Maalim Seif awataka CUF kusahau ya Kiembesamaki!!

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF),Maalim Seif Sharif Hamad.
 
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amewataka wanachama na viongozi wa chama hicho wasivunjike moyo na matokeo ya uchaguzi mdogo wa jimbo la Kiembesamaki na badala yake waendelee na juhudi za kukiimarisha chama ili kiweze  kukamata dola katika uchaguzi mkuu wa mwakani.

Akifungua mkutano wa viongozi wa matawi, majimbo na wilaya katika wilaya za Wete na Micheweni, Maalim Seif alisema kilichotangazwa Kiembesamaki si matakwa ya wananchi kwa vile wananchi wa jimbo hilo walisusia uchaguzi huo.

 
Maalim Seif alisema idadi kubwa ya wapiga kura walioshiriki katika uchaguzi huo wa Jumapili ya wiki iliyopita, si wakaazi wa eneo hilo na kuwa  walichukuliwa katika maeneo ya mbali na kuwa wananchi waliwashtukia.

 “Kama kuna wananchi wa Kiembesamaki waliokwenda kupiga kura basi hawazidi elfu moja, wengi walichukuliwa katika maeneo tafauti kama vile Makunduchi, Mtende, Kitope na Bumbwini na wakapelekwa kupigakura huku wakilindwa na vikosi vya serikali,” alisema Maalim Seif.

Alisema kuna baadhi ya wananchi wa Kiembesamaki walipewa vitisho kabla ya kufanyika uchaguzi huo kwa kutumiwa ujumbe unaowaonya wasijitokeze kwenda kupiga kura, vinginevyo watapatwa na matatizo makubwa.

 
Katika uchaguzi huo mdogo wa Kiembesamaki ambao uliofanyika Februari 2, mwaka huu, baada ya aliyekuwa Mwakilishi wa jimbo hilo, Mansour Yussuf Himid kutimuliwa uanachama wa CCM, mgombea wa CCM, Mahmoud Thabit Kombo alitangazwa mshindi.

Akizungumzia Katiba Mpya, Maalim Seif amewahimiza wajumbe wa Bunge la Katiba kuweka kando maslahi ya vyama au makundi yao, badala yake wahakikishe Tanzania inakuwa na Muungano wa haki, ili Zanzibar  na Tanganyika kila upande uridhike kuwa unapata haki sawa na mwingine.

“Kwa upande wetu Wazanzibari tusisahau tuna kilio kikubwa cha miaka mingi kutotendewa haki ndani ya Muungano huu, wajumbe wote wajali maslahi ya Zanzibar na waweke pembeni maslahi binafsi au ya vyama vyao,” alionya Maalim Seif.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment