VPL YAPISHA MECHI YA U20 WANAWAKE
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) imefanya marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) ili kupisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya
Tanzania na Msumbiji.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya kwanza
kwa mashindano ya wanawake wenye umri chini ya miaka 20 itachezwa
Jumamosi (Oktoba 26 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia
saa 10 jioni.
U20 tayari imehamishia kambi yake
hosteli ya Msimbazi Center, Dar es Salaam kutoka JKT Ruvu mkoani Pwani
tangu wiki iliyopita kujiandaa kwa mechi hiyo. Fainali za Kombe la Dunia
kwa U20 wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada.
Marekebisho ya ratiba ya VPL yamegusa
raundi zote tatu zilizobaki kukamilisha mzunguko wa kwanza. Kutokana na
marekebisho hayo mechi za raundi ya 11 zitakuwa ifuatavyo; Oktoba 28
mwaka huu ni Coastal Union vs Mtibwa Sugar, Oljoro JKT vs Ashanti
United, Ruvu Shooting vs Kagera Sugar na Simba vs Azam. Oktoba 29 mwaka
huu ni Tanzania Prisons vs Mbeya City, Yanga vs Mgambo Shooting na Rhino
Rangers vs JKT Ruvu.
Raundi ya 12 ni kama ifuatavyo; Oktoba
31 mwaka huu ni Simba vs Kagera Sugar, Novemba 1 mwaka huu ni JKT Ruvu
vs Yanga. Novemba 2 mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Coastal Union,
Tanzania Prisons vs Oljoro JKT, Azam vs Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar vs
Rhino Rangers na Mbeya City vs Ashanti United.
Raundi ya 13 ni kama ifuatavyo; Novemba 6
mwaka huu ni JKT Ruvu vs Coastal Union, Ashanti United vs Simba, Kagera
Sugar vs Mgambo Shooting, Rhino Rangers vs Tanzania Prisons na Ruvu
Shooting vs Mtibwa Sugar. Novemba 7 mwaka huu ni Azam vs Mbeya City.
Mechi za kufunga raundi ya 10 zitachezwa
keshokutwa (Oktoba 23 mwaka huu) kama ratiba inayoonesha. Mechi hizo ni
kati ya Coastal Union vs Simba, Tanzania Prisons vs Kagera Sugar na
Yanga vs Rhino Rangers.
MECHI YA SIMBA, YANGA YAINGIZA MIL 500/-
Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ya
watani wa jadi Simba na Yanga iliyochezwa jana (Oktoba 20 mwaka huu)
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa sare ya mabao
3-3 imeingiza sh. 500,727,000.
Washabiki 57,422 ndiyo waliokata tiketi
kushuhudia pambano hilo namba 63 kwa viingilio vya sh. 5,000, sh. 7,000,
sh. 10,000, sh. 15,000, sh. 20,000 na sh. 30,000.
Ni tiketi 131 tu ndizo hazikuuzwa ambazo
ni 90 za VIP A, 40 za VIP B na moja ya VIP C. Tiketi zilizochapwa kwa
ajili ya mechi hiyo ni 57,558 ambayo ndiyo idadi ya viti vilivyopo
kwenye uwanja huo.
Kila klabu imepata mgawo wa sh. 123,025,564.32 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 76,382,084.75.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni
asilimia 15 ya uwanja sh. 62,555,371.69, tiketi sh. 7,309,104, gharama
za mechi sh. 37,533,223.01, Kamati ya Ligi sh. 37,533,223.01, Mfuko wa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 18,766,611.51 na Chama cha Mpira
wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 14,596,253.39.
VITAMBULISHO MICHUANO YA CHALENJI
Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu
Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefungua maombi ya vitambulisho
(Accreditation) kwa ajili ya waandishi wa habari wanaotarajia kuripoti
mashindano ya Kombe la Chalenji.
Mashindano ya Kombe la Chalenji
yatafanyika nchini Kenya kuanzia Novemba 27 hadi Desemba 12 mwaka huu.
Kwa waandishi wa habari wanaotaka kuripoti mashindano hayo wanatakiwa
kutuma maombi yao kabla ya Oktoba 31 mwaka huu.
Mbali ya majina, katika maombi hayo
mwandishi wa habari ni lazima aoneshe chombo anachofanyia kazi na
kuambatanisha na picha moja ya pasipoti.
Boniface Wambura Mgoyo
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
POSTED BY:www.info@dirayetu.blogspot.com
0 comments:
Post a Comment