yangu kwamba, maadam suala hili limepewa umuhimu na Bunge lako Tukufu na hivyo kuunda Kamati ya kufuatilia migogoro hii, ni dhahiri tutapata ufumbuzi wa kudumu katika tatizo hili. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla wanaotoka katika maeneo yenye migogoro inayotokana na Wafugaji na Wakulima kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa muhimu kwa Kamati iliyoundwa ili kulisaidia Taifa katika kutatua migogoro hii. 

VIII:     HALI YA ULINZI NA USALAMA NCHINI.

Mheshimiwa Spika,
81.    Kwa ujumla hali ya Ulinzi na Usalama Nchini imeendelea kuwa shwari, isipokuwa katika maeneo machache ambako kulijitokeza vitendo vinavyoashiria kuwepo kwa vikundi vya uhalifu na ujambazi.  Serikali kupitia Jeshi la Polisi imeendelea kujipanga kukabiliana na matishio mbalimbali ya kiusalama ikiwemo ugaidi. Tukio lililotokea Nchini Kenya hivi karibuni na matukio ya kukamatwa kwa Vijana 12 kule Mtwara na lile lililotokea Wilaya ya Kilindi Mkoani Tanga ambapo zaidi ya watuhumiwa 46 wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali yanaashiria kwamba ugaidi hauna mipaka unaweza kutokea katika Nchi yoyote.

Mheshimiwa Spika
82.    Katika kuhakikisha kuwa amani na utulivu vinaendelea kudumu Nchini, Serikali imejipanga katika maeneo hayo kama ifuatavyo:
(i)    Kuhakikisha Vikao vya Kamati za Ulinzi na Usalama vya Mitaa, Vijiji na Vitongoji vinafanyika mara kwa mara kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa katika kila Kata/Shehia kwa kuwashirikisha madiwani ili kujadili na kubaini kero mbalimbali na kuzitafutia ufumbuzi.

(ii)    Kufufua mpango wa Daftari la Wakazi na Wageni katika kila Mtaa/Kitongoji kwa Tanzania Bara na Zanzibar ili kila Kiongozi wa Mtaa, Kijiji na Kitongoji ajue Watu wanaoishi katika himaya yake. Zoezi hili litasaidia kuepuka tatizo la wageni wasiojulikana au wahamiaji haramu. Aidha kamati za Ulinzi na Usalama za Serikali za Mitaa na Vijiji zinahimizwa kutekeleza mkakati wa Halmashauri wa kuzuia uhalifu kwa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani, kwa kuzingatia Sheria ya Serikali za Mitaa na Sheria Ndogo zilizotungwa ili kuimarisha usalama katika Halmashauri  husika.

(iii)    Kuhimiza wafanyabiashara wasaidiane na vikundi vya ulinzi shirikishi/ulinzi jirani vilivyo kwenye maeneo jirani na biashara zao kama sehemu ya kuimarisha usalama wa maeneo yao ya biashara. Pia, kwa wafanyabishara wenye biashara kubwa zenye mikusanyiko ya Watu wengi wanaagizwa kufunga “CCTV Camera” na kuziunganisha kimtandao na “Control Room” ya Polisi ili kutoa msaada wa kuzuia na kutanzua mapema uhalifu wowote utakaojitokeza. 

(iv)    Kuendelea kuunda Zonal Task Force za Jeshi la Polisi katika kila Tarafa/Jimbo ili kukusanya taarifa za uhalifu na kufanya operesheni za kuzuia uhalifu katika kila Kata au Shehia zilizo ndani ya Tarafa husika. Kwa kufanya hiovyo tutaokoa maisha ya watu wengi.

(v)    Kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu mbinu mbalimbali za kuzuia na kupambana na uhalifu kwa kutumia vyombo mbalimbali vya habari, mihadhara, mikutano, maonesho na usambazaji wa machapisho na vipeperushi.

Mheshimiwa Spika,
83.    Jukumu la kuhakikisha Ulinzi na Usalama katika Nchi yetu ni letu sote.  Kila Mwananchi popote alipo anawajibika kushiriki kwa vitendo kwa kubaini vitendo vyovyote vya uhalifu katika sehemu za kazi, biashara na maeneo tunamoishi.  Wito wangu kwa Waheshimiwa Wabunge wote, ni kuwaomba tuwahimize Wananchi kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha Nchi yetu inadumu katika hali ya Amani na Utulivu.

IX:    HITIMISHO
Mheshimiwa Spika,
84.    Kwa kuhitimisha, naomba nitumie nafasi hii ya mwisho kuwashukuru wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu. Kipekee nikushukuru wewe Mheshimiwa Spika, pamoja na Naibu Spika kwa kutuongoza vizuri.  Niwashukuru Wenyeviti wa Bunge kwa kazi nzuri ya kuongoza vikao vya Bunge lako Tukufu.  Aidha, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kazi nzuri na kwa michango mbalimbali wakati wa Mkutano huu. Namshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi wake wote pamoja na Wataalam wote wa Serikali na Taasisi zake ikijumuisha Taasisi za Sekta Binafsi, kwa misaada ya Kitaalam na huduma mbalimbali za kufanikisha Mkutano huu. Niwashukuru pia Waandishi wa Habari kwa kazi nzuri walizofanya kuhakikisha kuwa taarifa za majadiliano na maamuzi mbalimbali ya hapa Bungeni zinawafikia Wananchi.  Niwashukuru Madereva kwa kazi nzuri waliofanya ya kuwasafirisha kwa usalama Waheshimiwa Wabunge,Viongozi mbalimbali, Wataalam na Wasaidizi wote walioshiriki katika Mkutano huu.

Mheshimiwa Spika,
85.    Nimalizie kwa kuwatakia wote safari njema mnaporejea kwenye maeneo yenu ya kazi na katika majimbo yenu. Baada ya kusema hayo, naomba sasa kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi tarehe 3 Desemba, 2013 saa 3:00 Asubuhi litakapokutana katika Mkutano wa 14 kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.

Mheshimiwa Spika,
86.    Naomba kutoa hoja.

POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment