PITIA HISTORIA YA GWIJI WA VICHEKESHO "'MZEE SMALL"!!



IKIWA bado anga la sanaa nchini limegubikwa na hali ya sintofahamu kufuatia vifo vya waigizaji Adam Kuambiana, Sheila Haule ‘Recho’ na George Tyson, pigo lingine limetokea baada ya gwiji la vichekesho nchini, Said Ngamba ‘Mzee Small’ kuaga dunia mwishoni mwa wiki iliyopita.
Gwiji la vichekesho nchini, Said Ngamba ‘Mzee Small’ enzi za uhai wake.
Ni vigumu sana kuipokea taarifa ya msiba huo mzito lakini hakuna jinsi, yatupasa kushukuru kwa kila jambo. Sisi sote ni wa mavumbi, mavumbini tutarejea.

Mzee Small ni miongoni mwa wasanii wa kwanza kabisa kuanzisha sanaa ya vichekesho. Alianzia katika vichekesho vya majukwaa, kipindi hicho alikuwa na mwenzake Said Seif ‘Unono’ ambaye sasa ni marehemu, walipambana hadi kuisimamisha sanaa hiyo.
Mzee Small akiwa na wanahabari wa Global Publishers.
Miaka ya 90 ambayo Mzee Small na wenzake wakihangaika huku na kule kuchekesha watu katika majukwaa mbalimbali mitaani, hawakuwa wakipata kitu, hawakutarajia kama inaweza kufika wakati sanaa ikawa dili na msanii kuweza kujiingizia kipato kikubwa.

Kadiri siku zilivyozidi kuyoyoma, taratibu mzee Small na wenzake wakaanza kuona mwanga wa mafanikio.

Mzee Small akiwa na mke wake katika picha ya pamoja enzi za uhai wake.
Serikali ilimchukua Mzee Small na baadhi ya wasanii wenzake katika mashirika kama Reli na NASACO, ikawatumia katika kampeni mbalimbali za kijamii. 

Alizunguka karibu mikoa yote, nchi nzima ikamjua kupitia vichekesho vyake.
Kutokana na gwiji huyo kutumiwa sana na serikali na katika vikundi mbalimbali vya jeshi, kuna wakati Mzee Small alilazimika kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwani kila ambaye alifanya sanaa jeshini alitakiwa kupitia mafunzo ya kijeshi.
Mzee Small alipokuwa mzigoni na msanii Kingwendu.
Ingawa hakumaliza mafunzo, sanaa kwake ilikuwa katika damu. Alijifunza vitu vingi akiwa jeshini hadi pale teknolojia ya michezo ilipohamia katika redio na televisheni.

Hapo ndipo moto wa vichekesho ulipokolea, gwiji huyo pamoja na mkongwe mwenzake, Chausiku Salum ‘Bi Chau’ wakaanza kung’ara ambapo walifanya vizuri katika michezo kama 50, 50, 100, na ule wa Mjini Shule uliomwelezea mwanamke wa kijijini aliyeolewa mjini.


Marehemu mzee Small akiwa hospitalini.
Mzee Small alikuwa miongoni mwa wasanii wa kwanza kabisa kuibadilisha michezo ya runingani na kuiweka katika mfumo wa mikanda ya video (VHS). Mikanda yao ilipendwa sana hasa kutokana na mchanganyiko wake na Bi Chau ambaye alikuwa akiigiza kama mkewe katika mikanda mbalimbali.

Mwanga wa mafanikio ulizidi kuonekana, Mzee Small alikuwa ndiye mmiliki wa kundi la sanaa linalojulikana kama Afro-Dance ambalo alilisajili mwaka 1994 kwenye Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na kutoa ajira kwa vijana wa mitaani.


Komedi ya Mzee Small haikuwa katika michezo tu, katika maisha yake ya kawaida pia alikuwa mtu wa vichekesho sana. Kwa majirani ambao waliishi na nguli huyo  Tabata- Mawenzi, hakika ni mashahidi katika hili.

Alikuwa ni mtu wa kupenda utani, ukimkuta na watoto, vijana na hata watu wazima yeye ni kuwachekesha tu. Si mtu wa kukasirika. Maisha yake yote yeye alikuwa mtu wa kufurahi na kuwafurahisha wengine.

Legendary huyo alivuka mipaka zaidi kuendana na teknolojia, alichangia kuiendeleza sanaa katika mfumo wa DVD kutoka katika VHS. Makampuni mbalimbali yakaanza kujitokeza kumtumia kama balozi katika kutangaza bidhaa zao.


Mkali huyo ambaye kupitia sanaa aliweza kununua kiwanja na kujenga nyumba yake, alichangia kuwatoa wasanii wengi kufanya sanaa wakiwemo hawa wanaondelea kutusua kwa sasa katika soko la filamu.

Mbali na maisha ya uigizaji, katika maisha binafsi, mzee huyo alikuwa mtu wa watu kwa namna alivyokuwa akijitoa kwa ndugu na jamaa wanaomzunguka. Ilikuwa ni vigumu sana kumkosa Mzee Small katika shughuli zozote za majirani zake.

Uwezo wake kisanaa ulianza kushuka mwaka 2012 baada ya kupata ugonjwa wa kiharusi. Muda mrefu akawa mtu wa kuugua hadi mauti yalipomkuta Juni 7, mwaka huu.

Ni ngumu sana kuulezea mchango wake kwa msanii mmojammoja lakini kimsingi amewagusa wasanii wengi kisanaa, ataendelea kukumbukwa kama muasisi wa vichekesho na sanaa kwa jumla.

Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi. Amina.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment