Picha kutoka maktaba ikionyesha baadhi ya wapagazi wakiwa na watalii |
MGOMO uliotangazwa na Chama cha Wapagazi Tanzania (TPO) wa kugoma kutoa huduma kwa watalii katika Mlima Kilimanjaro na
Mlima Meru, umeanza kuwaumiza vichwa mawakala wa shuguli za utalii katika mikoa hiyo huku wakidai kuwa mgomo huo ni batili.
Mawakala hao wanaofanya shughuli za utalii katika milima hiyo mkoani
Arusha, wamelazimika kutoa taarifa ya kupingana na mgomo huo kupitia
Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Utalii Kilimanjaro (KIATO).
Hata hivyo, kauli ya KIATO inatolewa wakati tayari kukiwa na tangazo
la serikali namba 228 la Juni 29 mwaka 2009 likielekeza juu ya malipo ya
dola 10 kwa wapagazi kwa siku kulingana na mabadiliko ya fedha za
kigeni kwa siku hiyo.
Mbali na tangazo hilo pia kauli ya KIATO inapingana na Shirikisho la
Mawakala wa Utalii Tanzania (TATO) ambao wanaonekana kukubaliana na
madai ya wapagazi ya malipo ya si chini ya dola 10 kutokana na
uthibitisho wa barua yao iliyosainiwa na Katibu Mtendaji wake, Sirili
Akko, ikiwambusha juu ya tangazo hilo la serikali.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, KIATO kupitia katibu wake,
Paul Mgana, bila kuonyesha mgomo huo ni batili kwa namna gani,
ilikirushia shutuma chama cha wapagazi Tanzania huku ikidai kuwa ni
chama kipya ambacho kimeanzishwa kikiwa na mkakati wa kuvuruga utalii
wa milima.
Mgana alisema wao kama KIATO waliitisha mkutano na vyama vingine
ambavyo wananchama wake wanajishughulisha na Mlima Kilimanjaro na Mlima
Meru na kwamba TPO hawakutokea, licha ya kwamba walipatiwa mwaliko kwa
njia ya simu.
Alisema katika kikao hicho kwa pamoja walikubaliana kila chama kikae
na wanachama wake kufikisha mapendekezo ya kila upande na kuelezea
umuhimu wa pande zote kuondoa jazba na kuwa na majadiliano yenye kuleta
tija kwa pande zote.
"Tulikubaliana pia kile kiwango cha shilingi 10,000 ambacho
kilipendekezwa na KIATO ndicho kiendelee kutumika kwa sasa kama kiwango
cha chini kabisa na wenye uwezo zaidi na waliokuwa wakilipa sh 15,000
na kuendelea waendelee vile vile," alisema Mgana.
Alisema mazungumzo na vyama vingine bado yanaendelea bila uwepo wa
TPO na kwamba chama hicho kinaonekana kutotaka mazungumzo huku
kikilazimisha kiwango wakitakacho bila ya majadiliano na kutaka
kujiendesha kisiasa.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment