Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge akihojiwa kwenye Baraza la Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma |
Hata hivyo, Chenge, ambaye ni mhitimu wa Shahada
ya Umahiri wa Sheria kwenye Chuo Kikuu cha Harvard cha Marekani,
aliwasilisha amri ya zuio ya Mahakama Kuu inayokataza chombo chochote
cha Serikali kujadili sakata la escrow hadi hapo shauri lililopo
mahakamani litakapotolewa uamuzi, jambo lililozua mjadala wa kisheria na
kusababisha mwenyekiti wa Baraza la Sekretarieti ya Maadili, Jaji
Hamisi Msumi, kuahirisha hadi leo.
Chenge ni mmoja wa watu kadhaa wanaotarajiwa
kuhojiwa na kamati hiyo kutokana na kuhusishwa na kashfa ya uchotwaji wa
zaidi ya Sh306 bilioni kutoka kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow
iliyofunguliwa Benki Kuu kwa makubaliano kati ya Tanesco (shirika la
umeme la umma) na IPTL baada ya pande hizo mbili kutofautiana kuhusu
tozo za malipo ya umeme unaozalishwa na kampuni hiyo binafsi.
Mwingine ni mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Anna
Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na
ambaye pia aliingiziwa kwenye akaunti yake Sh1.6 bilioni zinazohusishwa
na akaunti hiyo ya escrow.
Wote wawili waliingiziwa fedha hizo na James
Rugemarila, mkurugenzi wa VIP Engineering iliyokuwa ikimiliki asilimia
30 ya hisa za kampuni ya IPTL.
Tangu sakata la escrow lianze, haikuwahi kuelezwa kuhusika kwa Chenge kwenye sakata hilo.
Lakini jana, akisoma hati ya malalamiko dhidi ya
mbunge huyo wa Bariadi, mwanasheria wa Sekretarieti ya Maadili, Hassan
Mayunga alisema mlalamikiwa, akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)
mwaka 1995, aliishauri Serikali kuingia mkataba wa miaka 20 na IPTL wa
kuongeza uzalishaji wa umme.
“Mlalamikiwa baada ya kustaafu wadhifa wa AG,
Desemba 24 mwaka 2005, mwaka 2006 aliingia mkataba wa kuwa mshauri
mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited iliyokuwa
inamiliki asilimia 30 ya hisa za IPTL,” alisema Mayunga akikariri hati
hiyo ya malalamiko.
“Kitendo cha mlalamikiwa kuingia mkataba na VIP
Engineering and Marketing Limited iliyokuwa na asilimia 30 ya hisa
kwenye kampuni ya IPTL ni ukiukwaji wa fungu la 6 (j) la Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma
kujinufaisha na utumishi wake uliopita kwa kutumia taarifa alizozipata
alipokuwa anatekeleza majukumu yake kwa manufaa binafsi.
“Kitendo cha mlalamikiwa kuendelea kuwa mshauri
mwelekezi wa kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited akiwa na
wadhifa wa ubunge ni ukiukwaji wa fungu la 6(e) la Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma ambalo linamzuia kiongozi wa umma kujiingiza katika
mgongano wa maslahi.”
Mwanasheria huyo aliendelea kusema kuwa mkataba
ambao mlalamikiwa aliingia na kampuni ya VIP Engineering and Marketing
Limited ulimpatia manufaa ya kifedha ya Sh1.617 bilioni kinyume na fungu
la 12(1)(e) la Sheria ya maadili ya viongozi wa umma. Aliongeza kuwa
mlalamikiwa hakutamka maslahi aliyokuwa nayo katika mkataba wa Tanesco
na IPTL kinyume na fungu 14 la sheria ya Maadili.
Aliongeza kuwa mlalamikiwa hakutamka madeni yake aliyokuwa
anaidai kampuni ya VIP Engineering and Marketing Limited kwa Kamishna wa
Maadili kinyume na matakwa ya fungu la 9(6)(b) la sheria hiyo.
“Malalamiko dhidi ya Chenge yanawasilishwa mbele
ya Baraza la maadili lenye mamlaka ya kisheria ya kufanya uchunguzi wa
kina na kumtaka mlalamikiwa kutoa maelezo bayana kuhusu mwenendo wake
kabla ya hatua nyingine kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria,” aliongeza.
Baada ya kusoma tuhuma hizo, Chenge alitoa amri
hiyo ya zuio la Mahakama Kuu ambayo pia iliwasilishwa kwenye Bunge la
Jamhuri ya Muungano kulizuia kujadili ripoti ya Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC) kuhusu sakata hilo la escrow, lakini ikagonga
mwamba baada ya wabunge na spika kulinda muhimili wao.
“Kwa kuwa amri hii ya mahakama nilikuwa sijaipata
na ninyi (wanasheria wa sekretarieti) mlikuwa mmeipata mapema ngoja
nikaisome na wenzangu,” alisema Jaji Msumi ambaye alikuwa akisaidiana na
wajumbe wawili, Selina Wambura na Hilda Gondwe.
“Kama kweli mahakama imezuia vyombo vyote, suala
hapa ni kuangalia amri hiyo. Tupeni muda tukaangalie na kesho (leo)
tutatoa uamuzi kama tutaendelea au la.”
Kabla ya kuahirisha shauri hilo ulizuka mvutano mkubwa wa kisheria kuhusu amri hiyo ya zuio la mahakama.
“Suala hili ninavyofahamu mimi liko mbele ya
Mahakama Kuu, hivyo tusubiri uamuzi wa mahakama kwani amri ya mahakama
ilizuia vyombo vyote vya Serikali na hiki (Baraza la Maadili) ni chombo
cha serikali. Mwenyekiti, mimi nataka kupata mwongozo wa suala hili,
tukiendelea bila kupata mwongozo na mimi kama mwanasheria litanisumbua
sana,” alisema Chenge ambaye alikuwa Mwanasheria wa Serikali kati ya
mwaka 1972 na 1973.
Lakini Mayunga alisimama na kusema: “Mheshimiwa
mwenyekiti, hii amri ya mahakama ambayo mlalamikaji (Chenge) ameitoa
hapa, si Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inayohusika kama
mlalamikiwa alivyotaja.
“Tuhuma ambazo zimeletwa hapa ni tuhuma za
uvunjifu wa maadili ya viongozi wa umma na wala siyo suala
lililoonyeshwa katika hii amri... ni tofauti kabisa.”
Mayunga, katika kujenga hoja, alisoma Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 Ibara 132 (1) ya inayosema
kuwa “kutakuwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambayo
itakuwa na mamlaka ya kuchunguza tabia na mwenendo wa kiongozi wa umma
yeyote kwa madhumuni ya kuhakikisha kwamba masharti ya Sheria ya Maadili
ya Viongozi wa Umma yanazingatiwa ipasavyo”.
Pia alisoma fungu la 18 (2) (c) la sheria hiyo
linaloipa Sekretarieti ya Maadili mamlaka ya kuchunguza tuhuma yoyote ya
kuvunjwa kwa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma na viongozi wote wa
umma, wanaopaswa kuwajibika chini ya sheria hiyo.
“Kutokana na sheria hii, Sekretarieti haizuiwi kuendelea na
shauri hili. Madai dhidi ya mlalamikiwa ni ya jinai na rushwa. Hapa
tunajikita katika maadili wala sisi hatuzungumzii escrow, hapa ni
maadili kuwa amepokea fedha kutoka VIP Engineering,” alisema Mayunga
Jaji Msumi alisema hati hiyo aliipitia haraka haraka na akahoji kama ina amri inayozuia suala hilo kujadiliwa.
Chenge alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti, hoja
ambayo nimeileta mbele yako ni zuio la mahakama. Kueleza kwamba chombo
hiki kiko juu ya mahakama bila...”
Kabla ya kumalizia sentensi hiyo alisimama
mwanasheria wa Sekretarieti hiyo, Filotheus Manula na kusema: “Kauli
anayoisema mlalamikakiwa kuwa chombo hiki kiko juu ya mahakama siyo
sahihi. awali Mayunga alishaelezea. Katiba na Sheria ya Maadili na iko
wazi.”
Lakini Chenge akasema: “Ni vizuri vijana
wakajifunza... amri hii ya mahakama siyo maoni yangu, hivyo ni vyema
ikaheshimika. Itanisumbua mimi, mamlaka ya chombo hiki isitishwe siyo
kwamba haina mamlaka, mnaweza kuendelea sawa, lakini hili ni ombi langu.
“Utawala wa sheria ni bora ukaheshimiwa na masuala ya siasa tuache tukapige siasa majukwaani.”
Mayunga alisimama na kusema: “Mheshimiwa
mwenyekiti ukiruhusu hiki anachokisema au uhalisia wa kuzuia
kinachoendelea, siyo sahihi.”
Chenge alijibu, “mheshimiwa mwenyekiti amri ya
mahakama ni (inahusu) taarifa ya ukaguzi wa miamala ya akaunti ya Tegeta
Escrow ya (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) CAG, na
malalamiko yanayoletwa dhidi yangu ndiyo ambayo yamezuiwa... mimi
ninachoomba ni ufafanuzi au mwongozo kwa hili.”
Lakini Manula alipinga akisema: “Penal Code
(Sheria ya Kanuni ya Adhabu) haitumiki hapa. Mlalamikiwa ndiye aliyekuwa
AG, alisimamia kuitunga... madai, jinai na rushwa, lakini hapa
tunajadili maadili na siyo escrow.”
Chenge, aliyekuwa amesimama wakati wote,
aliendelea na msimamo wake wa kuomba mwongozo, hali iliyomfanya
mwanasheria mwingine wa sekretarieti hiyo, Getiruda Cyriacus kusimama na
kunukuu fungu la 18 (4) la sheria hiyo linalosema sekretarieti itakuwa
na mamlaka ya kuanzisha na kufanya uchunguzi wowote kuhusu ukiukwaji wa
maadili yaliyotajwa katika sheria hiyo.
Chenge aliingia kwenye viwanja vya Ukumbi wa
Karimjee saa 3:02 asubuhi akiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruizer
akiongea na simu na aliposhuka, aliwaambia waandishi wa habari waliokuwa
wakimpiga picha akisema: “Nendeni mkauze magazeti na sura ya Chenge.”
Alipotaka kuingia ukumbini, aliambiwa asubiri kwenye viti,
lakini aligoma na badala yake alishuka chini na kuanza kuzungumza na
simu huku akizungukazunguka takribani dakika 10 kabla ya kutakiwa
kuingia ukumbini saa 3:13 asubuhi.
Mara baada ya Jaji Hamis kuahirisha baraza hilo
saa 3:55, waandishi walianza tena kumpiga picha na kama kawaida alisema:
“Nendeni mkaandike mnavyoona... mnataka na mgongo muupige picha?”
Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari
walipotaka kufanya naye mahojiano ya suala hilo alijibu, “siwezi
kuzungumzia chochote kuhusu yaliyopo katika maadili” na kupanda gari,
kisha akaondoka
0 comments:
Post a Comment