Tido Mhando:NDEREMO


Tido Mhando 


Kwa kipindi cha miaka mingi sana nilikuwa nikifanya kazi ya utangazaji wa radio. Nilianza mwaka 1969 pale Radio Tanzania Dar es Salaam, (RTD), baadaye nikaenda Kenya, halafu Uingereza na hatimaye nikarejea tena RTD inayofahamika kama TBC siku hizi.
Kwa kipindi cha miaka mingi sana nilikuwa nikifanya kazi ya utangazaji wa radio. Nilianza mwaka 1969 pale Radio Tanzania Dar es Salaam, (RTD), baadaye nikaenda Kenya, halafu Uingereza na hatimaye nikarejea tena RTD inayofahamika kama TBC siku hizi. Katika kipindi chote hiki niliona na kushuhudia mambo mengi ambayo sasa ninasimulia baadhi yake kwenye simulizi zangu hizi za kila Jumapili. Wiki jana, nilielezea jinsi tulivyorejea kutoka New Zealand, mwaka 1974 na timu ya wanamichezo wa Tanzania walioshiriki kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, lakini tayari nikaingia kwenye hekaheka za maandalizi ya harusi yangu iliyokuwa inafanyika mwishoni mwa Februari. Lakini ikiwa imebakia karibu saa 12 kwa harusi yenyewe kufungwa suti zetu za harusi mimi na mpambe wangu Robert Mwaimu (Bob), zilikuwa hazijamalizika kushonwa. Sasa endelea…
Ilikuwa ni majira kama ya saa 10 hivi siku ya Ijumaa yaani siku ya mkesha wa harusi, wakati Bob aliponipigia simu na kwa mara ya kwanza kabisa tukawa tumeanza kutaharuki kuhusu hali hii ya kuchelewa kushonwa kwa hizo suti zetu za mtindo wa Marien Ngouabi.
Bob alikuwa kazini kwake, Bendera Tatu, makao makuu ya Shirika la Bandari, nami nilikuwa pale RTD, Pugu Road na tukazungumza kwa muda kuhusu hali hii iliyokuwa imejitokeza na kututia wasiwasi.
Pamoja na kwamba kwa kweli tulikuwa wenyewe tumeichelewesha sana kazi ile, lakini yule fundi wetu wa Kizaire pale Magomeni alikuwa ametuhakikishia kuwa angekamilisha kila kitu baada ya siku mbili tu. Sasa mambo ndiyo hivyo yanaelekea kubaya na zaidi zaidi hatukuwa na suti nyingine zozote za kusema kama mambo yakiharibika tungezitumia, si unajua tena mambo ya vijana na suti suti, wapi na wapi! Tukaamua kumwondolea uvivu.
Tulikata shauri kukutana na kwenda Magomeni tukapige kambi huko hadi kieleweke. Hatukutaka kuumbuka kwa hiyo tukakubaliana tukutane baadaye jioni ile hata kama itakuwa tukazisubiri hapo hapo hadi usiku wa manane.
Nilifahamu ya kwamba nitakuwa nikiondoka ofisini baadaye siku hiyo ikiwa ni mara yangu ya mwisho nikiwa kama bachela, lakini nirejeapo nitakuwa mume wa mtu. Mume wa Binti Amos Mwaipopo, duu nikawa nawaza mengi. Nikamua kupita ofisi moja hadi nyingine kuwaaga washikaji.
Naam, naona nilifanya vyema kwani kumbe kulikuwa na wengine ambao pia walikuwa wakitafakari jinsi ya kuniaga rasmi kibinafsi, maana karibu wafanyakazi wote nilikuwa nimewaalika kuja kwenye sherehe yenyewe pale kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee.
Basi ofisi nyingine nilikuwa napatiwa mawaidha mazito, kwingine nikikumbatiwa na kuagwa kwa kumbatio la nguvu na kwingineko wengine ati walikuwa wanatokwa hata na machozi, nikajiuliza “kwani nilikuwa nakwenda kufa ama vipi si nilikuwa tu naingia hatua nyingine ya maisha?”
Lakini kulikuwa na wengine hata walinipatia zawadi maalumu zilizoambatana na kadi zenye maneno “Good Luck Boy. We acha tu, nikajua ya kwamba kumbe kuna washkaji wengine ambao hii harusi yangu ilikuwa imewagusa sana. Niliondoka baadaye taratibu ofisini pale na nilipofika kwenye lango kuu nikageuka nyuma na kujisemea “nitakaporejea tena hapa nitakuwa Mister Tido Mhando halisi.”
Kwa kuwa hii ilikuwa ni siku ya chesha nilipofika nyumbani Chang’ombe niliikuta nyumba imejaa furifuri. Wamefika wageni ambao wengine wengi nilikuwa sijakutana nao huko nyuma ingawaje wote walikuwa ndugu zangu wa karibu sana. Wengi wakitokea wilayani Muheza, Bonde.
Nadhani Bonde yote ilikuwepo pale maana kila nikipita kona hii nakumbana na huyu ananisalimu kwa hili, wengi wakinisemesha kwa Kibondei ingawaje lugha yenyewe haipandi hivyo, lakini kiasi nilikuwa nababaisha.
Mara nikiingia hapa utasikia “waona vihi tate” ama huyu “waambaze mwezetu” ama yule “soo uku mwaya” ilimradi ilikuwa hoihoi ya kwelikweli, nderemo ya kukata na shoka huku kelele na vifijo vya furaha vikisikika nyumba nzima “hache ugai, hache ugai” ndugu zangu hao wakishabikia na kufurahia kwa dhati kabisa kupata kwangu jiko.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment