Rais Jakaya Kikwete (kushoto) akimsikiliza Mwenyekiti wa Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD), James Mbatia siku za hizi karibuni. Picha na
Maktaba
Dar es Salaam. Kauli
ya Rais Jakaya Kikwete ya kuwataka wanachama, wadau na makada wa CCM,
kuondokana na unyonge, imepokewa kwa hisia tofauti huku ikielezwa kuwa
ni ya vitisho.
Juzi, wakati akifungua Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma,
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho tawala alisema: “Ni
wakati wa kuacha unyonge na uvumilivu una kikomo chake.”
Alisema CCM inaingia kwenye uchaguzi huku ikishindana na wagomvi:
“...Ugomvi ndiyo sehemu ya mwongozo wao kufanya siasa,” alisema Kikwete
bila kutaja jina la chama chochote cha siasa.
Alisema amechoshwa na vitendo vya ugomvi huku akitolea mfano wa tukio la
Kahama mkoani Shinyanga ambako kijana mmoja alitolewa macho kwa
bisibisi na mwingine kumwagiwa tindikali katika uchaguzi mdogo wa ubunge
Igunga, mkoani Tabora.
Akizungumza kwa simu jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alieleza
kushangazwa kwake na kauli ya Rais Kikwete akisema: “Nimeipokea kwa
mshtuko na ninawataka wafuasi wa chama changu kuwa watulivu na kuchukua
tahadhari kubwa.”
“Nilichokifanya ni kuwaagiza wafuasi wa Chadema kufanya kampeni za
kistaarabu kwa kutolipiza kisasi ili kuhakikisha kwamba hakuna damu ya
Mtanzania itakayomwagika Kalenga,” alisema.
Hatua ya Rais Kikwete, imekuja baada ya CCM kumtangaza, Godfrey Mgimwa
kuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Kalenga. Mgimwa ni mtoto wa aliyekuwa
mbunge wa jimbo hilo, ambaye pia alikuwa Waziri wa Fedha, hayati Dk
William Mgimwa aliyefariki mwezi uliopita nchini Afrika Kusini.
Mgombea huyo atachuana na mgombea wa Chadema, Grace Tengega.
Jana, Mbowe alisema ingawa Kikwete ni Mwenyekiti wa CCM, alitakiwa
kufahamu kwamba ni kiongozi wa nchi na ni Amiri Jeshi Mkuu ambaye vikosi
vya Ulinzi na Usalama vipo chini yake.
“Anapotoa kauli nzito kama hiyo, inatakiwa afahamu kwamba yeye si
Mwenyekiti wa CCM tu, bali ni Rais na Amiri Jeshi Mkuu, hakustahili
kutoa kauli kama hiyo inayoweza kuamsha hisia,” alisema Mbowe.
Alisema kauli zake za kiitikadi za kupendelea chama chake wakati
akifahamu kuwa yeye ni kiongozi wa Watanzania wote, zinawafanya wananchi
wagawanyike kwa misingi ya vyama.
“Rais Kikwete anadai kwamba mtu wao alimwagiwa tindikali na mwingine
kutolewa macho kwa bisibisi, lakini hazungumzii viongozi na wanachama wa
Chadema waliouawa kwa kupigwa risasi na wengine kwa mabomu. Anasema
hayo huku akifahamu fika kwamba kuna vyombo vya dola na Mahakama ambavyo
vinashughulikia matukio hayo.”
Mbowe alidai kuwa Juni 15, 2013 wakati akifunga kampeni za udiwani
mkoani Arusha, alirushiwa bomu la kivita na kusababisha vifo vya watu
wanne lakini uongozi wa chama hicho ulipomwomba Rais aunde tume huru ya
kimahakama hakuna kilichofanyika.
“Tumemwomba mara kadhaa Rais Kikwete kuunda tume huru ya kimahakama ili
kuchunguza mauaji ya viongozi na wanachama wa Chadema ambayo yamekuwa
yakitokea, lakini hakuna kilichofanyika,” alisema Mbowe ambaye ni pia
kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
Alisema: “Rais Kikwete anasema wamekubaliana kwenye Halmashauri Kuu (ya
CCM) kuacha unyonge, Halmashauri Kuu ina viongozi wote wakuu wa nchi,
wanakubaliana kuwatenga wananchi kwa kufuata itikadi za chama chao, hii
ni hatari.”
Mbowe alisema kauli ya Rais Kikwete inafanana na ile ya Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda aliyoitoa bungeni ya kuwataka askari polisi kuwapiga raia
kwa wale wasiotaka kutii amri halali.
Mbatia ataka ufafanuzi
Akizungumzia kauli hiyo, Mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania
(TCD), James Mbatia alisema ameshtushwa na kauli ya Rais Kikwete na
kumtaka kuitolea ufafanuzi ili kuondoa mgawanyiko katika jamii.
Alisema kauli ya ‘unyonge CCM sasa basi’ haikupaswa kutolewa naye hasa
ikizingatiwa kwamba ndiye kiongozi mkuu wa nchi ambaye vyombo vya ulinzi
na usalama viko chini yake.
“Ni kama amevielekeza vyombo vya ulinzi na usalama kuchukua hatua kali
dhidi ya vyama vingine vya siasa, ninamwomba alitolee ufafanuzi suala
hili kabla halijaleta madhara kwenye jamii,” alisema Mbatia.
CUF yahofia Kalenga
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro alisema kauli ya Kikwete
inaashiria kuwa kutakuwa na matumizi makubwa ya vyombo vya dola katika
uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga.
“Ninavyofahamu siyo kwamba anawaagiza wafuasi wa CCM kuacha unyonge na
kuchukua hatua, bali anavielekeza vyombo vya dola kutumia nguvu kubwa
zaidi,” alidai.
Mtatiro alisema anashangaa kauli ya namna hiyo kutolewa na Rais wakati ndiye anayetakiwa kuhubiri amani na kuvumiliana.
Akizungumza suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,
Bashiru Ali alisema wananchi wanatakiwa kuwa makini na kauli za
wanasiasa zenye kujenga chuki.
“Vijana tusipigane kwa kugombanishwa na wanasiasa, tofauti zetu za
kiitikadi zisitufanye tugombane kwani malengo ya wanasiasa ni kutoa
kauli zenye utata kwa lengo la kupata kura, matatizo yetu
yatuunganishe,” alisema Bashiru.
0 comments:
Post a Comment