WATUMISHI MAMLAKA YA BANDARI (TPA) WATAADHARISHWA!!


WAZIRI wa Uchukuzi, Bw. Samuel Sitta, amewatahadharisha watumishi wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA) waliombeza aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Bw. Harrison Mwakyembe akiwataka wasijidanganye na kujiona wamepona.

Alisema ataendeleza makali na wembe ule ule alioutumia Dkt. Mwakyembe kwa watumishi wanaokiuka maadili, wasiojituma kazini, wadokozi, wezi wa vifaa vya magari, kontena kwani hayupo tayari kufanyakazi na watumishi wa aina hiyo.

Bw. Sitta aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipoitembelea Mamlaka hiyo ili kupata taarifa ya utendaji wa kazi.

"Kwanza nampongeza mdogo wangu ambaye tupo kama mapacha (Dkt. Mwakyembe), kwa utendajikazi wake ni wa hali ya juu...kilichonishangaza baada ya kuhamishwa Wizara kuna watu walifanya sherehe...hivi unafanya sherehe unajua huyo anayekuja yukoje," alihoji na kuongeza;

"Sasa nimekuja mimi ambaye sina tofauti naye ingawa mimi ni mkali zaidi yake lakini napenda niwaeleze wazi kwamba, ili tupige hatua katika kipindi hiki, sitakubali kufanyakazi kwa kutishana wala majungu...yeyote ambaye atalegalega ataniona mbaya.

"Umefika wakati wa Mkurugenzi kutolimbikiziwa majukumu, kila aliyepewa madaraka anastahili kutoa maamuzi ili mradi yasiwe ya uchochezi, uchonganishi wala majungu...fanyeni kazi kama timu kwani imebaki miezi 10 ili kubadilisha uongozi," alisema.

Bw. Sitta alisema, matatizo yaliyopo yasemwe ili yaweze kufanyiwa kazi kwani TPA inafanyakazi katika ushindani hivyo lazima wafanyakazi wake washirikiane ili kufanikisha jukumu walilonalo kwa kila idara.

Alisema Serikali inaitegemea sana bandari hivyo mtumishi yeyote ambaye atajihusisha na wizi, uhujumu uchumi wa bandari atachukuliwa hatua bila kujali nafasi aliyonayo pamoja na kufunguliwa mashtaka.

Aliutaka uongozi ulioko madarakani kuwa wabunifu, kutoogopa kuitwa wala rushwa bali waendelee kujituma na kama wataitwa wala rushwa wakati wao hawafanyi hivyo wasiwe na wasiwasi wowote.

"Watanzania tuna tatizo la woga na kutojiamini, hii ni karne ya 21 kila mtu abadilike, aende na wakati ili kufikia malengo...tatizo la viongozi kukaimu nafasi mbalimbali sijapendezwa nalo, wekeni vijana wafanye kazi na kutoa maamuzi sahihi," alisema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Mhandisi Madeni Kipande, alisema awali mamlaka hiyo ilikuwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya wizi wa makontena, vifaa kwenye magari lakini miaka miwili iliyopita, wizi huo umeisha na atakayebainika kufanya hivyo sheria itachukua mkondo wake.

Alisema ipo changamoto ya miundombinu ya zamani katika sekta ya usafiri wa reli na kusababisha utendaji hafifu ambao unachangia mizigo mingi kusafirishwa kwa njia ya barabara.

"Pia tuna uhaba wa ardhi kwa ajili ya upanuzi wa bandari kwa mfano, ujenzi wa gati 13/14 unahitaji kujengwa upande wa pili ambako kuna eneo la Jeshi ili kuruhusu meli kubwa kupita," alisema Kipande.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment