MWENYEKITI
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amemvaa
Rais Jakaya Kikwete, akimtaka kuacha kutafuta huruma ya Watanzania juu
ya suala la Katiba na badala yake atumie nafasi hiyo kuwataka wabunge
wake kuheshimu maoni ya wananchi.
Mbowe
ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisema kuwa
hotuba ya Rais Kikwete juzi kwamba Katiba haiwezi kupatikana kwa ngumi
imejaa upotoshaji kwa wananchi.
Katika
hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 37 ya kuzaliwa kwa CCM,
yaliyofanyika mkoani Mbeya, Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa
CCM, alimshangaa Mbowe kwa kauli yake kwamba mfumo wa serikali tatu
ukikataliwa katika Bunge hilo nchi haitatawalika.
“Huku
ni kuwadanganya wananchi, pale hakuna ngumi wala vurugu yoyote, kila
ibara iliyopo katika rasimu itajadiliwa ili upatikane mwafaka. Huku ni
kukosa ukomavu wa kisiasa,” alisema.
Akizungumza
na Tanzania Daima jana, Mbowe alisema ni vema Rais Kikwete akaacha
kuhangaika na wapinzani, badala yake awe tayari kuheshimu mawazo ya
wananchi waliyotoa wakati wa kutoa maoni ya Katiba.
Mbowe
alisema kuwa Rais Kikwete ni mwanasiasa na mtu anayejaribu kupotosha
hoja, kwani CHADEMA waliposema watapambana, hawakumaanisha kupigana
ngumi kama alivyosema kiongozi huyo.
Alisema
kuwa viongozi wa CCM wamekuwa wakilazimisha ajenda ya Katiba mpya
kuonekana kama sera yao, jambo ambalo CHADEMA haiwezi kuafiki.
“Katiba
ni ya wananchi, si ya chama chochote cha siasa, ndiyo maana hatukubali
kuona mawazo ya wananchi yakishindwa kuheshimiwa,” alisema.
Mwenyekiti
huyo alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph
Warioba imefanya kazi nzuri ambapo Rais Kikwete na wabunge wake
wanapaswa kuheshimu mchango huo.
Alisema
kuwa CHADEMA itahakikisha inashindana kwa hoja katika Bunge la Katiba
litakaloketi hivi karibuni na iwapo hilo litashindikana watarudi kwa
wananchi ambao ndio wenye uamuzi wa mwisho juu ya suala hilo.
“Wajumbe
watakaoshiriki Bunge la Katiba ni 640 ambao hao si waamuzi wa mwisho na
kama tutaona kuna suala lolote linaloenda kinyume, sisi
tutakachokifanya ni kurudi kwa wananchi kuwaeleza juu ya kilichotokea na
hao ndio wenye maamuzi ya mwisho katika kura ya maoni,” alisema.
Mbowe
alisema kuwa hata katika kushindana kwa hoja CCM wanapaswa wasiweke
hila, maana wataweza kuchangia mchakato huo kushindwa kufanikiwa.
Alisema
kuwa nia ya CHADEMA ni kuhakikisha Katiba nzuri, bora na iliyo ya
wananchi inapatikana na si kusababisha vurugu kama ambavyo Rais Kikwete
amejaribu kupotosha.
“Hila
hiyo imeonekana wazi maana kuna hali ya kutaka kupuuza mawazo ya
wananchi na CCM kulazimisha mawazo yao, hilo hatutalikubali na
tutapambana…hiyo si mara ya kwanza kupambana katika suala hilo,”
alisema.
Mbowe
alisema kuwa kuhusu serikali tatu ni muhimu Rais Kikwete akaheshimu
mawazo hayo na CHADEMA itashindana kwa hoja juu ya suala hilo ili
kuhakikisha mawazo hayo yaliyowasilishwa na Jaji Warioba yanaheshimiwa.
Katika
ziara ya mikutano ya hadhara ya CHADEMA iliyopewa jina la Operesheni
M4C Pamoja Daima, Mbowe na viongozi wengine waliionya Serikali ya CCM
kutochakachua mchakato wa Katiba, kwani Watanzania hawako tayari kurudi
kwenye Katiba ya sasa ambayo alidai imekosa uhalali wa kuongoza nchi.
Alisema
CCM kwa kutumia wabunge wake wakiamua kuhujumu mchakato huo bungeni,
yeye na viongozi wenzake watapita nchi nzima kuwataka wananchi
wasishiriki kura za maoni na yuko tayari kufunguliwa kesi kwa kudai
Katiba mpya.
0 comments:
Post a Comment