Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Dk Thomas Kashililah |
Akizungumza na gazeti hili jana katika Ofisi za
Bunge mjini hapa, Katibu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Dk Thomas
Kashililah, alisema Bunge limechukua hatua hiyo baada ya Mweta kuwajibu
kuwa fedha walizompatia alikuwa ameshazitumia.
“Yeye (Amina Mweta), ni mwajiriwa wa Halmashauri
ya Mwanga, tulichokifanya ni kumwandikia barua mwajiri wake ili akatwe
katika mshahara wake,” alisema na kuongeza: “Atajua mwenyewe kama
atalipa kwa kukatwa kidogo kidogo ama yote, lakini lazima ailipe posho
hiyo aliyoichukua, kwa sababu alichukua na kuweka sahihi.”
Gazeti hili lilikuwa la kwanza kuripoti baada ya
kutokea utata huo wa majina mawili ya wajumbe kufanana huku ikielezwa
kuwa wote walikuwa wamesaini fomu za fedha za posho ya kujikimu ya
Sh80,000 kwa siku kwa muda wa siku 13 unaomalizika Februari 28 mwaka huu
ikiwa na maana kwamba kila mmoja alilipwa Sh1,040,000.
Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel, awali, alipoulizwa kuhusu utata huo alisema mjumbe halali ni yule aliyetoka Songea.
Hata hivyo, alisema kinachowashangaza ni kwamba
yule mwenzake wa Mwanga alipotakiwa kurudisha fedha alizopewa kimakosa
alisema ameshatumia sehemu kubwa na kubakiza Sh50,000 tu.
Akizungumza na gazeti hili, Mweta kutoka Mwanga
alisema alipigiwa simu na Ofisi ya Bunge Maalumu la Katiba na kupongezwa
kwa kuteuliwa na Rais kuwa mjumbe. “Mimi ni personal secretary (katibu
muhtasi) wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga na nilipigiwa
simu na Ofisi ya Bunge wiki iliyopita nikipongezwa kwa uteuzi huo,”
alisema.
Alisema alipofika na kujisajili baada ya kutoa
kitambulisho chenye jina lake, alipewa kitambulisho na kisha kupewa
malipo yake ya posho.
Naye Mweta kutoka Songea alisema alipigiwa simu na
Katibu Mkuu wa COTWU kwamba aliteuliwa na Rais kuwa mjumbe na kutakiwa
kuripoti bungeni.
Tayari Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta)
limeeleza kusikitishwa na utata wa watu hao wawili wenye majina
yanayofanana kuwasili katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma kwa
nafasi ya ujumbe wa Bunge hilo, huku likisema halimfahamu Amina Mweta wa
Kilimanjaro.
Katibu Mkuu wa Tucta, Nicholaus Mgaya mapema
alikaririwa na gazeti hili akisema kuwa mazingira ya tukio hilo
yamewatisha, hivyo kulazimika kumwandikia barua Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue ili kumthibitisha mjumbe wao halali.
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment