BARAZA la Maadili ya Utumishi wa Umma limesikiliza shauri la mgawo wa
fedha za Escrow dhidi ya aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo
ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ambaye anadaiwa amekiuka Sheria ya
Maadili ya Utumishi wa Umma namba 12 (e) (1) ya mwaka 1995.
Kutokana na madai hayo, waziri huyo wa zamani wa Serikali ya awamu ya
nne, amefichua namna alivyotumia fedha za mgawo wa Escrow ikiwamo
kutumia Sh milioni 10 kwa ajili ya kununua mboga.
Profesa Tibaijuka alifikishwa mbele ya Baraza la Maadili jana jijini Dar
es Salaam, na kusomewa mashtaka dhidi yake na Mwanasheria wa baraza
hilo, Wema Winfred.
Mwanasheria huyo, alidai kuwa Profesa Tibaijuka anakabiliwa na mashtaka
matatu, ambayo ni kuomba fadhila za kiuchumi kinyume na sheria ya
maadili kifungu namba 6, kupokea fadhila za kiuchumi kinyume na sheria
hiyo na kuwa na mgogoro wa kimasilahi.
Alidai kuwa mshtakiwa huyo alikiuka maadili ya umma kwa kuomba
kuingiziwa fedha kiasi cha Sh bilioni 1.6 kutoka katika Kampuni ya VIP
Engineering and Marketing Tanzania Limited ambazo aliingiziwa kwenye
akaunti namba 001200102640201 iliyopo Benki ya Mkombozi, Tawi la St.
Joseph jijini Dar es Salaam.
Mwanasheria huyo alidai kuwa mshtakiwa kwa kutumia wadhifa wake,
alijinufaisha kifedha, hivyo baraza linamtaka kueleza bayana mwenendo
wake kabla ya hatua zaidi za kisheria hazijachukuliwa dhidi yake.
Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mbele ya baraza hilo, alisimama
mwanasheria wa Profesa Tibaijuka aliyejitambulisha kwa jina la Dk.
Rugemaleza Nshara na kupinga tuhuma zinazomkabili mteja wake kwa kudai
ameonewa katika shauri hilo.
Kutokana na maelezo ya wakili wa upande wa utetezi, Mwenyekiti wa
Baraza, Jaji Mstaafu Hamis Msumi, alimtaka mwanasheria huyo kuelewa kuwa
baraza hilo si mahakama ya kisheria, na kwamba taratibu zake
hazitofautiani na taratibu za kimahakama.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Msumi aliutaka upande wa walalamikaji ambao
ni Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoa ushahidi wao,
ambapo aliyekuwa wa kwanza kutoa maelezo yake ni Katibu Msaidizi Idara
ya Uongozi wa Siasa wa sekretarieti hiyo, Waziri Kipache (45) aliyedai
kuwa anamfahamu mlalamikiwa kuwa alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi na ni Mbunge wa Muleba Kusini.
Alisema baada ya kupata taarifa mbalimbali za kuwapo kwa baadhi ya
viongozi wa umma kutuhumiwa kupokea fedha kutoka Kampuni ya VIP kinyume
na maadili, alikutana na Tibaijuka na kumhoji kuhusu suala hilo.
“Baada ya taarifa hizo, tulifanya uchunguzi ili tuweze kujiridhisha kama
kanuni na taratibu za masharti ya uongozi wa umma yamezingatiwa katika
upokeaji wa fedha hizo.
“Tulibaini kuwa Aprili 4, mwaka 2012, Profesa Tibaijuka aliomba fedha
kwa mke wa mmiliki wa Kampuni ya VIP, James Rugemalila na maombi hayo
yaliwasilishwa kwa barua,” alisema Kipeche.
Shahidi huyo ambaye alitoa maelezo yake mbele ya jopo la viongozi wa
Baraza la Maadili akitimia dakika kumi, pia alitoa barua ya Profesa
Tibaijuka ya kuomba fedha hizo.
Alidai kuwa Profesa Tibaijuka akiwa mmoja wa wadhamini wa Bodi ya
Wakurugenzi wa Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust, pia ndiye
mmiliki wa Shule ya Kajumulo Alexandre iliyopo mkoani Kagera akiwa ni
meneja wa shule hiyo.
“Kwa mujibu wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma, hawaruhusiwi
kuomba fedha kwa masilahi ya kiuchumi, hivyo basi Profesa Tibaijuka
ametenda kosa hilo,” alisema Kipache.
Kutokana na maelezo hayo ya shahidi huyo, Jaji Msumi, aliutaka upande wa
utetezi kuwasilisha ushahidi mbele ya baraza kuhusu madai yake hayo.
Kwa kuwa ilikuwa imetimu saa 11: 45, Jaji Msumi aliahirisha shauri hilo
hadi mchana kwa kuwa tayari ulikuwa umefika muda wa mapumziko, huku
akimtaka Profesa Tibaijuka na timu yake wajipange kwa maelezo na
kuwasilisha vielelezo kutokana na tuhuma alizokuwa akituhumiwa.
Ilipotimu saa 6:30 mchana, shauri hilo liliendelea kwa Jaji Msumi
kumsimamisha Profesa Tibaijuka atoe ushahidi wake mwenyewe na aeleze
namna miamala ya fedha ilivyofanyika.
UTETEZI WA TIBAIJUKA
Akizungumza baada ya madai hayo kutolewa, Profesa Tibaijuka alipinga
ushahidi wa Kipeche na kudai kuwa uhusiano wake na taasisi hiyo ni kuwa
yeye ni miongoni mwa waanzilishi akiwa na mumewe.
Alisema uamuzi wa kuanzisha shule hiyo, ulitokana na kuona umuhimu wa
kupigania elimu ya mtoto wa kike ili aweze kupata fursa ya kuendelezwa
kielimu, kiuchumi na kijamii.
Alisema kabla ya hapo alifanya utafiti mwaka 1994 na 1995 ambapo ripoti
yake inaonyesha kuwa mtoto wa kike hana thamani kwenye jamii, ndiyo
maana anashindwa kupatiwa haki ya kupata elimu katika ngazi mbalimbali.
Profesa Tibaijuka alisema kutokana na utafiti huo, ndipo akafikia uamuzi
wa kuanzisha taasisi hiyo ili aweze kuwasaidia watoto hao, hasa wale
wenye vipaji na wanaotoka katika mazingira magumu.
“Nikiwa mkereketwa wa Umoja wa Mataifa (UN), sielewi masilahi gani
nimepata kupitia fedha hizi, ikiwa shughuli za ‘fund rising’ sijaanza
leo, nimeisomea kabisa nchini Marekani kwa fedha za Serikali mwaka 1980.
“Hata nilipokuwa UN nilikuwa nikifanya hivyo na aliyekuwa Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa wakati huo, Kofii Annan, aliniruhsu na kunipongeza
kuwa ninachokifanya ni muhimu kwa jamii,” alisema Profesa Tibaijuka.
Kutokana na maelezo hayo, aliomba apewe mwongozo nini maana ya kukiuka
maadili ya utumishi wa umma, huku akidai kuwa amedhalilishwa,
amefedheheshwa na kwamba anaonekana ni tapeli katika jamii, jambo ambalo
limemsababishia kukosa amani katika nafsi yake.
“Nimeshangaa kuitwa kwenye baraza hili na kuambiwa kuwa nimekiuka
maadili ya utumishi wa umma, kwani maadili maana yake nini? Kufanya
shughuli za kuisadia jamii ni kukiuka maadili?
“Ninaomba mwenyekiti unisaidie katika hili ili haki itendeke dhidi
yangu, maana nimeanza kuhukumiwa tangu niko bungeni bila hata ya kupewa
nafasi ya kusikilizwa, nilijaribu kumwomba Mheshimiwa Spika Anne Makinda
ili aweze kunisikiliza, lakini alikataa,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo, alilishukuru baraza hilo kumwita na
kumsikiliza kwa sababu hajawahi kupata haki yoyote ya kusikilizwa, ndiyo
maana alikubali kwenda mwenyewe ili aweze kusema yanayomsibu.
Baada ya maelezo hayo ya Profesa Tibaijuka, walisimama wanasheria watatu
wakiongozwa na Getrude Cyriacus, ambaye alikuwa wa kwanza kumuhoji
kuhusu malalamiko dhidi yake kuwa aliomba fedha kwa Rugemalila na
kuzipokea kupitia Kampuni ya VIP hali ya kuwa maadili hayaruhusu.
Swali hilo lilionekana kuwa mwiba kwa Profesa Tibaijuka, ambaye muda
wote alikuwa akisikiliza kwa makini, ambapo alikiri kuomba fedha hizo,
lakini si kwa masilahi yake binafsi, bali ni kwa ajili ya Taasisi ya
Barbro Johannson Girls Trust.
Wakili Getrude: Wakati unapewa fedha hizo ulikuwa na cheo gani, ni waziri na mbunge au la.
Profesa Tibaijuka: Sioni mantiki ya swali hilo.
Baada ya kujibu, alimwangalia wakili wake, Dk. Nshala ambaye alimtaka
alijibu swali hilo, ndipo Tibaijuka alisema kipindi anapokea fedha hizo
alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa
Muleba Kusini.
Mwanasheria Hassan Mayunga alimhoji Profesa Tibaijuka kwanini alifanya
haraka kutoa fedha hizo zilizoingizwa kwenye akaunti yake katiba Benki
ya Mkombozi na kuzitumia katika kazi zake binafsi.
Alisema fedha hizo ziliingizwa tarehe 12 mwaka 2014 na kuanza kufanya
miamala binafsi tarehe 14 ambapo Sh milioni mbili alizitumia kununua
hisa Makongo Parish.
Profesa Tibaijuka alisema baada ya hapo alitoa Sh 400,000 na kununua
hisa Kijiwe Parish na siku hiyohiyo alitoa Sh milioni 10 ambazo hazina
maelezo sahihi.
“Sh milioni 10 nilitoa kwa ajili ya kununua mboga kwa sababu fedha hizo ni zangu.
“Nashangaa kuambiwa nimevunja maadili, kwanza fedha hizi ni ndogo japo ni hela, lakini mimi sina shida na fedha hizi.
“Mimi ni mstaafu wa miaka mingi, nina pensheni ya kila mwezi, sina shida
na fedha hizo ndiyo maana hata hizo fedha zilizobaki kwenye akaunti
hiyo sijaenda kuziangalia kwa sababu sina shida za hivyo,” alisema.
Kabla ya Tibaijuka kuanza kutoa maelezo yake mbele ya baraza hilo,
Wakili wa upande wa utetezi, Dk. Rugemaleza Nshala, alisimama na
kumuhoji shahidi Kipache na kuzua mabishano.
Dk. Nshala: Kwenye sheria ya maadili wapi inaonyesha kiongozi wa umma kupewa zawadi ni dhambi?
Kipache: Si dhambi ila kisheria inatakiwa isizidi Sh 50,000.
Dk. Nshala: Je, fedha alizopewa Tibaijuka ni zake au za taasisi?
Kipache: Ni za taasisi, lakini tatizo lililopo ni kwamba ameingiziwa
fedha katika akaunti yake binafsi na si akaunti ya taasisi na hapo ndiyo
amekiuka maadili.
Dk. Nshala: Je, kiongozi wa umma kuomba michango ya maendeleo kwa wadau
ni dhambi? Mbona Waziri Mkuu Pinda alikuwa mgeni rasmi kusaidia
kukusanya michango ya Taasisi ya Maajar Trust Fund. Je, alikiuka sheria
ya maadili?
Kipache: Waziri Mkuu alihamasisha kutoa michango, lakini fedha
zilizotolewa hazijaingia katika akaunti yake binafsi, tukio hilo ni
tofauti kwa sababu fedha za Tibaijuka aliingiza kwenye akaunti yake
binafsi.
Dk. Nshala: Kwanini hawajaenda kwenye bodi ya wadhamini kuuliza kama
fedha hizo zimetumikaje au kwenda mbali zaidi kwenye benki ya Mkombozi
kuulizia miamala?
Kipache: Hatukuona umuhimu wa kwenda kwa sababu waliokuwa na ‘statement’
ya benki ilionyesha miamala yote iliyofanyika kwa Tibaijuka, lakini pia
tulikwenda Rita kufanya uchunguzi ili kuweza kuangalia usajili wa
taasisi hii na wamiliki wake.
SHAHIDI WA TIBAIJUKA
Naye shahidi wa Profesa Tibaijuka ambaye ni Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini
wa Taasisi ya Barbro Johannson Girls Trust, Balozi Paul Rupia, alisema
fedha hizo zimetafutwa na Profesa Tibaijuka na kutoa taarifa kwenye bodi
hiyo kuwa kuna fedha zimeingia ambazo zinatakiwa kulipwa madeni.
Alisema bodi hiyo haijampa masharti yoyote ya kumaliza kulipa madeni
hayo na kwamba hawakuwa na sababu ya kumfuatilia kwa sababu walimwamini
kutokana na juhudi zake binafsi za kupata fedha hizo.
Katika shauri hilo lililoanza saa 3:00 asubuhi na kuendelea hadi saa
11:45 jioni, Profesa Tibaijuka alitoa ushahidi kwa zaidi ya saa tatu
kuanzia saa 6:30 mchana hadi saa 9:30 alasiri.
Shauri hilo limehairishwa hadi Machi 13, mwaka huu baada ya wakili wa
Profesa Tibaijuka kuomba hudhuru ya kwenda nchini Marekani kwa siku
kumi.
Jaji Msumi alikubali ombi hilo na kudai kuwa shauri hilo litaendelea
siku hiyo na kutolewa hukumu huku baraza hilo likiamua namna ya kujadili
shauri hilo, kwamba itaamuliwa kama liwe la uamuzi wa ndani au
hadharani.
Idadi kubwa ya watu walijitokeza katika Ukumbi wa Karimjee kusikiliza shauri hilo.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment