JESHI la
Polisi limempa ulinzi wa siri Mbunge wa Kigoma Kaskazini,Zitto Kabwe
(CHADEMA) kama njia ya kumkinga asidhuriwe na maadui wake katika siasa.
Hatua
hiyo ya polisi imechukuliwa siku chache baada ya mwanasiasa huyo kijana
na mama yake mzazi, Shida Salum, kwa nyakati tofauti, kudai kuwa Zitto
amekuwa akiwindwa na watu ambao wamekuwa wakitishia uhai wa wake
kutokana na siasa zinazoendelea ndani ya Chadema.
Chanzo
cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi, kiliiambia RAI kuwa
uamuzi huo ulifikiwa katika kikao wiki iliyopita, baada ya jeshi hilo
kupata taarifa za tishio la kudhuriwa kwa kiongozi huyo kwa kile
kilichoelezwa kuwa tofauti baina yake na viongozi wenzake wa Chadema.
Kikao
hicho ambacho kiliwahusisha makamishna kutoka makao makuu ya jeshi hilo,
kilipitia kwa kina taarifa ya kutaka kudhuriwa kwa Zitto kwa
kutofautiana msimamo na viongozi wenzake ndani ya chama hicho.
"Kikao
kilifanyika Novemba 11 mwaka huu ambako pamoja na mambo mengine kimeweza
kujadili kwa kina kutaka kudhuriwa Zitto ... hivyo walitumwa makachero
wa jeshi la polisi waweze kubaini anapoishi.
"Wamefanya
kazi hii na sasa kiongozi huyo analindwa kuanzia nyumbani kwake Tabata.
Askari maalumu wamepewa kazi ya kuimarisha ulinzi nyumbani kwake hadi
katika nyendo zake," kilisema chanzo hicho ndani ya jeshi la polisi.
Zitto,
ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, kwa muda mrefu amekuwa
akitofautiana na viongozi wenzake hasa katika masuala ya taifa hali
inayofanya atafsiriwe kuwa anatumika kutaka kuivuruga Chadema.
RAI
ilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, Advera Senso kupata
uthibitisho wa uamuzi huo lakini alisema suala hilo liko mikononi mwa
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
"Kwa
jambo hili nakuomba mtafute Kamanda wa Mkoa husika, yeye anaweza kukupa
maelezo ya kina ya jambo hilo ndugu yangu au Kamanda wa Polisi Kanda
Maalum ya Dar es Salaam," alisema Senso.
KOVA
Alipotafutwa
jana, Kova alisema hawezi kukubali au kukata kwa sababu suala hilo liko
katika mamlaka ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Minangi.
"Siwezi kusema ndiyo au hapana, nakuomba umtafute kamanda wa mkoa husika atakupatia maelezo ya kina,"alisema Kamanda Kova.
KAMANDA WA ILALA
Kamanda
Minangi alipoulizwa jana kuhusiana na suala hilo, naye alimrushia mpira
Kova akisema ndiye pekee anayeweza kutoa ufafanuzi wa suala hilo.
"Jamani nawaomba suala hili mmtafute Kamanda Kova ndiye anayeweza kulitolea ufafanuzi,"alisema Kamanda Minangi.
Kwa muda
mrefu sasa, Zitto amekuwa akishutumiwa na viongozi wenzake wa ngazi za
juu katika Chadema akidaiwa kutengeneza ufa baina yake na wazito ndani
ya chama hicho tangu mwaka 2009.
Zitto
amekwisha kuwahi kutangaza uamuzi wa kutaka kuwania uenyekiti wa chama
hicho aweze kupambana na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.
Hata
hivyo baadaye alijiondoa kuwania nafasi hiyo baada ya wazee wa chama
hicho kuingilia kati na kumsihi atumie busara kutogombea.
Katika
siku za hivi karibuni, Zitto amejikuta akihusishwa na kile kinachotajwa
kuwa nyuma ya 'usaliti' unaodaiwa kufanywa na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa
wa Arusha aliyesimamishwa, Samson Mwigamba.
Hata
hivyo, Zitto alikanusha tuhuma hizo na kuwataka viongozi wenzake
kuelekeza nguvu kwa wanachama akisema malumbano hayatakijenga chama.
Mbali na hilo, kwa muda mrefu Zitto amekuwa na msuguano wa ndani na nje ya chama, hasa kutokana na misimamo yake.
Hivi
karibuni, Mbunge Arusha Godbless Lema (Chadema) aliibuka na kumtuhumu
Zitto kwa uamuzi wake wa kutochukua posho za vikao bungeni tofauti na
msimamo alioutoa mwaka 2011.
Msuguano
mwingine ni baina yake na vyama vya siasa kwa msimamo wake wa kutaka
vyama vyenye wabunge ambavyo vinapata ruzuku ya serikali, viwasilishe
ripoti ya ukaguzi wa hesabu zake kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
Zitto
ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) pia
aliwaonya viongozi wenzake kuacha propaganda kwa kulichukulia suala hilo
kuwa ni la siasa au lake binafsi.
Alisema anachokifanya ni kusimamia sheria kutokana na nafasi yake kama mwenyekiti wa PAC.
Vyama vya siasa vinatajwa kuchukua ruzuku ya Sh bilioni 67.7, lakini havijaanika mchanganuo wa matumizi yake.
ATUA POLISI
Katika
hatua nyingine, jana Zitto alisambaza ujumbe kwenye mtandao wake wa
jamii akisema amelazimka kwenda makao makuu ya jeshi la polisi kutoa
maelezo kwa kutishiwa kifo.
Katika
ujumbe huo alindika: "Nimetoka makao makuu ya upelelezi kuandika maelezo
kuhusu vitisho dhidi yangu, kufuatia hekaya inayoitwa ripoti ya siri ya
Zitto Kabwe.
"Chanzo
cha hekaya ya sasa kinabadilishwa kutoka makao makuu ya Chadema na kuwa
ni Usalama wa Taifa au Chama Cha Mapinduzi (CCM)".
Taarifa
hiyo ilisema wahusika wanaendelea kuhamisha chanzo, lakini wanaopaswa
kujua watasakwa, kukamatwa na kuburuzwa mahakamani.
"Nimewashtaki
kwa kunitishia maisha, ninawashtaki kwa kunichafua kwa tuhuma za uongo,
nafanya haya kwa lengo la kuhakikisha siasa za kuzushiana na kusambaza
uongo zinakuwa na gharama kubwa,"ilisema taarifa hiyo.
MSIMAMO WAKE
Mwanasiasa
huyo kijana ambaye amejipambanua kuwa mtetezi wa misingi ya utaifa,
raslimali za nchi, uchumi na masuala ya utawala bora ndani na nje ya
chama chake, alitoa msimamo wake kwa mara ya kwanza wiki iliyopita
alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara katika uwanja wa Kolimba wilayani
Kaliua, Mkoa wa Tabora.
"Katika
umri huu mdogo, nimepigwa mishale mingi ya siasa, mimi ni binadamu nina
damu, nikipigwa hii mishale damu inatoka, ninaumia, sasa nimechoka
kupigwa mishale, lazima sasa tuambiane ukweli," alisema Zitto.
Saa kadhaa baada ya hotuba yake hiyo, alisambaza tamko la maandishi ambalo lilibeba ujumbe unaofanana na ule alioutoa Kaliua.
Awali
katika mkutano wa Kaliua, Zitto alisema alikuwa hayuko tayari kuendelea
kukaa kimya pasipo kuchukua hatua zikiwamo za sheria wakati
akichafuliwa.
Alisema
alikuwa ameshamwandikia barua Katibu Mkuu wake, Dk. Willbrod Slaa
akihoji iwapo taarifa ya kumchafua iliyosambazwa katika mitandao ya
intaneti chini ya kichwa cha habari kisemacho, "Taarifa ya Siri ya
Chadema" ni ya chama hicho au la.
Zitto
aliyekuwa akizungumzia matokeo ya ziara yake ya kufuatilia fedha
zilizofichwa na baadhi ya Watanzania katika benki za Uswisi na
kwingineko Ulaya, alieleza kusikitishwa na kile alichodai kuwa ni
kikundi cha watu ndani ya Chadema ambacho kimekuwa mstari wa mbele
kumpaka matope.
"Wakati
nafanya kazi hii ya hatari ya kufuatilia hizo fedha zilizofichwa nje ya
nchi, navunjwa nguvu na watu ambao tuko chama kimoja kwani imekuwa ni
kawaida unapofanya siasa, lazima upate mashambulio na sasa nashambuliwa
na chama changu.
"Katika
hali ya kawaida, wenzagu tulionao katika chama ndiyo waliopaswa kunipa
nguvu kwa vile tuna kazi kubwa ya kupambana na 'lidude likubwa
linaloitwa CCM," alisema Zitto.
Bila
kutaja jina la mtu, alisema kuna watu wachache ambao hawana kazi ndani
ya chama hicho ambao shughuli yao imekuwa ni kugonganisha viongozi
wagombane.
Akirejea
historia ya kuchafuliwa kwake, Zitto alisema hali hiyo ilianza mwaka
2009 baada ya kujitokeza kutaka kugombea uenyekiti wa Chadema akichuana
na Freeman Mbowe.
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment